Prime
Cleopa Msuya alama ya binadamu aliyeishi mbele ya wakati

Muktasari:
- Msuya alianzisha Benki ya Wananchi Mwanga wakati akikaribia kustaafu ubunge. Ni kipindi ambacho Mungai na Msuya wote walikuwa wabunge. Hiyo ndiyo sababu ilikuwa rahisi kuchangia maono, halafu benki za Mucoba na Mwanga zikaanzishwa.
Mtumishi wa umma aliyegeuka mwanasiasa. Mhusika muhimu katika ukuaji wa sekta binafsi. Kiongozi mwenye maono aliyeifanya tasnia ya fedha Tanzania ifike ngazi ya kijamii. Ndivyo unaweza kuuelezea kwa kifupi kabisa, uhusika wa Cleopa David Msuya.
Mwaka 2000, Msuya alikuwa mhusika kiongozi na mbeba maono, aliyefanikisha kuanzishwa kwa Benki ya Kijamii Mwanga. Ikajulikana zaidi kama Benki ya Wananchi Mwanga. Ilibeba usajili namba mbili Tanzania. Nyuma ya Benki ya Kijamii Mufindi (Mucoba).
Nilipata kuzungumza na mwasisi wa Benki ya Mucoba, marehemu Joseph Mungai, ambaye alipata kuwa waziri katika mabaraza ya mawaziri ya marais, Mwalimu Julius Nyerere, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete. Mungai alisema, Mwanga ilipaswa kusajiliwa ya kwanza.

Aliyewahi kuwa Makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu, Cleopa Msuya.
Mungai aligundua kuwa Msuya alikuwa akishawishi wananchi wa Wilaya ya Mwanga kuhamasika kuanzisha benki yao. Baadaye, Mungai aliweza kufanikisha mipango ya haraka Mufindi, Mucoba ikawa ya kwanza kusajiliwa na Benki Kuu, kabla ya Benki ya Wananchi Mwanga.
Hadi hapo, inatosheleza kuonesha ni kiasi gani Msuya alivyokuwa mbeba maono ya mbali kuhusu huduma za kifedha ngazi ya jamii. Uwepo wa Benki ya Mwanga wakati wowote, ukuaji wake, wingi wa wanahisa wenye misuli mikubwa na umiliki wa rasilimali, daima Msuya ni alama.
Msuya alianzisha Benki ya Wananchi Mwanga wakati akikaribia kustaafu ubunge. Ni kipindi ambacho Mungai na Msuya wote walikuwa wabunge. Hiyo ndiyo sababu ilikuwa rahisi kuchangia maono, halafu benki za Mucoba na Mwanga zikaanzishwa.
Msuya, mwanahisa na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kwa muda mrefu, kuliko yeyote kabla yake, na hajapatikana mwingine baada yake. Msuya alianza kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TBL, Agosti 17, 2005, alistaafu Novemba 24, 2021.
Kimahesabu, Msuya aliiongoza TBL, akiwa Mwenyekiti wa Bodi, kwa miaka 16, miezi mitatu na siku saba. Kipindi chake, TBL ilishuhudiwa ikikua kwa kasi na kampuni hiyo kupata ukwasi mkubwa mwaka hadi mwaka, hivyo kutoa gawio (dividend), lililonona kwa wanahisa.
Ukuaji wa TBL nyakati za uongozi wa Msuya, ukwasi mkubwa kisha kuifanya TBL kuwa kumpuni iliyokuwa ikitajwa msimu mmoja wa kifedha hadi mwingine kwa ulipaji mkubwa wa kodi serikalini, siyo tu inampambanua Msuya kama alama muhimu ya ukuaji wa sekta binafsi, bali kiungo bora wa ushirikiano baina ya sekta binafsi na umma (PPP).
Kisiasa, ukiwauliza wananchi wa Mwanga, Kilimanjaro, watakujibu kuwa Msuya, nyakati za utumishi wa jimbo lao akiwa mbunge, aliwawakilisha vizuri, vilevile kuwaunganisha kupata maendeleo ya kimsingi, hasa miundombinu ya kijamii.
Msuya alipotoka
Januari 4, 1931, Kijiji cha Chomvu, Usangi, Wilaya ya Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro, alizaliwa mtoto aliyeitwa Cleopa. Halafu kwa ukamilifu, jina rasmi likawa Cleopa David Msuya. Matokeo ya baadaye yakampambanua kama mtoto bora kabisa wa Mwanga.
Msuya, alisoma Shule ya Msingi ya Kilutheri, Mwanga, Kilimanjaro na kuhitimu. Alipata ufaulu bora uliomwezesha kuchaguliwa kusoma Shule ya Sekondari ya Old Moshi, Kilimanjaro. Alifaulu vizuri kabisa, akajiunga na Shule ya Juu ya Wavulana Tabora (Tabora Boys High School). Alifaulu pia.
Mwaka 1952, Msuya akiwa na umri wa miaka 21, alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, aliposoma Jiografia, Sayansi ya Siasa na Historia. Alihitimu Makerere mwaka 1955, akipata shahada yake ya kwanza ya sanaa.

Baada ya kuhitimu shahada yake Makerere, Uganda, safari ya Msuya kwenye utumishi wa umma ilianza. Alirejea nyumbani kwao Mwanga, na mwaka 1956, aliajiriwa kama ofisa wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Vijijini. Mwaka 1960, Msuya alihamishiwa Dar es Salaam, na ulipofika mwaka 1962, alipandishwa cheo kuwa Kamishna wa Maendeleo ya Jamii Vijijini.
Mwaka 1964, Msuya aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Utamaduni. Nafasi hiyo aliitumikia kwa mwaka mmoja (1964 – 1965), akahamishwa kwenda kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Maji (1965 – 1967), Wizara ya Mambo ya Uchumi na Mipango (1967 – 1970), halafu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha (1970 – 1972).
Kuanzia Februari 18, 1972, Msuya alipanda ngazi kutoka mtumishi wa umma namba moja Wizara ya Fedha (Katibu Mkuu) mpaka kuwa Kiongozi wa Wizara (Waziri). Alitumikia uwaziri wa fedha kwa miaka mitatu, miezi nane na siku 15 (Februari 18, 1972 – Novemba 3, 1975).
Msuya, kuanzia Novemba 3, 1975, alikuwa Waziri wa Viwanda. Aliitumikia wizara hiyo kwa muhula mzima wa serikali ulioanza Novemba 1975 hadi Oktoba 1980. Kuanzia Novemba 1980, Msuya aliteuliwa na Mwalimu Nyerere, kisha kuthibitishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Utumishi wa Msuya akiwa Waziri Mkuu wa Tanzania, ulidumu kwa miaka miwili na miezi mitatu (Novemba 1980 mpaka Februari 1983). Baada ya kuachia ofisi ya Waziri Mkuu, Msuya alirejeshwa na Mwalimu Nyerere kuwa Waziri wa Fedha kwa kipindi kingine. Nafasi hiyo ya Waziri wa Fedha, Msuya aliitumikia hadi Mwalimu Nyerere alipomaliza muhula wake wa mwisho wa urais na kung’atuka, Novemba 1985.
Novemba 6, 1985, Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, alimteua Msuya kuwa Waziri wa Fedha, lakini wizara ikiwa imepanuliwa kuwa Wizara ya Fedha, Mambo ya Uchumi na Mipango. Nafasi hiyo aliitumikia kwa miaka mitatu na miezi minne (Novemba 1985 – Machi 1989).
Kuanzia Machi 1989, Wizara ya Fedha ilipunguzwa. Uchumi na Mipango viliondolewa, hivyo kubaki Wizara ya Fedha peke yake. Msuya aliendelea kuwa Waziri wa Fedha mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu 1990.
Baada ya uchaguzi na Mwinyi kushinda muhula wa pili, alimteua Msuya kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Ulipofika mwaka 1994, Mwinyi alimpandisha cheo kuwa Waziri Mkuu, kwa kipindi cha pili. Uteuzi huo ulimfanya Msuya kuweka rekodi ya kuwa waziri mkuu wa kwanza Tanzania, kutumikia nchi chini ya marais wawili tofauti.
Mwingine aliyeweka rekodi hiyo baada ya Msuya ni Kassim Majaliwa, ambaye ametumikia uwaziri mkuu chini ya Rais wa Tano Tanzania, Dk John Magufuli na Rais wa Sita, Dk Samia Suluhu Hassan. Msuya, alipoteuliwa kuwa waziri mkuu na Mwinyi, alishika pia nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Tanzania.
Hiyo ilitokana na matakwa ya kikatiba wakati huo. Rais Mwinyi alikuwa Mzanzibari, kwa hiyo ilikuwa lazima Makamu wa Rais atoke Tanzania Bara. Hivyo, Msuya akawa Makamu wa Kwanza wa Rais, halafu aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk Salmin Amour, alikuwa Makamu wa Pili wa Rais, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nguli amefumba macho
Mei 7, 2025, mchana, Msuya alifumba macho kwa mara ya mwisho, na hatafumbua tena. Rais Samia aliutangazia umma kuwa Msuya alifikwa na mauti akiwa Hospitali ya Mzena, Mikocheni, Dar es Salaam. Kutoka Januari 4, 1931 mpaka Mei 7, 2025, ni miaka 94, miezi minne na siku tatu. Huo ndiyo umri wa Msuya duniani.

Mwanga wanamwita “Baba wa Mwanga”, alikuwa kichocheo cha kuanzishwa wilaya hiyo Septemba Mosi, 1979, kisha akawa mbunge wa kwanza wa jimbo hilo, aliyehudumia kwa zaidi ya miongo miwili, mpaka alipostaafu kwa hiyari Oktoba 2000.
Kwa jumla, Msuya alikuwa mbunge kwa miaka 28 na miezi nane. Yaani kuanzia Februari 1972 alipoteuliwa kuwa mbunge ili kuwa Waziri wa Fedha, hadi Oktoba 2000, alipoona imetosha ubunge na kuamua kukaa pembeni.
Uchaguzi Mkuu 1995, Msuya alikuwa jina kubwa lililochanja mbuga kuelekea uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya CCM. Msuya aliingia hadi tatu bora, alipochuana na Mkapa pamoja na Kikwete. Mwisho, Mkapa alishinda, Kikwete alitoka wa pili.
Unapomzungumzia Msuya, unamtaja kiongozi mwanaharakati wa maendeleo. Alishakuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo Kilimanjaro, ongeza uasisi wa Benki ya Wananchi Mwanga, halafu maendeo ya huduma za kijamii Mwanga, kama umeme, maji na barabara.
Machi 9, 2025, Rais Samia alizindua rasmi mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe, ambao Msuya, katika kipindi cha utumishi wake serikalini, bungeni na hata nje ya Bunge, aliupigania kwa muda mrefu. Angalau, Msuya amepumzika akiwa ameshaona matunda ya mradi alioupigania.
Miaka ya 1990, jina la Msuya lilikuwa simulizi ya kila kijiwe cha kahawa. Alitajwa kama mwanasiasa aliyekuwa na utajiri mkubwa. Hadithi moja ikatungwa, kwamba Mwalimu Nyerere alipata kutembelea nchi moja Ulaya, akaingia hotelini, akakuta hadi masahani na vijiko vinavyotumika kuhudumia wateja vilikuwa na jina Msuya.
Ilikuwa simulizi ya vijiweni, ni kama tu hekaya za Abunuwasi na tungo za Alfu Lela Ulela. Hata hivyo, jambo lenye uhakika usio na shaka ni kwamba Msuya ni mwanamageuzi ya kiuchumi Tanzania. Alikuwa Waziri wa Fedha, Mambo ya Uchumi na Mipango, kipindi Tanzania ilipohama kutoka Uchumi wa Ujamaa mpaka Uchumi wa Soko Huria.
Sifa nyingi ambazo humwendea Rais Mwinyi kwa mageuzi aliyoyafanya kwenye sera za uchumi, kwa sehemu kubwa zinamhusu Msuya, ambaye kama Waziri wa Fedha, aliongoza mabadiliko kwa vitendo. Msuya ana sifa zote za kuwa mmoja wa wahusika wa historia ya Tanzania.
Nyota wa filamu Uingereza, Alan Cox, amepata kusema: “Live fast, die old, and make very sure everyone knows you were there” – “Ishi haraka, kufa ukiwa mzee, na hakikisha kila mtu anatambua ulikuwepo.” Maisha ya Msuya yameakisi matakwa ya nukuu hiyo.
Msuya aliishi haraka na kufanya mambo mengi, ndiyo maana marais Mwalimu Nyerere na Mwinyi, walimwamini katika uwaziri wa fedha, viwanda na uwaziri mkuu. Nafasi zote ambazo Nyerere alimteua Msuya kwa nyakati tofauti, na kwa Mwinyi ilikuwa vivyo hivyo.
Matokeo makubwa ambayo Msuya ameyatengeneza Mwanga, na taifa la Tanzania kwa jumla, ni kipimo kuwa Msuya aliishi haraka. Miaka 94 aliyoishi duniani, ni uthibitisho kwamba amekufa akiwa mzee. Wastani wa Mtanzania kuishi duniani kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni ni miaka 66, kwa hiyo Msuya aliuvuka wastani huo kwa miaka 28 zaidi.
Nyakati zote Msuya atakumbukwa kwamba alikuwepo Mwanga na aliitumikia Tanzania. Mambo aliyoyaanzisha na kuyasimamia ni kumbukumbu kwa vizazi vingi vijavyo. Hakika, kila mtu atatambua kwamba Msuya alikuwepo na aliishi.
Kwa heri Baba wa Mwanga, kwa heri Mzee Msuya.