Rais Samia kuongoza waombolezaji kuaga mwili wa Msuya

Rais Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Waziri Mkuu mstaafu Mzee Cleopa David Msuya enzi za uhai wake mara baada ya kufungua mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe kwenye hafla iliyofanyika Mwanga mkoani Kilimanjaro Machi 9, 2025.
Muktasari:
- Tukio hilo litaambatana na ibada maalumu, inatarajiwa kufanyika Mei 11, 2025 katika viwanja wa Karimjee kuanzia saa 3 asubuhi na kuongozwa na viongozi wa dini, pia, kutakuwa na salamu za viongozi mbalimbali pamoja na kuaga mwili.
Dar es Salaam. Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ataowangoza Watanzania katika tukio la kumuaga marehemu Waziri Mkuu na Makamu wa Rais mstaafu, Cleopa Msuya.
Hafla hiyo itakayoambatana na ibada maalumu, inatarajiwa kufanyika Mei 11, 2025 katika viwanja wa Karimjee kuanzia saa 3 asubuhi na kuongozwa na viongozi wa dini, pia, kutakuwa na salamu za viongozi mbalimbali pamoja na kuaga mwili.
Msuya alifariki dunia Jumatano Mei 7, 2025 saa 3 asubuhi katika Hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu ya moyo. Amekuwa akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Mzena na huko London nchini Uingereza.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 9, 2025, Msigwa amesema kamati ya kitaifa ya mazishi ya viongozi inayoongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwa kushirikiana na familia ya marehemu, imeendelea kuratibu hatua mbalimbali za msiba na kujumuisha kuhifadhi mwili wa marehemu.
“Uratibu umejumuisha uagaji, salamu za rambirambi, usafirishaji wa msiba na mazishi yatakayofanyika katika Kijiji cha Usangi,” amesema Msigwa ambaye pia ni na Katibu Mkuu wa Wizara Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Amesema kwa sasa maombolezo yataendelea Jumamosi Mei 10, 2025, mwili wa marehemu utafikishwa nyumbani kwake Upanga, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya taratibu za kifamilia.
“Tunatarajia ibada, salamu pamoja na kumuaga marehemu ifanyike kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 7 mchana na Jumatatu Mei 12, 2025, mwili wa hayati Msuya utasafirisha kwa ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanga,” amesema Msigwa.
Msigwa amesema mwili huo unatarajiwa kupokelewa Jumatatu katika uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) kati saa 2:30 hadi 3:30 asubuhi na mwili huo utasafirishwa kwa magari na kupelekwa katika uwanja wa Cleopa Msuya uliopo Mwanga ambapo viongozi na wananchi watapata nafasi ya kuuaga kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 10 jioni.
Ametoa wito kwa wananchi wa Mwanga wanaotaka kumuaga marehemu Msuya watumie nafasi hiyo iliyotengwa kwa ajili yao na baada ya hapo mwili utapelekwa kijijini kwao Usangi ambapo kutakuwa na ibada fupi ya maombolezo.
Amesema siku hiyo itakuwa ni mazishi ya hayati Msuya ambapo ratiba itaanza kwa ibada maalumu itakayofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) lililopo Usangi na kisha kufuatiwa na mazishi ya Kiserikali yatakayoongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ).