Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI WA MJEMA: Tanapa, Ngorongoro zilivyopita tanuru la moto kupitia OC

Kama ni uamuzi wenye masilahi mapana kwa nchi, basi ni huu uamuzi wa Serikali kuamua kurejesha utaratibu wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) na Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kukusanya na kutumia sehemu ya mapato yake.

Ukweli una sifa moja tu, kwamba hata ukiukataa hauwezi kugeuka kuwa uongo, kwa hiyo utaratibu wa sasa ulioanza ulioanza kutumika kwa Sheria ya Fedha ya mwaka 2020/2021, ulikuwa na athari kubwa katika shughuli za uhifadhi na utalii.

Ni kupitia sheria hii, taasisi hizo mbili ziliondolewa utaratibu wa kukusanya na kutumia mapato yake kwa shughuli za uhifadhi badala yake walikusanya na kupeleka zote mfuko mkuu wa Serikali.

Kisha wanatakiwa kuomba Hazina, fedha za matumizi ya uendeshaji wa shughuli za utalii kila mwezi kupitia utaratibu wa ‘other charges’ (OC), utaratibu ambao ulionekana kuzorotesha shughuli za uhifadhi na Utalii katika taasisi hizo.

Fedha hizo hazitumwi Tanapa na Ngorongoro kwa wakati na wakati mwingine zinaweza zisitumwe hata kwa miezi miwili na kuna wakati hata zikija, haziji katika kiwango kile kilichoombwa ila iliyokuwa ikitumwa kwa wakati ni OC ya mishahara.

Nini kinachotokea? Kunajitokeza dharura ya matengenezo ya barabara ndani ya hifadhi lakini fedha hakuna ni mpaka ziombwe hazina na hii inasababisha watalii wanaoliletea Taifa fedha za kigeni kushindwa kufika katika baadhi ya vivutio.

Sote ni mashahidi kwamba tumekuwa tukiona video fupi fupi (video clip) hasa wakati wa masika, za namna watalii, waongoza watalii (Guides) wakilalamikia ubovu wa barabara ndani ya hifadhi, jambo linaloleta sura mbaya kimataifa.

Kwa hiyo, tunaweza kuilaumu Tanapa au NCAA kwa kadhia hii kumbe ni taasisi zinazokufa na tai shingoni kwa kukosa fedha za uendeshaji kwa vile kila wanachokusanya kinaenda Hazina, na kutakiwa kuomba matumizi kupitia OC.

Mathalani, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2023/2024 inasema Tanapa ilipokea Sh1.06 bilioni kati ya Sh23.03 bilioni zilizoidhinishwa kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya hifadhi.

Hii kwa mujibu wa CAG, anasema kiasi cha Sh21.97 bilioni sawa na asilimia 95 haikupelekwa Tanapa kwa mwaka huo wa fedha licha ya Tanapa kuzifuatilia fedha hizo kwa mamlaka husika. Kumbuka walishakusanya na kupeleka mfuko mkuu wa Serikali.

CAG anasema ukosefu wa fedha za maendeleo ulisababisha kuchelewa kukamilika kwa miradi ya maendeleo 15 yenye thamani ya Sh14.12 bilioni inayotekelezwa na hifadhi za Taifa 10 na ucheleweshaji ulianzia mezi 10 hadi 33.

Katika NCAA, huko ndio ilikuwa mbaya zaidi, kwa sababu CAG anasema bajeti ya maendeleo iliyoidhinishwa kwa mwaka 2023/2024 ikiwamo ya miundombinu ilikuwa Sh28.61 bilioni, lakini Serikali haikupeleka hata senti tano ya bajeti hiyo.

CAG katika taarifa yake amependekeza Serikali izipe kipaumbele hifadhi za Taifa na maeneo ya hifadhi kwa kuzipa fedha za kutosha zinazohitajika kusaidia shughuli za ujenzi na utekelezaji wa miundombinu ndani ya hifadhi za Taifa.

Lakini kuna jambo ambalo halisemwi sana ambalo limeletwa na utaratibu huu wa OC, kwamba inakuwa vigumu kukabiliana na vitendo vya ujangili ndani ya hifadhi kwa sababu ili kuwakabili majangili, huwezi kutegemea kuomba fedha za OC.

Fedha zinatakiwa ziwepo wakati wote kwa ajili ya kuwezesha doria kufanyika na hata pale zinapopatikana taarifa za kiintelijensia za uwepo wa majangili sehemu fulani, basi operesheni za kuwakabili zifanyike kwa haraka bila kusubiri OC.

Kuna watoa huduma ambao hutoa huduma mbalimbali katika taasisi hizo, wanajikuta wakisubiri muda mrefu kulipwa wakisubiri OC, ambayo kama nilivyotangulia kusema inachelewa kutumwa na hata ikitumwa, haitoshelezi.

Kwa hiyo nilipomsikia Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kupitia hotuba yake ya bajeti kuu kwa mwaka wa fedha 2025/2026, akisema wanakwenda kufanya mabadiliko ya sheria iliyoibua kadhia hii nilifarijika sana.

Katika hotuba yake, Dk Mwigulu alipendekeza kufanyika kwa marekebisho katika kifungu cha 9 cha Sheria ya Hifadhi za Taifa, Sura 282 kama kilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Fedha ya 2024, ili kubadili utaratibu huo wa sasa.

Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, anapendekeza kufutwa kwa kifungu kidogo cha 2(b) cha mgao wa asilimia 91 kwenda mfuko mkuu wa Serikali na badala yake, kuweka mgao wa wasilimia 51 ili fedha hizo zibaki katika akaunti ya Tanapa iliyopo BoT.

Kwa muktadha huo huo, waziri akapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu cha 12 cha sheria ya NCAA sura ya 284 kama kilivyorekebishwa na Sheria ya Fedha ya 2024 ili nao waweze kubakia na asilimia 51 ya mapato kama Tanapa.

Uamuzi huu si tu umepongezwa na wabunge, la hasha, umepongezwa pia na wadau wa utalii wakiwamo Mawakala wa Utalii kupitia Tanzania Tour Operators Association (TATO), ambao wanasema unakwenda kuboresha uhifadhi na utalii.

Kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TATO, Elirehema Matulo, anasema kuhifadhi wanyamapori na  maliasili zingine ni gharama kubwa hivyo kilichofanywa na Wizara ya Fedha kwa Tanapa na NCAA ni busara kubwa na inahitaji kupongezwa.

Lakini mimi ni Tomaso, kwamba siamini hili mpaka niuone muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2025 kwa sababu mwaka jana tulipewa maneno matamu hivi hivi na Serikali ya kuzifanya Tanapa na NCAA kukusanya na kutumia sehemu.

Tuliahidiwa hili na wadau wakapongeza sana Serikali na kuwapa maua yao, lakini ilipokuja Sheria ya Fedha ya 2024, suala hili la kuzipa Taasisi hizo mamlaka ya kubaki na sehemu ya mapato (retention), halikuwepo kabisa kwenye sheria hiyo.

Huwa siamini mpaka nione kwa macho hasa nikirejea kilichotokea katika Bunge lililopita, hivyo ninasubiri niione ahadi hii ya Serikali kwenye Sheria ya Fedha ya 2025, kwa sababu kama ni kupita tanuru la moto, basi NCAA na Tanapa wamepita huko.

Lakini kwa kauli ya Waziri Mwigulu, inaonesha usikivu wa Serikali kwani athari za OC, limezungumzwa pia kwa kirefu na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakiishauri Serikali kurudisha utaratibu wa 'retention' ilipowasilisha maoni yake kuhusu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Mei 19 2025.

Kama alivyosema Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Priscus Tarimo, ng’ombe ambaye unamfaidi kwa maziwa hawezi kuchinjwa kwa ajili ya kuliwa sikukuu, bali anatunzwa vizuri hivyo Serikali ivitunze vyanzo hivi muhimu vya mapato.

Ninaamini nitaliona suala hili kwenye muswada wa fedha 2024 ili nisiwe Tomaso na ninaamini pia katika msimu ujao wa utoaji wa gawio kwa Serikali, taasisi hizi mbili zitajitokeza katika mashirika ya umma yaliyofanya vizuri zaidi. 0656600900