Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwanga yaomboleza: Cleopa Msuya ameacha alama isiyofutika

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisaini kitabu cha maombolezo, nyumbani kwa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, marehemu Cleopa Msuya jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Mashuhuda watoa taswira ya uongozi wa kipekee uliosheheni uadilifu, maono na upendo kwa nchi na watu wake, jambo linalothibitisha kwa nini hayati Cleopa Msuya atabaki kuwa kielelezo cha kizazi na urithi usiosahaulika.

Mwanga/Dar. Wakati maandalizi ya mazishi ya aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, hayati Cleopa David Msuya yakiendelea, wananchi wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro wameeleza namna kifo chake kilivyoacha pengo lisilozibika, wakimtaja kama kiongozi aliyeweka historia ya umoja, mshikamano na maendeleo pasipo na ubaguzi.

Mazishi ya kiongozi huyo mkongwe yanatarajiwa kufanyika Mei 13, 2025, katika kijiji alikozaliwa cha Chomvu, kata ya Chomvu wilayani Mwanga, ambako maandalizi yanaendelea chini ya usimamizi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro, ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Nurdin Babu.

Katika mahojiano na Mwananchi, baadhi ya wakazi wa Mwanga wamesema Msuya alikuwa zaidi ya kiongozi, alikuwa ni mlezi wa fikra na dira ya maendeleo kwa wana Mwanga.

“Alikuwa kioo cha uadilifu, mshauri wetu na mtu aliyekuwa tayari kutoa msaada wa mawazo kila tulipomuhitaji. Hakika tumepoteza hazina kubwa,” amesema mmoja wa wakazi hao kwa uchungu.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa aliyekuwa Makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya Kijiji cha Chomvu, kilichopo Wilaya ya Mwanga Mkoani humo. Picha na Omben Daniel

Hayati Msuya, aliyezaliwa mwaka 1931, alifariki dunia Mei 7, 2025, akiwa katika Hospitali ya Nzena jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo.

Miongoni mwa waliomzungumzia ni Abdi Msangi, jirani na aliyewahi kufanya kazi na hayati Msuya miaka ya 1990.

Amesema Msuya alikuwa mtu mkarimu, mchapakazi na mshauri aliyehimiza maadili, umoja na maendeleo kwa wananchi wote bila ubaguzi.

"Tulimwita 'Baba wa Mwanga' kwa sababu ya mchango wake mkubwa. Alitufundisha kuwa waadilifu na kuwaheshimu wote bila kujali cheo au hali ya mtu," amesema Msangi.

Wananchi wengine wa Chomvu wameeleza huzuni yao kwa kumpoteza mtu waliomtazama kama hazina ya ushauri na dira ya maendeleo.

Abdalah Kiluvia ameeleza kuwa hayati Msuya alihamasisha sekta za elimu, afya na miundombinu.

“Ametujengea shule, kutuletea umeme na kuhakikisha barabara zinafunguliwa. Ni kweli tumepoteza nguzo kuu ya maendeleo ya Mwanga,” amesema kwa masikitiko.

Reshi Ndoile, mkazi mwingine, amekumbuka jitihada za Msuya katika kuanzisha Benki ya Wananchi wa Mwanga, taasisi iliyobeba ndoto za wakazi wa eneo hilo kiuchumi.

“Aliunganisha watu wote bila kujali tofauti zao. Huyu ni mtu wa pekee na tutamuenzi milele,” amesema Ndoile.

Diwani wa Chomvu, Shagira Mchomvu, amesema Msuya alikuwa daraja la kuunganisha mawazo ya maendeleo kwa jamii nzima ya Mwanga.

“Tulitegemea sana hekima zake. Ameacha alama kubwa ambayo tutaiendeleza,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amethibitisha kuwa maandalizi ya mazishi yako katika hatua nzuri na kwamba shughuli rasmi ya maziko itafanyika Jumanne, Mei 13.

Amesema jina la 'Baba wa Mwanga' alilopewa na wananchi linaakisi upendo na mchango wake kwa mkoa.

“Alikuwa kiongozi aliyejali watu wake hata baada ya kustaafu, aliendelea kufuatilia maendeleo ya mkoa wetu,” amesema Babu.


Jijini Dar es Salaam

Pia, jijini Dar es Salaam, viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Jaji Joseph Warioba, pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Balozi Ombeni Sefue, ni miongoni mwa waomboleaji waliofika nyumbani kwa marehemu maeneo ya Upanga kutoa salamu za rambirambi na kuungana na familia katika kipindi hiki cha maombolezo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisaini kitabu cha maombolezo, nyumbani kwa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, marehemu Cleopa Msuya jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Akizungumza na waombolezaji nyumbani kwa marehemu, Majaliwa amesema msiba wa Msuya ni pigo kubwa na zito kwa Taifa, kutokana na mchango wake mkubwa katika uongozi wa nchi akiwa katika nafasi za juu serikalini.

Amesisitiza kuwa Serikali itashiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa maandalizi ya mazishi hadi siku ya mwisho atakapopumzishwa katika nyumba yake ya milele.

Majaliwa amesema maandalizi hayo yanafanyika kwa kufuata taratibu za kiserikali kwa kushirikiana na familia ya marehemu, tayari imewasilisha ushauri wake kuhusu baadhi ya hatua muhimu za msiba huo.

"Kwa sasa taratibu za kiserikali zinaendelea. Ushauri wa familia ni kusubiri baadhi ya wanafamilia walioko nje ya nchi ili nao wafike na kushiriki shughuli hizi muhimu za kumuaga mpendwa wetu," amesema Majaliwa.

Ameongeza kuwa kuanzia kesho (Mei 9), Ofisi ya Waziri Mkuu itaanza kutoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu hatua mbalimbali za maandalizi ya mazishi ya Mzee Msuya.

Majaliwa amesema makatibu wakuu kupitia Kamati ya Uendeshaji wa Mazishi ya Viongozi wa Kitaifa wanaendelea na maandalizi hayo kwa karibu kwa kushirikiana na familia.

“Ninawaomba waombolezaji wote waendelee kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu. Hata wale walioko Wilaya ya Mwanga ambako taratibu za awali zinaendelea, nimewasihi waendelee kwa utulivu na heshima kwa kiongozi wetu,” amesema Majaliwa.

Miongoni mwa waombolezaji waliowasili nyumbani kwa Msuya ni Profesa Anna Tibaijuka, ambaye alimkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika kuwawezesha wakulima nchini.

Akizungumza kwa hisia, Profesa Tibaijuka amesema moja ya mambo makubwa aliyoyafanya Msuya wakati akiwa Waziri Mkuu ni kuruhusu wakulima kuuza mazao yao katika maeneo mbalimbali bila vikwazo vya kisera.

“Alifungua njia, akaondoa mazuio yaliyowazuia wakulima kusafirisha mazao yao kutoka wilaya moja kwenda nyingine au hata kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine.

“Hili lilikuwa jambo kubwa kwa wakulima wetu. Msuya alikuwa kiongozi mwelewa, mwenye maono ya mbele. Hivyo, ni muhimu simulizi hizi zisahauliwe; tuzisimulie kama hazina ya taifa na alama aliyotuachia,” amesema Profesa Tibaijuka.

Kwa upande wake, Balozi Mstaafu Daniel ole Njoolay ameeleza kuwa Msuya alikuwa kiongozi thabiti, asiyelegea katika misimamo yake, na asiyependa unafiki.

Amemtaja kama mtu mchapakazi, aliyefanya kazi kubwa katika nafasi mbalimbali, hususan alipokuwa Waziri wa Viwanda na baadaye Waziri Mkuu.

“Katika sekta ya viwanda, hayati Msuya ndiye aliyeanzisha Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO), ambalo limeendelea kuwa msaada mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo nchini. Alikuwa kiongozi wa mfano, mwenye maono makubwa na aliyetanguliza maslahi ya Taifa kila mara,” amesema Njoolay.

Balozi mwingine mstaafu, Ali Mchumo, alimkumbuka Msuya kwa mchango wake katika kusimamia sera za viwanda, akisema ndiye aliyesimamia mpango wa kitaifa wa kuanzisha viwanda kwenye kila mkoa.

Amesema enzi hizo zilishuhudia uanzishaji wa viwanda vya saruji, nondo, nguo na vingine vya kimkakati vilivyochangia kuimarisha uchumi wa taifa.

“Mzee Msuya alikuwa kiongozi jasiri, aliyejikita katika maendeleo ya kiuchumi. Alikuwa na ndoto ya kuona kila mkoa una viwanda vyake na aliweka misingi hiyo. Hakika mchango wake katika maendeleo ya viwanda hauwezi kufutika,” amesema Mchumo.

Akiendelea kumuelezea marehemu, Mchumo amesema alikuwa mwalimu na mlezi, aliyependa kuwaelekeza watu kwa upole lakini kwa msimamo.

“Nilipoteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Waziri wa Biashara, alikuwa ndiye aliyenipokea na kunielekeza kazi. Alikuwa si tu kiongozi bali pia rafiki wa kweli kwa waliomzunguka,” ameongeza.


Mjukuu amzungumzia

Nje ya maisha ya uongozi wa kitaifa, ndani ya familia Msuya anakumbukwa kama mlezi na mshauri wa karibu. Mjukuu wake wa kwanza, Ngazo Msuya, amesema babu yake alikuwa mfano wa maadili, kazi na upendo.

“Nimejifunza kutoka kwake kuwa mwadilifu na mpenda kazi. Alikuwa mtu wa busara, aliyejitahidi kupata muda wa kutukusanya, kutushauri na kutupa maono ya maisha. Nafasi yake ni kubwa kwetu kama familia, na mafanikio yangu mengi nayatambua kuwa yamechangiwa na mafundisho yake,” amesema Ngazo kwa hisia Ngazo.mwisho