Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wachumi wachambua nyongeza ya mshahara ya Serikali

Muktasari:

  • Kuanzia Julai mosi, 2025 kima cha chini cha mshahara kitakuwa Sh500,000 kutoka Sh370,000 iliyokuwa ikilipwa kabla ya makato ya kodi. Wachumi waeleza kuwa italeta nafuu ya maisha na kusisimua uchumi.

Dar es Salaam. Mei Mosi ya mwaka huu imeacha kicheko kwa maelfu ya watumishi wa umma baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza nyongeza ya kima cha chini cha mshahara kwa asilimia 35.1 kuanzia Julai mosi, 2025.

Hii inakuwa mara ya pili kwa Samia kuongeza mshahara kwa kiwango kikubwa baada ya kuongeza kwa asilimia 23.3 mwaka 2022. Hatua hiyo inachambuliwa na wachumi kuwa italeta nafuu ya maisha na kusisimua uchumi.

Kwa tangazo hilo la Rais, sasa kima cha chini cha mshahara kitakuwa Sh500,000 kutoka Sh370,000 iliyokuwa ikilipwa kabla ya makato ya kodi.

Akiwahutubia wafanyakazi waliofurika katika Uwanja wa Bombadia mjini Singida, ambako maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu yalifanyika kitaifa, Rais Samia alisema Serikali imeongeza kiwango hicho cha mshahara kutokana na uchumi kukua.

"…Kwa kuwa mcheza kwao hutunzwa, mimi na wenzangu, baada ya kuangalia uchumi ulivyopanda, ninayo furaha kuwatangazia kwamba, katika kuzidi kuleta ustawi kwa wafanyakazi, mwaka huu Serikali itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1," alisema Rais Samia.

Rais Samia, akizungumzia ngazi nyingine za mishahara, aliahidi kuwa nazo zitapanda kwa kiwango kizuri kulingana na bajeti inavyoruhusu.

Akizungumzia hatua hiyo, mchambuzi wa masuala ya fedha, Dk Thobias Swai, amesema ongezeko hilo la mshahara ni hatua nzuri yenye matokeo chanya katika uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Dk Swai, ambaye ni mhadhiri wa masomo ya fedha wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema ni jambo lililotegemewa kwa muda mrefu kwani hali ya maisha imekuwa ikibadilika, lakini eneo hilo halijakumbukwa.

"Ni ongezeko kubwa ambalo pengine halijawahi kutokea, lakini lilitegemewa kwa muda mrefu kwani gharama za maisha zimepanda. Huduma za usafiri, chakula, matibabu na nyingine muhimu zote zimepanda," amesema Dk Swai.

Amesema pamoja na kugusa uchumi wa wale ambao wataongezewa mshahara, pia uchumi wa nchi utachangamka kwa kuwa waliokuwa wakilipwa chini ya kiwango hicho ni wengi na hao wote sasa watakuwa na uwezo wa kutumia.

Aidha, ametoa tahadhari kwa waliongezewa, akisema wanapaswa kujipanga na kutumia nyongeza hiyo vizuri, kwani inaweza kuwaletea maendeleo.

"Kwa nyongeza hiyo ya mshahara mtu unaweza kukopa au kutunza akiba itakayomwezesha kufanya ujasiriamali wa kukuza kipato lakini pia kukidhi mahitaji ya kila siku," amesema.

Mhadhiri wa Uchumi wa UDSM, Profesa Abel Kinyondo naye anaunga mkono athari chanya zilizoelezwa na Dk Swai, akisema ongezeko hilo litaongeza mzunguko wa fedha katika uchumi na kuongeza ukuaji wake.

"Mzunguko wa fedha unaongezeka watu wakiwa na fedha mfukoni, na hatua ya kuongeza mshahara inamaanisha watu watakuwa na fedha zaidi mifukoni mwao. Fedha zikiwa nyingi, watu wanatumia zaidi na uchumi unasisimuka," amesema.

Amesema nyongeza hiyo huenda ikakuza sekta nyingi, kwani kwa ambao kipato kimeongezeka wataongeza mlo na hata kubadilisha huduma tofauti wanazopata katika jamii.

Hata hivyo, Dk Kinyondo ametoa tahadhari kwa wafanyakazi kutokuwa na matarajio makubwa, kwani kwa mfumo wa kodi wa nchi ulivyo, kadri kipato kinavyoongezeka ndivyo viwango vya kodi vinavyozidi kuwa juu.

"Muhimu ni kutokuwa na matarajio makubwa, kwani kodi hutozwa kulingana na kipato, lakini kwa vyovyote vile kutakuwa na athari chanya," amesema.