Kilichoipa ushindi Tanzania tuzo ya Almasi Jumuiya ya Ulaya

Muktasari:
- Tanzania imeng'ara kwa mara ya sita katika tuzo za kimataifa za uhifadhi zinazotolewa na Umoja wa Ulaya.
Dar es Salaam. Huduma bora za kimataifa za utalii, ushirikishwaji wa wananchi, wadau wa huduma pamoja na usimamizi wa shughuli za kiutalii ni miongoni mwa sababu zilizoipa ushindi Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) katika tuzo ya ubora wa kimataifa mwaka 2025.
Tuzo hiyo imetolewa na Jumuiya ya Ulaya inayojishughulisha na utafiti wa viwango vya ubora ya Ulaya (ESQR) Stockholm, Sweden usiku wa Mei 29, 2025.
Akizungumza mara baada ya kuwasili jana Jumatatu, Juni 2, 2025 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Kamishna wa Uhifadhi Tanapa, Mussa Kuji amesema ushindi huo ni mara ya sita mfululizo na kwa mwaka huu wameshinda daraja la Almasi.

"Kulikiwa na mashirika zaidi ya 40 duniani, shirika letu la Tanapa ndilo lililoibuka mshindi, ni kitu cha kujivunia kama taifa kwani ushiriki wa Watanzania kwanzia wananchi, askari na watoa huduma ndiyo wamefanikisha hili," amesema kamishna huyo.
Pia, tuzo hiyo ameielekeza kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akionyesha juhudi ikiwemo kucheza filamu maarufu za 'The Royal Tour na 'Amazing Tanzania', kuvutia watalii.
"Kwa kiwango tulichofikia tusibweteke bali tuongeze nguvu, ushirikiano zaidi ili tuendelee kufanya vizuri na wageni wetu wazidi kuja kwa wingi wakae muda mrefu waongeze mapato," amesisitiza.
Kamishina Kuji amesema anaitoa tuzo hiyo ni maalumu kwa Rais Samia kwa juhudi zake binafsi za kuitangaza Tanzania na kuwa nchi inayoshika nafasi ya pili duniani kwa kuwa na vivutio bora zaidi.
"Rais Samia anastahili tuzo hii kutokana na sababu mbili, moja ya filamu mbili alizoshiriki maarufu ambazo zimetoa ufahamu zaidi kuhusu uzuri wa nchi duniani na pili kwa mwongozo wake, maagizo na mchango wake katika utoaji wa huduma za hali ya juu kwa sekta ya utalii na uhifadhi nchini," amesema Kuji.

Tuzo hiyo pia imechangiwa na majibu mazuri ya huduma walizopata wageni wanaokuja nchini.
Awali, Naibu Kamishna wa Uhifadhi ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kaskazini, Steria Ndaga amesema jamii inayozunguka hifadhi za taifa ndiyo wahifadhi namba moja wanaochangia kupata tuzo hizo.
Amesema wataendelea kushirikiana na jamii hizo, kama anavyosisitiza Kamishna wa Tanapa ya kwamba kila askari, kila hifadhi iwe na uhusiano mwema na jamii inayoizunguka.
"Mtalii akija Tanzania anashuka uwanja wa ndege anakuja kwenye hifadhi ambapo anapokelewa na waongozaji, anakutana na jamii kwa hiyo kila mmoja anashiriki katika kutoa huduma bora za uhifadhi na utalii," amesema.
Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Godwell Olle Meing’ataki amesema Tanzania imejiunga na mfumo wa utoaji huduma bora ISO 9001 wa mwaka 2005 ambao unatathimini vigezo vya utoaji huduma bora.
Amesema mfumo huo unawezesha kutoa huduma za kitalii kwa hali ya kimataifa ambapo ni miongoni mwa sababu za Tanapa kuendelea kutoa huduma hizo.
"Tuzo hii ni chachu kwa Watanzania kwa ujumla kuendelea kufanya vizuri katika huduma ili kuendelea kukidhi vigezo vya kimataifa," amesema.
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi amesema Tanzania inapaswa kujivunia mafanikio hayo.
"Ni furaha kwa Tanzania kupitia Tanapa kutambuliwa kama moja ya washindi wa Tuzo ya Ubora wa ESQR mwaka 2025 kwa mwaka wa sita mfululizo.
"Mafanikio haya yanathibitisha Tanzania kama eneo kuu la utalii kwa jamii za kimataifa na dunia kwa ujumla,” amesema Balozi Matinyi.