Jarida la Tanapa lang’ara mkutano mkuu CCM

Muktasari:
- Tanapa inasimamia jumla ya hifadhi za Taifa 21 ambazo zimechukua eneo la kilomita za mraba 99,306.5.
Dar es Salaam. Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) limeonyesha kwa vitendo namna lilivyotekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/25 kwa weledi na ufanisi mkubwa.
Jarida hilo ambalo lilisambazwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu, wageni na waalikwa, limeonyesha namna Tanapa ilivyotekeleza ilani hiyo na kupata mafanikio na kipekee kupitia vivutio vya utalii nchini.

Kwa nyakati tofauti, wajumbe wa mkutano mkuu walionekana wakiperuzi jarida hilo katika makundi na wengine wakiwa mmoja mmoja huku wakionyesha kufurahia kusoma taarifa zilizopo kwenye jarida hilo.
Moja ya mambo ambayo jarida hilo limeyataja kama mafanikio katika utekelezaji wa ilani ni pamoja na kuongezeka kwa mapato ya Serikali yatokanayo na utalii wa vivutio vya Tanapa na kumaliza migogoro baina ya wananchi wanaoishi karibu na hifadhi za Taifa.

Mafanikio mengine ni shirika hilo kuvunja rekodi ya makusanyo tangu kuanzishwa kwake, hatua ambayo imeelezwa kuwa imetokana na jitihada mahsusi chini ya Kamishna wa Uhifadhi, Juma Nassoro Kuji.
Hatua ya kuandaa jarida hilo inatokana na ukweli kuwa CCM ndiyo inaisimamia Serikali, hivyo ni haki ya wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho kufahamu utekelezaji wa ilani yake unaofanywa na Serikali kupitia taasisi zake.