Serikali kuzinusuru Tanapa, Ngorongoro

Muktasari:
Juni 12, 2025, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2025/26 ikiwa na mapendekezo ya kuresha utaratibu wa awali kwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wa kukusanya fedha na kutumia kiasi.
Dar es Salaam. Uamuzi wa Serikali wa kurejesha utaratibu wa awali kwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) umepongezwa na wadau mbalimbali.
Awali, taasisi hizo zilikuwa zikikusanya mapato na kutumia sehemu ya mapato hayo kwa shughuli za utalii, lakini Serikali ilibadili utaratibu ambapo taasisi hizo zinakusanya mapato yote na kupeleka Mfuko mkuu.
Baadaye taasisi hizo zilitakiwa kuomba fedha kila mwezi kwa ajili ya mishahara na matumizi mengine au OC.
Hatua hiyo ilisababisha Tanapa na Ngorongoro kuyumba na wadau wakiwemo wabunge wamekuwa wakipaza sauti kuitaka Serikali kurejesha utaratibu wa awali ili kuziwezesha taasisi hizo kujimudu kifedha.
Hata siku ya Gawio Day, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu baada ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutoa gawio serikalini, alisema kuna mambo yanaangaliwa kwa Tanapa na Ngorongoro ambazo nazo zitaacha kutoa gawio.
Juni 12, 2025, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2025/26 alisema Serikali inakwenda kubadili utaratibu huo na ili kuruhusu hilo, Sheria ya Fedha ya mwaka 2024 itafanyiwa marekebisho ili ziweze kutumia sehemu ya mapato.
“Napendekeza kufanya marekebisho katika Kifungu cha 9 cha Sheria ya Hifadhi za Taifa, Sura 282 kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Fedha ya mwaka 2024 ili kufuta kifungu kidogo cha 2(b) cha mgao wa asilimia 91 kwenda Mfuko Mkuu wa Serikali.
“Na badala yake kuweka mgao wa asilimia 51 ya mapato yatokanayo na huduma zinazotolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania kuwekwa kwenye akaunti ya taasisi hiyo iliyopo Benki Kuu ya Tanzania na matumizi yake yatafanyika kwa kuomba kibali kutoka kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali, na asilimia 40 ya mapato hayo yataingizwa Mfuko Mkuu wa Serikali.”
Uamuzi huo wa Serikali ni kuitikia kilio cha Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na wabunge ambao walisema uamuzi wa taasisi hizo kukusanya fedha na kuzipeleka zote mfuko mkuu wa Serikali, kisha kuomba fedha za matumizi umeathiri shughuli za uhifadhi.
Mmoja wa watumishi wa Tanapa aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema:”Hali ilikuwa mbaya sana, uamuzi huo unakwenda kuyanusuru kwani yalikuwa yanajiendesha kigumu kigumu. Kwa hiyo Serikali imesikia na hali hiyo inakwenda kuchochea sasa uhifadhi.”
Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga amesema sekta ya utalii unahitaji maboresho ya mara kwa mara na zinahitaji kuwa na fedha na mabadiliko yalivyofanyika yameonekana kuwaathiri kwani wakiomba fedha zinachelewa.
“Ili kuongeza ufanisi kama ulivyokuwa mwanzo, kwani utaimarisha miundombinu ya hifadhi. Sekta ya utalii inahitaji kuboreshwa mara kwa mara.” “Ni vyema waweze kukusanya na kutumia wao wenyewe. Tunatarajia mwaka ujao wa fedha hili linakwenda kufanyika na Waziri wa Fedha atalileta kwenye sheria ya fedha kwani taasisi hizi mbili zinakusanya na kutumia na Serikali isimamie matumizi.”
Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi yeye amesema: “Hilo ni jambo jema kuona Serikali inasikiliza maoni na ushauri wa wabunge. Tanapa na Ngorongoro zinatoa huduma na ni vizuri wakarejeshewa utaratibu wa mwanzo.
“Ili wakusanye vizuri lazima waweke maeneo yao vizuri ya miundombinu, kama miundombinu haitaboreshwa haiwezi kuvutia na wakiwa na fedha zinazopatikana kwa wakati itachochea zaidi maboresho,” amesema Shangazi.
Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Priscus Tarimo amesema Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2023/24 kuna maeneo ameonesha fedha zilizotakiwa kurudi: “Hazikurudi.”
Tarimo amesema kupanga ni jambo moja na kutekeleza ni jambo jingine: “Nilisema ng’ombe ambaye unamfaidi kwa maziwa hawezi kuchinjwa kwa kuliwa sikukuu, badala yake anatunzwa vizuri.”
“Mimi naona Serikali ijitahidi kile kiasi ambacho kinapaswa kurudi kinarudi ili maendeleo ya hifadhi zetu ziendelee kwani biashara ya utalii ni ya kipindi maalumu na hifadhi zina ushindani lazima tuziboreshe,” amesema Tarimo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama wa Waongoza Watalii Tanzania (Tato), Elirehema Maturo amesema uamuzi huo utasaidia kuboresha miundombinu ya hifadhi na shughuli mbalimbali kwani zinahitaji fedha.
“Serikali inapaswa kuangalia kwa jicho ka kipekee hizi taasisi kupewa fedha ili kuziwezesha kujiendesha. Wito wetu kama Tato, fedha hizo zinatumika kama zilivyotarajia,” amesema Maturo.
Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Pareso amesema kipindi cha nyuma utaratibu ulibadilika ambapo fedha zote zilikuwa zinapelekwa mfuko mkuu wa Serikali na shughuli za uhifadhi zilipitia kipindi kigumu.
“Kuanza kuomba fedha ni mchakato mrefu, sisi wajumbe wa kamati tulishauri ili Serikali iweze kuachia fedha kiasi ili zikasaidie maendeleo ya uhifadhi,” amesema.