Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huu hapa wasifu wa marehemu Cleopa Msuya

Muktasari:

  • Kifo cha Msuya aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu, kimetangazwa leo, Jumatano, Mei 7, 2025, na Rais Samia Suluhu Hassan.

Tanzania imepoteza mmoja wa nguzo muhimu za historia yake, Cleopa Msuya, aliyewahi kushika nafasi ya Waziri Mkuu wa Tanzania mara mbili.

Alizaliwa Januari 4, 1931, katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, wilayani Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro. Tangu akiwa mdogo, Msuya alionyesha kiu ya elimu na dhamira ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Alianza masomo katika Shule ya Msingi Kivindu na baadaye kujiunga na Old Moshi, moja ya shule bora za sekondari kwa wakati huo. Kwa ufaulu na juhudi, alipata nafasi ya kuendelea na masomo ya juu katika Shule ya Tabora Boys, na baadaye kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda ambako alihitimu shahada ya sanaa (BA) katika historia, jiografia na sayansi ya siasa kati ya mwaka 1952 hadi 1955.

Baada ya kuhitimu, Msuya alirudi nyumbani na kuanza kazi ya Ofisa Maendeleo ya Jamii mwaka 1956, kazi aliyoifanya kwa moyo katika maeneo ya vijijini. Hapa ndipo alipojifunza mahitaji ya watu na changamoto za maendeleo.

Kufikia mwaka 1964, umahiri wake ulimletea uteuzi wa kuwa Katibu Mkuu katika wizara mbalimbali.

Alianza na Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Utamaduni (1964–1965), akahamia Wizara ya Ardhi, Makazi na Maji (1965–1967), kisha Wizara ya Mipango na Uchumi (1967–1970), na hatimaye Wizara ya Fedha (1970–1972).

Mwaka 1972, Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, alimteua kuwa Waziri wa Fedha. Katika kipindi hicho kigumu kiuchumi, Msuya aliongoza juhudi za kupanga matumizi ya Serikali na kuweka msingi wa nidhamu ya kifedha.

Baada ya mafanikio katika nafasi hiyo, alihamishiwa Wizara ya Viwanda (1975–1980), ambako alisaidia kusukuma mbele ajenda ya viwanda vya kitaifa, ikiwa ni pamoja na viwanda vya nguo, usindikaji wa mazao ya kilimo na uzalishaji wa zana za kilimo.

Novemba 7, 1980, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa mara ya kwanza. Ilikuwa ni kipindi kigumu ambapo Taifa lilikuwa linakumbwa na mtikisiko wa kiuchumi uliotokana na Vita ya Kagera na changamoto za utekelezaji wa siasa ya ujamaa.

Desemba 7, 1994, alirejeshwa tena katika nafasi ya Waziri Mkuu, wakati huu pia akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais chini ya Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi. Kipindi hicho kilishuhudia mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kisiasa, ikiwa ni pamoja na mageuzi ya soko huria na ujio wa mfumo wa vyama vingi. Msuya alihusika moja kwa moja katika usimamizi wa mageuzi hayo, akihakikisha kuwa Serikali inabaki kuwa nguzo ya uongozi na ustawi wa jamii.

Mbali na nafasi za juu serikalini, mchango wake katika kuimarisha uchumi wa taifa ulikuwa wa kipekee. Alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kushiriki katika mipango ya kuokoa uchumi wa Tanzania wakati wa hali mbaya ya kifedha miaka ya 1980 na 1990.

Pia alikuwa sehemu muhimu ya jukwaa la kupanga na kutekeleza sera za viwanda, sera ambazo hadi sasa zimebaki kuwa msingi wa ujenzi wa uchumi wa kati.

Msuya alikuwa si tu kiongozi wa Taifa, bali pia mwana maendeleo wa nyumbani. Aliongoza Jukwaa la Maendeleo ya Kilimanjaro kwa muda mrefu, akihamasisha miradi ya elimu, maji na huduma za jamii katika mkoa wake wa kuzaliwa.

Katika maisha ya kifamilia, Msuya alijulikana kama mtu mwenye upendo, utulivu na maadili ya juu. Alifunga ndoa na Rhoda Mshana, na pamoja walijenga familia iliyojengwa juu ya misingi ya heshima na mshikamano. Licha ya vyeo vyake, aliendelea kuwa mtu wa kawaida baada ya kustaafu.

Hadi miaka ya mwisho ya maisha yake, Msuya aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika masuala ya kitaifa.

Mwaka 2019, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), nafasi aliyoitumia kushiriki katika mjadala wa kitaaluma kuhusu matumizi bora ya ardhi na maendeleo ya miji.

Pia alishiriki mijadala ya kitaifa kuhusu hali ya uchumi, utawala bora na mustakabali wa Taifa. Hata hivyo, aliendelea kutumika hadi mauti ilipomkuta.