Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ahueni kwa magari, bajaji za gesi

Muktasari:

  • Serikali imezindua kituo mama kitakachotoa huduma kwa vyombo vya moto 1,200 kwa siku.

Dar es Salaam. Changamoto ya madereva kukaa foleni muda mrefu kusubiri nishati ya gesi jijini Dar es Salaam huenda ikafikia tamati baada ya Serikali kuzindua kituo mama kitakachotoa huduma kwa vyombo vya moto 1,200 kwa siku.

Kituo mali ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kilichozinduliwa mkabala na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kinaongeza idadi ya vituo vya kujaza gesi kufikia vinane jijini humo.

Kwa mujibu wa TPDC, mpango uliopo ni kupeleka huduma Dodoma na Morogoro, ikielezwa pia ununuzi wa vituo vitano vinavyohamishika upo hatua ya mwisho.

Baada ya uzinduzi wa kituo hicho leo Mei 9, 2025, dereva wa bajaji, Faustine Michael amelieleza Mwananchi bado kuna uhitaji wa vituo vingi zaidi vyenye ukubwa sawa na kilichozinduliwa.

“Ni hatua nzuri kwetu tunaotegemea nishati hii. Kituo hiki ni kikubwa, kinahudumia vyombo vingi vya usafiri. Hasara tuliyokuwa tunapata kwa kukaa kwenye foleni zaidi ya saa nne na wakati mwingine siku nzima, itakuwa historia kwetu,” amesema.

Amesema uchache wa vituo vya kujaza gesi kwenye magari na bajaji, unawaathiri zaidi madereva wanaofanya biashara mtandao, kwani muda wanaokaa kusubiri nishati hiyo walipaswa kufanya kazi.

Isaac Mkonye, mkazi wa Mbezi ambaye ni dereva wa teksi mtandao amesema kituo hicho ni kikubwa, lakini uhitaji wa vingi zaidi ni mkubwa, akieleza kuwa wengi wanaelekea kutumia gesi ambayo kilo moja ni Sh1,550 tofauti na mafuta ambayo ni Sh2,900 kwa lita moja.

Akizungumzia kilio cha foleni, Mwenyekiti wa Bodi TPDC, Balozi Ombeni Sefue amesema ilikuwa ikiwakosesha usingizi, akisisitiza hatua zinazochukuliwa sasa ni kutatua changamoto hiyo.

Naibu Waziri Nishati, Judith Kapinga (katikati) akiwa na uongozi wa UDART, viongozi wa TPDC na wa Wizara ya Nishati wakishuhudia ujazwaji wa gesi katika basi jipya la mwendokasi katika Kituo mama cha gesi (CNG) kilichozinduliwa leo Ijumaa Mei 9, 2025 eneo la Mliman City, Dar es Salaam. Picha na Sunday George


Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akizindua kituo hicho ameitaka TPDC kuhakikisha vituo vingine vya gesi vinavyojengwa Lindi na Dodoma vikamilike kwa kasi.

Amewatoa hofu wenye nia ya kubadilisha mifumo ya vyombo vya moto kwenda kwenye gesi, akisema teknolojia ya ubadilishaji ni salama na bei nafuu.

Kapinga amesema Serikali inatumia fedha nyingi kuwekeza kwenye miradi ya kuwasaidia wananchi lakini changamoto ni uendeshaji.

“Nitoe rai TPDC ninyi ndio wasimamizi wa wadau wengine wa gesi kwenye magari, naomba muonyeshe mfano wa huduma bora zenye uhakika, ili muwe mfano kwa wengine pale mnapowasimamia,” amesema.

Ameitaka TPDC kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa wadau katika sekta ya gesi asilia ili kuvutia wadau wengi zaidi na kutatua changamoto zilizopo kwa wakati.

Kaimu Mkurugenzi wa TPDC, Francis Mwakapalila amesema wanakusudia kuongeza vituo vya kujaza gesi kwenye vyombo vya moto Dar es Salaam na mikoa mingine.

“Tupo hatua ya mwisho ya ununuzi wa vituo tano hamishika vya kujaza gesi katika mikoa ya Dodoma na Morogoro na tuna kampuni zaidi ya 60 ambazo zimeonyesha nia ya kujenga vituo maeneo mbalimbali nchini,” amesema.

Mwakapalila amesema hadi mwishoni mwa 2026 vituo vingine vipya saba vitakuwa vimejengwa na sekta binafsi.

Meneja Mradi wa TPDC, Emmanuel Gilbert amesema Sh18.9 bilioni zimetumika kujenga kituo hicho na vingine vidogo eneo la Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Kibaha, mkoani Pwani.

Amesema kituo hicho kina uwezo wa kuhudumia vyombo vya moto 1,200 kwa siku na vituo vinane kwa wakati mmoja.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio amesema kituo hicho ni cha kwanza kwa ukubwa Afrika Mashariki na cha pili kwa Afrika.

Amesema kituo cha kwanza kipo Nigeria kikiwa na uwezo wa kuhifadhi gesi futi za ujazo milioni 5.1 na cha Tanzania kina uwezo wa kuhifadhi gesi yenye ujazo wa futi milioni 4.2.

Mbali na kituo hicho, vipo vingine vinane vinavyotoa huduma vilivyopo Uwanja wa Ndege, Tazara, Ubungo Maziwa, Barabara ya Sam Nujoma na viwili TOT Tabata.

Taarifa ya TPDC iliyotolewa mwaka jana ilionyesha vyombo vya moto vinavyotumia gesi nchini ni zaidi ya 4,800.

Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) katika taarifa inaonyesha matumizi ya gesi asilia huokoa zaidi ya asilimia 50 ya gharama anazotumia mtu kwenye dizeli na petroli.

Mtungi wa kilo 15 wa CNG hujazwa kwa Sh23,000 na hutembea wastani wa kilomita 250 kwa gari aina ya Toyota IST, ambayo ingegharimu wastani wa Sh80,000 kwa petroli.