Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Basi la mwendokasi linalotumia gesi kuanza, wananchi kupanda bure

Muktasari:

  • Watakaopata fursa ya kupanda basi hilo ni abiria wenye kadi za kieletroniki za mabasi yaendayo haraka ambao wanafanya safari kati ya Morocco na Kivukoni na huduma hiyo itakatolewa kwa wiki moja.

Dar es Salaam. Mpango wa matumizi ya gesi asilia kwenye mabasi ya Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) umeanza baada ya Serikali kuzindua kwa mara ya kwanza basi linatumia gesi asilia.

Majaribio ya basi hilo likiwa na abiria, sasa yatafanyika kwa wiki nzima kuanzia Jumatatu Mei 12, 2025 na safari zitakuwa bure kati ya Morocco na Kivukoni.

Basi hilo la majaribio ni miongoni mwa mabasi 99 yaliyotarajiwa kuwasili nchini ambapo usafiri huo sasa unaelezwa utatatua kero ya usafiri kwa Dar es Salaam.

Basi jipya la mwendokasi wakati likijazwa gesi katika kituo mama cha gesi (CNG) eneo la Mliman City, Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Basi hilo limezinduliwa na Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga leo Mei 9, 2025 wakati akizindua pia kituo cha gesi asilia kinachomilikiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Kapinga amesema gesi kwenye magari ni mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita ambayo inahimiza matumizi ya nishati safi.

“Tunafungua ukurasa mpya katika sekta ya usafiri katika Mkoa wa Dar es Salaam, UDART inazindua basi litakalotumia gesi asilia na gesi kwenye magari ndio mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita,” amesema.


Kuhusu basi hilo

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), Waziri Kindamba amesema basi hilo la kwanza la mfano linalotumia gesi iliyoshindiliwa (CNG), ni sehemu ya mkakati wa kuondoa kero za usafiri Dar es Salaam.

“Magari yataingia mwezi wa saba (Julai) au wa nane (Agosti) mwishoni na yataanza safari za Kimara, Kivukoni, Morocco, Gerezani, mradi awamu ya kwanza na wale wa sekta binafsi wakileta yataenda awamu nyingine.

“Awamu ya kwanza tu inahitaji mabasi 265 mpaka 300, lakini hivi sasa yanayotoa huduma yapo 80 hadi 100, hivyo ni machache,” amesema.

Kindamba amesema kampuni hiyo kwa muda mrefu imeelemewa na mabasi chakavu na yapo machache.

“Tulipokea maelekezo ya bodi kuleta magari ya kisasa yanayotumia teknolojia ya gesi asilia ambapo kutokana na hali ya fedha, tukasema tuanze na hilo moja.

“Tunataka kuliingiza barabarani watu walipande, walikosoe, yale 99 yatakapokuja katika kipindi cha miezi miwili na nusu hadi mitatu, tutajua wapi pa kurekebisha,” amesema.

Kindamba amesema basi hilo ni mwanzo mzuri, kwa kuwa kampuni hiyo imepitia changamoto nyingi.

Kuhusu mifumo ya basi hilo la majaribio, amesema abiria watakuwa na uwezo wa kuchaji simu zao, kuwa na mtandao wa intaneti, kamera na kiyoyozi na malipo ya nauli yatakuwa ya kidigitali.

“Niwaahidi watu wa Dar es Salaam, mwaka 2025 ndiyo wa mwisho wa kupata tabu katika usafiri, zile tabu za kuibiwa simu na kuchafuliwa kwenye mwendokasi zinakwenda kwisha,” amesema.

Naibu Waziri Nishati, Judith Kapinga (katikati) akiwa na uongozi wa UDART, viongozi wa TPDC na wa Wizara ya Nishati wakishuhudia ujazwaji wa gesi katika basi jipya la mwendokasi katika Kituo mama cha gesi (CNG) kilichozinduliwa leo Ijumaa Mei 9, 2025 eneo la Mliman City, Dar es Salaam. Picha na Sunday George


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya UDART, Meja Jenerali mstaafu Michael Isamuyo amesema UDART ilianzishwa Desemba 19, 2014 ikiwa kampuni tanzu ya UDA.

Amesema baada ya Serikali kuona UDA haina uwezo wa kuendesha magari ya mwendokasi, iliamua kuchukua hatua hizo kwa kuanzisha UDART.