Askofu Mwaikali: Hakuna mbadala wa Tanzania

Askofu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) Nyanda za Juu Kusini Dk Edward Mwaikali. Picha na Saddam Sadick
Muktasari:
- Askofu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) Nyanda za Juu Kusini, Dk Edward Mwaikali amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa jumla
Mbeya. Askofu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) Nyanda za Juu Kusini, Dk Edward Mwaikali amesema muda wa kuliombea Taifa kuendelea kuwa salama ni sasa kutokana na tukio kubwa la uchaguzi mkuu linalotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Amewaomba Wakristo, wakiwamo waumini wa Usharika wa Ruanda, jijini Mbeya kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu kugombea urais, ubunge na udiwani kwa vyama ambavyo havijaweka ukomo katika nafasi hizo.
Ametoa wito huo leo Aprili 20, 2025 wakati wa ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Usharika wa Ruanda.
Dk Mwaikali amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa jumla.
Amesema ukiwa mwaka wa uchaguzi mkuu, kila mmoja anapaswa kuwa mbele kutetea amani kama ilivyo kwa mzazi, hasa mama kwani yakitokea machafuko Tanzania, hakuna Taifa mbadala.
"Huenda akatokea baba mbadala lakini siyo mama mbadala, kwa maana hiyo amani ya nchi yetu ikitoweka hatutapata mbadala wa nchi nyingine. Niombe viongozi wa dini na Wakristo wote tuendelee kuliombea Taifa letu na mwaka huu ndiyo wa uchaguzi mkuu.
"Hii amani iliyopo viongozi wa Serikali wamejitahidi sana, lakini isitoshe watumishi wa Mungu wa dini zote wamehusika. Tushikilie sana amani yetu tuvuke kwa pamoja, tusijifananishe na baadhi ya mataifa ambayo vita na migogoro imetawala," amesema.
Amesema Wakristo wanapaswa kujitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.

Askofu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) Nyanda za Juu Kusini Dk Edward Mwaikali akiwaombea watoto wakati wa ibada ya siku kuu ya Pasaka iliyofanyika kanisa la Usharika wa Ruanda jijini Mbeya. Picha na Saddam Sadick
Amesema wanapopatikana wagombea wenye hofu ya Mungu huweza kuongoza vizuri kuliko kuwaachia nafasi wasio na dini ambao uongozi wao huwa si bora.
Amesema atatamani kuona wana Usharika wa Ruanda wakijitokeza wengi kugombea.
"Chama cha Mapinduzi (CCM) ndio pekee wameweka ukomo upande wa urais, lakini vyama vingine vyote nafasi iko wazi, niombe waumini hapa kanisani mjitokeze tupate wabunge, madiwani na hata Rais," amesema.
"Itapendeza sana kuona kiongozi akiwa mtumishi wa Mungu kwa kuwa hofu itakuwapo kuliko kuwaachia wengine, kwa sasa nimeona mmoja kanisani hapa aliyeonyesha nia kugombea na ameshaniambia tumuombee," amesema.
Amewashukuru na kuwapongeza waumini kwa namna wanavyoongezeka kila siku, akisema kwa miaka mitatu sasa tangu ashike nafasi hiyo wamefikia zaidi ya 17,000.
"Hii ni Pasaka yetu ya tatu tangu tuanzishe kanisa hili lakini idadi inaongezeka, kwa sasa tunazidi waumini 17,000, tuendelee kushukuru Mungu kwa maendeleo haya na tupambane kumaliza ujenzi wa kanisa letu," amesema.