Prime
CCM yazindua Ilani mpya, kugusa maeneo haya nyeti

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa Ilani Mpya ya Uchaguzi ya chama hicho.
Muktasari:
- Yaahidi kuuisha mchakati wa Katiba mpya ambao umekuwa ukipigiwa kelele kwa muda mrefu sasa tangu ulipokwama 2014
Dodoma. Makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamesema Ilani ya Uchaguzi ya 2025-2030 iliyozinduliwa leo imegusa maisha na changamoto za Watanzania na kwamba, kwa uwezo na umahiri wa wagombea wake inatekelezeka.
CCM imezindua Ilani hiyo leo Mei 30 kwenye mkutano mkuu wake maalumu jijini Dodoma, huku ikitaja mkakati wa kuongeza ajira, ukuzaji wa haki na demokrasia na kuhusisha mchakato wa Katiba mpya ambao, umekuwa ukipigiwa kelele kwa muda mrefu sasa tangu ulipokwama 2014.
Waziri wa Mipango na Uchumi, Profesa Kitila Mkumbo ndiye aliyewasilisha Ilani hiyo ya kurasa 78 kwa wajumbe wa mkutano mkuu, ikiwa imebeba vipaumbele tisa na maelekezo mbalimbali kwa Serikali, kisha ikapitishwa kwa kauli moja.
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hasan amesema yote yaliyomo ndani ya Ilani hiyo yanatekelezeka.
“Ndugu zangu, yaliyomo kwenye Ilani hii tunaweza kuyatekeleza, kuendana na mipango na uwezo tulionao. Tunajiamini tutaweza kama tumeweza kipindi hiki, tutaweza kipindi kijacho. Kubwa kwa Watanzania ni kuweka utulivu ndani ya nchi yetu,” amesema Rais Samia.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Ndele Mwaselela amesema Ilani hiyo imeangalia changamoto za Watanania na ndio sababu anagusa maisha ya watu moja kwa moja.
Amesema kabla ya kuandikwa kwa ilani hiyo makundi mbalimbali yalifikiwa kwa namna tofauti hivyo, kuakisi matakwa, maoni na mahitaji ya Watanzania.
Miongoni mwa ahadi zilizomo kwenye ilani hiyo ni kuzalishwa kwa ajira milioni 8 kwa vijana katika kipindi cha miaka mitano ijayo zikiwemo rasmi na zisizo rasmi.
Pia, CCM imeahidi kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia sekta za kilimo na ufugaji, ikigusia kuanzishwa kwa vyama vya kuwawezesha vijana.

Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi akisoma moja ya kitabu cha Ilani mpya ya Uchaguzo ya chama hicho ilipokuwa ikiwasilishwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa CCM jijini Dodoma leo ijumaa Mei 30, 2025. Picha na Edwin Mjwahuzi
Kwa sasa tatizo la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana limekuwa bomu kutokana na wengi wanaohitimu vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya kati kusota mitaani bila ajira.
Mara kwa mara changamoto hiyo imekuwa ikizungumzwa kwenye majukwaa ya kisiasa, ya kitaaluma na bungeni, ambapo wabunge wamekuwa wakiikalia kooni Serikali kuhakikisha inaweka mikakati madhubuti ya kuzalisha ajira ili kulinda kizazi kijacho.
Kupitia ilani hiyo, CCM inaielekeza Serikali kuweka mazingira wezeshi ya kisera na kimkakati kwa kuhamasisha uanzishwaji na kuimarisha makampuni ya vijana na vyama vya ushirika (SACCOS) vyenye kujiendesha kibiashara katika halmashauri zote nchini ili yaweze kupata mikopo, mitaji na nyenzo kwa lengo la kuwezesha wananchi wengi zaidi wakiwemo wanaohitimu elimu ya juu na vyuo vya ufundi kujiajiri na kutoa ajira.
Pia, inaelekeza kuwajengea vijana uwezo wa kuajirika nje ya nchi, Serikali ya CCM itaanzisha vituo vya mafunzo stadi kwa ajili ya kuwaandaa vijana katika kushindana kupata fursa za ajira nje ya nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema nchi inataka kutengeneza ajira kama ambavyo ilani ya uchaguzi hiyo imesema, lakini ili kufikia hayo ni lazima kuongeza thamani mazao yanayozalishwa.
“Miaka minane iliyopita nikiwa Simiyu, tulianzisha kitu kinaitwa district product factory (uzalishaji wa bidhaa katika wilaya) yaani kila tunachokizalisha tukiongezee thamani, hii ni sawa ya hii ya kujenga viwanda kwenye kila maeneo ya uzalishaji,” amesema Mtaka.
Amesema Ilani ya uchaguzi kuja na wazo hilo la kujenga viwanda vya kuongeza thamani kwenye wilaya, inakwenda kujibu kila kitu.
“Katika mahala ambapo nchi yetu haitauza kitu ghafi kwenye uzalishaji tutatengeneza ajira, tukiongeza thamani, ajira zinaongezeka toka shambani kwenye viwanda vidogo kwenda sokoni.
Mbali na ajira, ahadi nyingine iliyopo kwenye ilani hiyo ni ukuzaji wa demokrasia nchini ambapo, Ilani inaelekeza kuwekwa kwa mfumo wa kisheria katika kutekeleza falsafa ya uongozi ya 4R ambazo zilianzishwa na Rais Samia.
Rais Samia alianzisha falsafa ya 4R inayoangazia Mageuzi, Maridhiano, Ustahimilivu na Kujenga upya, ambazo zilimpambanua tofauti na mtangulizi wake, Hayati John Magufuli.
Kwenye eneo la kudumisha demokrasia, Ilani ya CCM inaelekeza kuanza kuhuishwa mchakato wa Katiba mpya ambao ulikwama.
Hii inaweza kuwa habari njema hasa wakati huu ambao kumeibuka mvutano kwa baadhi ya vyama vya siasa vikipigania kuzia kushiriki uchaguzi vikidai mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi kwanza.
Kukwama kwa mchakato wa Katiba mpya kimekuwa kilio cha muda mrefu miongoni mwa Watanzania hivyo, kuwekwa kwenye Ilani ya CCM kunamaanisha kinachofuata ni utekelezaji.
Hata hivyo, ukiacha ilani ya mwaka 2020-2025; nyingine za miaka ya karibuni zilikuwa zinagusia suala hilo na bado halijahitimishwa.
Ufisadi, usafi kumulikwa
Katika wasilisho lake, Profesa Mkumbo ametaja uimarishaji wa mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi kwa kuzuia na kudhibiti vitendo vya rushwa ikiwemo kuchukua hatua kali za kisheria na kinidhamu dhidi ya viongozi na watumishi wa umma wanaojihusisha navyo.
Tuhuma za rushwa na ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka ni miongoni mwa mambo yanayopigiwa kelele kila kukicha. Wananchi wamekuwa wakilalamika kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwenye maeneo ya utoaji huduma za msingi kwa jamii, hivyo kuwafanya wasio na uwezo kukosa haki zao za msingi.

Wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa CCM wakisoma vitabu vinavyoeleza Ilani mpya ya uchaguzi ya chama hicho kwa mwaka 2025-2030 wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo alipokuwa akiiwasilisha kwa wajumbe, jijini Dodoma leo Ijumaa Mei 30, 2025. Picha na Edwin Mjwahuzi
Mjumbe wa mkutano huo, Neema Lugangira amesema asasi za kiraia zimenufaika sana na Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025-2030 ina mambo mengi ambayo yanakwenda kutoa majawabu katika kukuza na kuharakisha ustawi na maendeleo ya nchi.
“Nikiwa kama mdau wa masuala ya usawa wa kijinsia katika siasa, nimefarijika sana na sehemu hii ambayo inaongelea masuala ya usawa kijinsia, lakini inaongelea masuala ya kudumisha demokrasia,”amesema.
Alisema CCM inaendelea kujidhihirisha namna ambavyo kitaimarisha mazingira ya ushiriki katika siasa na demokrasia ili wanawake, vijana na watu wenye ulemavu waweze kushiriki katika siasa.
Alisema pamoja na utekelezaji wa sheria ambazo zilipitishwa hivi karibuni bungeni, Sheria za Vyama vya Siasa na Sheria za Uchaguzi, CCM inakwenda kuwa na Sera ya Jinsia ya CCM pamoja na dawati la jinsia.
Katika miaka mitano, Serikali ya CCM inalenga kuanzisha na kutekeleza Gridi ya Taifa ya Maji itakayotumia vyanzo vikubwa vya maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, uchumi na mazingira.
Vyanzo hivyo ni Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa, pamoja na mito mikubwa ya Rufiji, Ruvuma na Pangani.
Kama utekelezaji wa maelekezo hayo ya Ilani utafanyika kwa mafanikio, basi huenda tatizo la upatikanaji wa majisafi na salama nchini likapatiwa ufumbuzi.
Katika maeneo mbalimbali nchini, suala la upatikanaji wa uhakika wa majisafi ni changamoto ambayo kila kukicha imekuwa ikipigiwa kelele. Kwa sasa huduma hiyo haijakidhi mahitaji ya wananchi hususan wa maeneo ya mijini huku kwa vijiji hali ikiwa nafuu kwa baadhi ya maeneo.
Wasanii hawakuachwa nyuma
Katika Ilani yake, CCM imeahidi kujenga maktaba ya kisasa ya kitaifa ya muziki na filamu (National
Music and Film Dijital Library) na kuimarisha mafunzo ya kitaalamu kwa wasanii na walimu wa sanaa ili kuongeza ujuzi na kuwafikia vijana wengi katika kupata mafunzo ya sanaa.
"Kukuza masoko ya bidhaa za sanaa ndani na nje ya nchi kwa kuhamasisha ushiriki wa wasanii katika maonyesho na matamasha ya kitaifa, kikanda na kimataifa," inasema sehemu ya Ilani.
Wakati mkakati mwingine utakuwa ni kuunganisha vyuo vya sanaa na wasanii walio kwenye jamii ili kuendeleza vipaji na kuhamasisha kukuaji wa sanaa nchini.
Changamoto ya makazi
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, CCM kupitia ilani yake kimeahidi kuwa ifikapo mwaka 2030 Serikali itakuwa imejenga au kuwezesha ujenzi wa nyumba bora na za bei nafuu zisizopungua 50,000 ili kupunguza uhaba wa nyumba za kuishi.
Taarifa ya Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2022 inaonyesha kuwa Tanzania ina uhaba wa nyumba 3,800,000 na uhaba huo unaongezeka kwa nyumba 300,000 kila mwaka.
Wakati uhaba huo ukiongezeka, idadi ya watu nayo itaongezeka kutoka watu milioni 61 hadi kufikia watu milioni 78 ifikapo mwaka 2030.
Neema sekta ya kilimo
"Kwa kutambua nafasi ya kilimo katika usalama wa nchi, ujenzi wa uchumi na kukuza kipato cha wananchi, CCM itaendelea kusimamia mapinduzi katika sekta ya kilimo ili kukifanya kuwa cha kisasa na chenye tija," amesema Profesa Mkumbo.

Wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa CCM wakisoma vitabu vinavyoeleza Ilani mpya ya uchaguzi ya chama hicho kwa mwaka 2025-2030 wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo alipokuwa akiiwasilisha kwa wajumbe, jijini Dodoma leo Ijumaa Mei 30, 2025. Picha na Edwin Mjwahuzi
Amesema lengo ni kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa chakula, kuongeza kipato cha wakulima, kukuza pato la Taifa, kuwa kichocheo cha kukua kwa viwanda, na kuongeza ajira.
Amesema CCM inaweka shabaha ya kuona kuwa sekta ya kilimo inakua kutoka asilimia 4.6 mwaka 2025 hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 ambapo wataimarisha upatikanaji wa mbegu bora na kwa bei nafuu na kuendelea kutoa ruzuku ya pembejeo mbalimbali kwa wakulima, ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija.
Ni eneo hilo pia wamepanga kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 983,466.06 mwaka 2024 hadi hekta milioni tano mwaka 2030 ili kupunguza utegemezi wa mvua lakini watanunua na kusambaza matrekta 10,000 kwa wakulima.
Mifugo mambo safi
Wakati kilimo kikiangaliwa kwa jicho la tatu, hali iko vivyo hivyo kwa sekta ya mifugo ambako Ilani imeweka lengo la kupima na kutenga hekta milioni tatu hadi kufikia mwaka 2030 kwa ajili ya kupunguza ama kumaliza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Katika Ilani inayoishia mwaka huu, Serikali ilipanga kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuwawezesha wafugaji kufanya ufugaji wa kisasa kwa kuwa na mifugo michache yenye tija. Pia, ilianzisha mradi wa ufugaji maarufu kama BBT ya mifugo ambao umehusisha vijana waliopewa mafunzo ya kufuga kisasa kwa kuongeza thamani.
Vijana hao, mbali na mafunzo, waliwezeshwa kununua mifugo na kuinenepesha kisha kutafutiwa masoko ya uhakika. Ilani hiyo ya CCM pia inakwenda kutekelezwa visiwani Zanzibar, ikitaja mkakati wa kuboresha uchumi na maisha ya wananchi na kuwaongezea kipato.
Mpango mwingine utakuwa ujenzi wa daraja la kihistoria litakalopita baharini kuunganisha Kijiji cha Charawe na Chwaka katika Mkoa wa Kusini, ambalo lilishatajwa mara kadhaa.
Wananchi wa Zanzibar pia watanufaika na ujenzi wa nyumba 4,715 za makazi ambazo zitagawiwa kwa wananchi katika eneo la Chumbuni.
Mpango mwingine ni utoaji wa mikopo ya Sh10 bilioni kwa wananchi pamoja na mafunzo ya usimamizi wa fedha ili kuwainua kiuchumi.
Wasiwasi katika utekezaji
Baadhi ya wataalamu wa uchumi waliozungumza na Mwananchi wamesema ni Ilani nzuri itakayoleta mapinduzi katika sekta ya uchumi, ingawa wameonyesha wasiwasi kuhusu utekelezaji wake.
Mhadhiri wa Ndaki ya Uchumi na Stadi za Biashara ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Dk Felix Nandonde amesema ni Ilani itakayoleta mageuzi ya kiuchumi hasa katika uboreshaji wa miundombinu, kilimo, na mapinduzi ya kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani.
Ameongeza kuwa kipengele cha maendeleo jumuishi ni muhimu kwa sababu kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikikumbwa na changamoto ya maendeleo ambayo hayawagusi wananchi wote kwa usawa, hivyo Ilani hii inaweza kushughulikia hilo.
Pia amesema kuwa suala la ajira kwa vijana ni muhimu na likisimamiwa kama ilivyoelezwa katika Ilani, litazalisha ajira nyingi na kwenda sambamba na maendeleo jumuishi, huku akisisitiza kuwa utekelezaji na ushirikiano kati ya Serikali na chama tawala ndio nguzo kuu.
Naye mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude amesema CCM haijawahi kuwa na Ilani mbaya kwa sababu wataalamu wanaoiandaa hutumia akili na ujuzi wao, lakini tatizo limekuwa katika utekelezaji. Amesema kuwa mara nyingi viongozi wanapotangaza mafanikio jukwaani husema wamefikia asilimia fulani ya utekelezaji, lakini hawasemi ukweli kuhusu changamoto na maeneo ambayo hawakufanikisha.
Mkude amesema tatizo ni utekelezaji na si Ilani, akitoa mfano kuwa tangu enzi za Hayati Benjamini Mkapa, kulikuwa na ahadi nyingi lakini utekelezaji wake ulikuwa na changamoto.