Rais Samia atangaza kuongeza mishahara kwa wafanyakazi

Muktasari:
- Taarifa ya nyongeza ya mshahara iliyoibua matumaini mapya kwa watumishi wa umma, imetolewa leo na Rais Samia Suluhu wakati wa maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Singida
Dar es Salaam. Mei mosi ya kicheko kwa watumishi wa umma, hivi ndivyo inavyoweza kuelezewa baada ya kutangazwa kwa nyongeza ya kima cha chini cha mshahara kwa asilimia 35.1.
Kutokana na nyongeza hiyo itakayoanza Julai mwaka huu, kima cha chini cha mshahara sasa kitakuwa Sh500,000 kutoka Sh370,000 iliyokuwa ikilipwa kabla ya makato ya kodi.
Taarifa hiyo iliyoibua matumaini mapya kwa watumishi wa umma, imetolewa leo Alhamisi Mei mosi, 2025 na Rais Samia Suluhu wakati wa maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Singida.

Akiwatuhubia wafanyakazi waliofurika katika Uwanja wa Bombadia yalikofanyika maadhimisho hayo, Rais Samia alisema Serikali imeweza kuongeza kiwango hicho cha mshahara kutokana na uchumi kukua.
“Kwa mapenzi makubwa na kwa namna mlivyoiunga mkono Serikali tulipowaomba mfunge mkanda na mkaamua kujituma na kufanya kazi kwa bidii na kufanya uchumi wetu ukue kwa asilimia 5.5 mwaka huu.
“Kwa kuwa mcheza kwao hutunzwa mimi na wenzangu, baada ya kuangalia uchumi ulivyopanda ninayo furaha kuwatangazia kwamba, katika kuzidi kuleta ustawi kwa wafanyakazi, mwaka huu Serikali itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1,” amesema Rais Samia.
Rais Samia akizungumzia ngazi nyingine za mshahara, aliahidi kuwa nazo zitapanda kwa kiwango kizuri kulingana na bajeti inavyoruhusu huku akiwahakikishia watumishi hao kuwa kutakuwa na nyongeza nzuri na kubwa.
Sekta binafsi
Wakati hali ikiwa hivyo kwa watumishi wa umma, mambo bado magumu kwa wale wa sekta binafsi.
Hata hivyo, kwa kutambua hilo, Rais Samia katika hotuba yake ameitaka bodi ya kima cha chini cha mshahara kwa sekta hiyo, kuharakisha mapitio ya viwango vya chini vya mishahara kwa sekta hiyo.
“Naendelea kuhimiza wizara na vyama vya wafanyakazi kufanya mijadala na waajiri ili kutekeleza mikataba ya hali bora ya wafanyakazi katika sekta binafsi kusudi waendane na wenzao wa sekta ya umma. “Tutaendea kuboresha mazingira ya kazi ikiwamo masilahi ya wafanyakazi kadiri hali ya uchumi itakavyoruhusu,” amesema Rais Samia.
Amesema kwa sasa dunia imepata mtikisiko wa kiuchumi kutokana na kubadilika mwelekeo wa kisiasa za kanda na umeleta mabadiliko kwenye sera za kifedha na kupunguza misaada ya maendeleo kutoka kwa wabia.

Kutokana na hilo, Rais huyo amesema ni muhimu kwa nchi kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato ndani na kubana matumizi ili kuweka kutekeleza majukumu ya msingi ya ujenzi wa nchi na utoaji wa huduma za kijamii.
“Huu ni wakati ambao wafanyakazi, waajiri na Serikali tunapaswa tushikamane katika vita hii ya kiuchumi ili tusiiyumbishe nchi yetu,” amesema.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi alisema tofauti na miaka mingine, maadhimisho ya siku ya wafanyakazi mwaka huu, hakuna malalamiko makubwa kutokana na Serikali kuzifanyia kazi changamoto nyingi zilizoainishwa miaka ya nyuma.
Amesema, “nimesikiliza kwa makini risala yenu wafanyakazi iliyosomwa na katibu mkuu Tucta, tofauti na miaka mingine mwaka huu pamoja na kuanisha maeneo ya maboresho na kutoa mapendekezo nimefarijika kusikia risala yenu ikipongeza na kuwa wingi wa shukrani kwa Serikali.

“Hii inatokana na kwamba vyama vya wafanyakazi vimekuwa vikiwasilisha hoja, ushauri na mikakati ya kukabiliana na changamoto zenu kwa weledi serikalini, lakini hata kwa waajiri.
“Niwahakikishie kuwa, hatutayapuuza maombi yenu na hatutapunguza utashi wa kisiasa kwenye kuyashughulikia.”
Pia, aliwataka wafanyakazi kote nchini kuwa vinara wa kulinda amani na kuhakikisha utulivu unaendelea kutawala nchini.
Amesema, “ili tuweze kujenga vyema Taifa letu ni lazima tuimarishe amani na utulivu nchini. Kwa namna yoyote ile tusitoe fursa kwa vyama vya wafanyakazi kutumika kuichafua nchi yetu.
“Historia ya vyama vya wafanyakazi ni vyama vilivyotumika kuleta vuguvugu la uhuru wa nchi hii, sasa tusijibadilishe tukawa vyama vya kusaliti uhuru wetu tulioutafuta kwa nguvu kubwa.”
Katibu Mkuu Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Hery Mkunda amesema Serikali imetengeneza mazingira bora yanayoboresha maisha na masilahi ya wafanyakazi.
Mafanikio hayo ni pamoja na punguzo la kiwango cha makato ya kodi inayotokana na mshahara (Payee) kutoka asilimia tisa hadi nane kwa msharaha wa kima cha chini, mipango ya motisha kwa watumishi wa taasisi za umma.
“Maboresho ya mifuko ya hifadhi ya jamii iliyowezesha kulipwa kwa mafao ya wastaafu waliongoja kwa muda mrefu. Katika kipindi chako, kikokotoo kilipanda kutoka asilimia 33 hadi 40 kwa watumishi wa umma na asilmia 25 hadi 35 kwa watumishi sekta binafsi.
“Kuongezeka kwa kima cha chini kwa pensheni kwa wastaafu kutoka Sh100,000 kwa mwezi hadi Sh150,000. Wastaafu kuendelea kupata huduma za matibabu, ulinzi na usimamizi wa usalama wa wafanyakazi kupewa kipaumbele na umri wa mtoto mnufaika wa bima ya afya umeongezeka kutoka miaka 18 hadi 21,” amebainisha.
Aidha, Mkunda amesema kuondoa tozo ya asilimia sita kwa wanufaika wa mkopo wa elimu ya juu iliyokuwa kero kwa wafanyakazi, kupunguza tatizo la ajira, kupandishwa madaraja kwa watumishi wa umma kwa asilimia 90 sambamba na kuongezwa likizo kwa wazazi waliojifungua mtoto njiti.
Ujumbe wa ATE, ILO
Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Oscar Mgaya amesema wafanyakazi wanapaswa kuepusha migogoro isiyo ya lazima kwa kufuata mifumo ya majadiliano.
“Niwaombe wafanyakazi kutumia mifumo ya majadiliano na miongozo mahali pa kazi kutatua changamoto ili kuepusha migogoro isiyo na lazima,” amesema Mgaya.
Amesema ushirikiano kati ya Serikali, waajiri na wafanyakazi ikiwa ni mfumo wa utatu ndiyo msingi wa mafanikio katika kuboresha haki mazingira rafiki ya kazi na uzalishaji.

Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Caroline Mugalla amesema shirika hilo limeendelea kushirikiana bega kwa bega na Serikali katika kuboresha mazingira ya ufanyajikazi kwa wafanyakazi wa Tanzania.
“ILO inashirikiana na Serikali vyama vya wafanyakazi na waajiri, ikiwamo katika sera, mipango ya kazi zenye staha, bima, sekta isiyo rasmi, kutoa mafunzo kwa maofisa kazi na kutokomeza utumikishaji wa watoto, yote ikiwa ni kuboresha mazingira,” amesema.
Dk Mpango anena
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango amesema wafanyakazi wananguvu ya kuiweka Serikali madarakani, hivyo wanapaswa kujiandikisha kisha kupiga kura ifikapo Oktoba.
“Niwasihi sana wafanyakazi, asibakie hata mmoja wa sekta ya umma au binafsi ambaye hatajiandikisha kwenye daftari la kudumu na siku ya uchaguzi asibakie hata mmoja nyumbani twende wote tukapige kura,” amesema Dk Mpango.
Mbali na nguvu ya kisiasa, alisema nguvu ya wafanyakazi kiuchumi ni utendaji kazi wao ndiyo unakuza uchumi nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akiwa na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson pamoja na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Tumaini Nyamhokya wakiimba Wimbo wa Mshikamano (Solidarity Forever) kwenye Maadhimisho ya Siku wa Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ambapo Kitaifa Sherehe hizo zimefanyika katika uwanja wa Bombadia Mkoani Singida tarehe Mei 1, 2025.
“Duniani kote wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi, ndiyo nguvu kuu ya uchumi wa nchi, hivyo tunaposherehekea siku hii katika kipindi hiki cha awamu ya Rais Samia licha ya magumu ya uchumi yanayoendelea duniani, uchumi wa Tanzania umeimarika sana katika kipindi hiki ukilinganisha na nchi nyingine zinazolingana na sisi, hivyo pongezi za dhati kwa wafanyakazi wa Tanzania,” amesema Dk Mpango.
Migogoro vyama vya wafanyakazi
Kuhusu migogoro inayoendelea kwenye vyama vya wafanyakazi hali inayosababishwa kuibuka kwa vyama vipya Rais Samia ameitaka Tucta kuhakikisha vyama vya wafanyakazi vinatoa huduma na kusimamia kikamilifu masilahi ya wanachama ili kuwaepusha na ushawishi wa namna unaoweza kuwasababishia kujitoa kwenye vyama na kuunda vingine.
Rais Samia amesema uundaji wa vyama vya wafanyakazi hautaingiliwa na chombo chochote ikiwamo Serikali.
“Natamani kuona Tucta inayochangia kuongeza tija na ufanisi katika kazi, hali itakayochagiza maendeleo zaidi nchini kwetu. Endeleeni kutetea haki za wafanyakazi wote nchini wakiwamo wa ofisi za Tucta, wafanyakazi wenu wenyewe ambao wana madai mbalimbali ya stahiki zao. Muwakumbushe wafanyakazi wajibu wao katika sehemu za ajira na nchi yao pia,” amesema.