Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Taifa limuenzi Mzee Cleopa Msuya kwa alama alizoacha

Aliyewahi kuwa Makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu, Cleopa Msuya.

Kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Mzee Cleopa David Msuya, kimeacha pengo kubwa katika historia ya uongozi na maendeleo ya Tanzania.

Taifa limepoteza siyo tu aliyekuwa kiongozi mzoefu, bali kioo cha maadili, utulivu na utumishi uliotukuka kwa zaidi ya miongo mitatu.

Katika kipindi hicho, Msuya alitoa mchango mkubwa katika maeneo mbalimbali ya utawala, uchumi, na mageuzi ya kisiasa, akiacha alama zisizofutika.

Msuya alikuwa mtumishi wa umma tangu mwaka 1964, akianza kama Katibu Mkuu, baadaye kushika nafasi nyeti kama Waziri wa Fedha na Waziri Mkuu mara mbili. Ujasiri wake wa kukabiliana na changamoto za kiuchumi katika kipindi kigumu cha mpito wa sera kutoka uchumi wa kijamaa kwenda soko huria ni ushahidi tosha wa uongozi wa maono na kufanya uamuzi mgumu uliojenga misingi ya taifa.

Alisimama kidete wakati mashirika ya kimataifa yalipokuwa yakiibana nchi na kuifanya Tanzania ifikie makubaliano ya kujikwamua kiuchumi, mchango ambao bado unahisiwa hadi leo.

Mchango wake mkubwa zaidi ni katika kurejesha Serikali za Mitaa, jambo ambalo linagusa maisha ya kila Mtanzania. Kupitia usimamizi wake kama Waziri Mkuu, Serikali ilipitisha muswada wa kufufua taasisi hizo za msingi, hatua iliyoimarisha ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya maeneo yao.

Hili ni jambo linalopaswa kuwa sehemu ya kumbukumbu ya kudumu kwa jina lake, kwani aliweka msingi wa ugatuaji wa madaraka na uwajibikaji wa karibu kati ya viongozi na wananchi.

Msuya pia alijulikana kwa utulivu, busara na nidhamu ya hali ya juu. Katika mahojiano na viongozi waliowahi kushirikiana naye kama Balozi Gertrude Mongella na Jaji Joseph Warioba, wote walikiri kuwa alikuwa mnyenyekevu, mwenye maono na msikilizaji mzuri.

Msuya ameondoka, lakini alama alizoziacha ni za milele. Katika kipindi hiki cha maombolezo ya siku saba, Watanzania tuna wajibu wa kutafakari namna ya kuyaenzi maisha ya kiongozi huyu kwa kuiga mfano wake wa uongozi wa kimaadili, uzalendo, na kujitoa kwa dhati katika maendeleo ya taifa.

Tusikubali alama zake kufutika. Ni wakati wa kuzihifadhi, kuzikuza, na kuziendeleza kwa vizazi vijavyo. Mzee Cleopa Msuya hakuwahi kujisifu, bali alitenda.

Hakika, kumuenzi Mzee  Msuya hakupaswi kubaki katika hotuba na kumbukumbu za msiba pekee. Ni wakati muafaka kwa Serikali na taasisi za elimu, historia na utawala kushirikiana kuweka kumbukumbu rasmi ya maisha na kazi zake.

Vilevile, maeneo aliyotokea kama Mwanga na Mkoa wa Kilimanjaro kwa jumla yana nafasi muhimu ya kuwa sehemu hai ya urithi wa Msuya. Inaweza kuanzishwa makumbusho au kituo cha maarifa kuhusu historia yake, ambacho kitahifadhi nyaraka, picha, na ushuhuda wa waliowahi kufanya naye kazi.

Hatua kama hizi zitasaidia vijana wanaochipukia kwenye uongozi na vizazi vijavyo kumjua kwa undani zaidi na kujifunza kutoka kwa misingi aliyosimamia, hususan utumishi wa umma uliojaa uadilifu, busara, na kujali maslahi ya wengi.