Nyongeza ya mshahara isiwe kigezo bei ya bidhaa kupaa

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya uamuzi wa kihistoria kwa kuongeza kima cha chini cha mishahara hadi kufikia shilingi 350,000. Hii ni hatua ya kupongezwa, kwani inalenga kuboresha maisha ya wafanyakazi na kuhakikisha kuwa wanapata kipato kinacholingana na hali halisi ya gharama za maisha.
Hata hivyo, hatua hii inahitaji uangalizi wa karibu na ushirikiano kati ya wadau wote ili isiwe chanzo cha athari hasi kwa uchumi wa nchi, hususan katika bei ya bidhaa muhimu sokoni.
Kwa upande wa Serikali, ongezeko hili linaonyesha dhamira yake ya dhati ya kusimamia masilahi ya wafanyakazi na kupunguza pengo la kipato. Kwa muda mrefu, wafanyakazi katika sekta mbalimbali wamekuwa wakikabiliwa na mishahara midogo isiyokidhi mahitaji ya msingi kama chakula, malazi, elimu na huduma za afya. Kwa kuongeza kiwango hiki, Serikali inalenga kuinua maisha ya wafanyakazi, kuongeza tija kazini na kuhimiza nidhamu ya kazi.
Hata hivyo, changamoto kubwa inayoweza kujitokeza ni kwa baadhi ya wafanyabiashara kutumia mwanya huu kuongeza bei za bidhaa bila sababu ya msingi. Tabia kama hii inaweza kufifisha lengo kuu la hatua ya Serikali, kwa kuwa ongezeko la mishahara linaweza kuonekana kama siyo kitu iwapo kupanda kwa gharama za bidhaa hakutadhibitiwa kama ilivyowahi kutokea miaka ya nyuma.
Ni muhimu kwa Serikali kupitia mamlaka husika kama Mamlaka ya Udhibiti wa Bei na Ushindani (FCC) kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bei sokoni na kuchukua hatua dhidi ya wafanyabiashara watakaobainika kupandisha bei kiholela. Aidha, watumiaji wanapaswa kuelimishwa kuhusu haki zao ili waweze kutoa taarifa pale wanapoona ongezeko lisilo la kawaida la bei.
Wafanyabiashara pia wana jukumu la kuchangia ustawi wa jamii. Kwa kuzingatia kuwa ongezeko la mishahara linaweza kuongeza uwezo wa wafanyakazi kununua bidhaa, ni busara kwao kuwa na mikakati ya muda mrefu inayolenga kuongeza uzalishaji na ubora wa huduma badala ya kutumia ongezeko hili kama kisingizio cha kupandisha bei. Kuongeza bei kiholela kunaweza kupunguza wateja na kuathiri biashara zao kwa muda mrefu.
Kwa upande mwingine, wafanyakazi hawapaswi kutumia hatua hii kama fursa ya kuacha kuwajibika au kudai haki bila kutimiza majukumu yao ya msingi. Haki huambatana na wajibu. Wafanyakazi wanapaswa kuongeza bidii kazini, kuwa waaminifu, na kuzingatia maadili ya kazi ili kuwahamisha waajiri wao waone ongezeko walilotoa lina tija kwa Taifa.
Tija kazini si tu kwa faida ya mwajiri, bali pia kwa ustawi wa taifa zima. Ongezeko la mshahara linapaswa kuendana na ongezeko la ufanisi kazini ili kuhakikisha kuwa sekta zote za uzalishaji zinaendelea kukua na kuongeza pato la taifa.
Zaidi ya hayo, vyama vya wafanyakazi vina wajibu mkubwa wa kuelimisha wanachama wao kuhusu namna bora ya kutumia mishahara yao kwa busara. Kupata ongezeko la mshahara si kigezo cha kuishi kwa matumizi ya anasa, bali ni fursa ya kupanga maisha kwa ufanisi, kuweka akiba, na kuwekeza katika shughuli za maendeleo.
Kwa ujumla, ongezeko la kima cha chini cha mishahara hadi Sh350,000 ni hatua chanya inayopaswa kuungwa mkono na Watanzania wote. Hili ni jibu kwa kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi, lakini pia ni mtihani wa maadili kwa wafanyabiashara na wafanyakazi wenyewe. Wote wanapaswa kushirikiana kwa dhati ili kuhakikisha kuwa hatua hii inaleta matokeo chanya kwa Taifa.