Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wafanyakazi wafurahia nyongeza ya mshahara

Muktasari:

  • Nyongeza ya asilimia 35.1 ya mshahara imetangazwa leo na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei mosi) na kubainisha kuwa ngazi nyingine za mishahara pia zitapanda kulingana na uwezo wa bajeti ya Serikali.

Dar/mikoani. Wafanyakazi wa umma nchini wamepokea kwa furaha nyongeza ya mshahara wa kima cha chini kutoka Sh370,000 hadi Sh500,000, wakitaja kuwa ni hatua chanya kuelekea kufikia viwango bora zaidi vya masilahi.

Nyongeza hiyo ya asilimia 35.1 imetangazwa leo na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Mei mosi na kubainisha kuwa ngazi nyingine za mishahara pia zitapanda kulingana na uwezo wa bajeti ya Serikali. Hatua hiyo inatarajiwa kuanza kutekelezwa Julai 2025.

"Tumeipokea nyongeza hiyo kwa matumaini makubwa,  tunaamini Serikali itaendelea kuboresha maisha yetu na kuongeza ufanisi kazini," amesema Godfrey Kanju, mfanyakazi kutoka mkoani Iringa.

Hata hivyo, baadhi ya watumishi wa kada ya kati na juu katika mkoa huo, walieleza kutoridhishwa na nyongeza hiyo kwa madai kuwa, haitoshelezi matarajio yao na bado kuna pengo kubwa la mishahara kati ya kada mbalimbali.

"Serikali iendelee kupitia upya viwango vya mishahara ili kuhakikisha haki na usawa kwa watumishi wote," amesema Anjelika Mwano, mwalimu kutoka Iringa.

Mkoani Njombe, mmoja wa watumishi kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Wiston Kilangi alisema kauli ya Rais imeleta faraja na matumaini kwa wafanyakazi waliokuwa wakingoja kwa hamu kusikia hatua hiyo.

"Tulikuwa na shauku kubwa ya kumsikia Mheshimiwa Rais katika maadhimisho ya Mei mosi, na kauli yake ya kuongeza mshahara imetufurahisha sana. Tunaahidi kuendelea kuchapa kazi kwa bidii zaidi," amesema Kilangi.

Kutoka mkoani Simiyu, Kulwa Dwese, ambaye ni Mwenyekiti wa Tucta Mkoa wa Simiyu amesema nyongeza hiyo inaleta unafuu kwa wafanyakazi wengi, huku Ahamed Makono wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa akisema itachochea bidii na tija kazini.

Devotha Soko wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) amesema hatua hiyo ni uthibitisho kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya Taifa.

Mkoani Tabora, mfanyakazi Ibrahim Songoro amesema gharama za maisha zimepanda na kuwa nyongeza hiyo itawasaidia kutosheleza mahitaji yao.

Advera Sizya ambaye ni mtunza hifadhi ya barabara, amesema Rais ameendana na hali halisi ya maisha, jambo litakaloongeza ari ya wafanyakazi kazini.

Pia, Matilda Moshi ambaye ni askari muhifadhi, alisema nyongeza hiyo inaweza pia kupunguza tamaa za rushwa, kwani mshahara unatarajiwa kuridhisha na kuleta ustawi kwa wafanyakazi.

Mkoani Mbeya, Ezekiel Kamanga ambaye ni mwalimu mstaafu na mfanyakazi wa taasisi binafsi, amesema ongezeko hilo litasaidia kuongeza motisha kwa watumishi wa umma na kuwaondoa katika hali ya unyonge, ingawa alionya kuwa, mfumuko wa gharama za maisha utaongezeka kutokana na ongezeko la mzunguko wa fedha kuanzia Juni mwaka huu.

Zamda Mickdad, pia amepongeza hatua hiyo, akisema itawaondoa wafanyakazi katika tabia ya kutegemea mikopo kutokana na mshahara mdogo na kuongeza hamasa ya utendaji kazi.

Wafanyakazi wa Taasisi mbalimbali Mkoa wa Pwani wakiwa kwenye maandamano wakati wa madhimisho ya siku ya wafanyakazi yaliyofanyika Kibaha kwa ngazi ya Mkoa wa Pwani. Picha na Sanjito Msafiri

Mkoani Shinyanga, Jacob Amos amesema ongezeko la asilimia 35 ni ndogo, wakati Kareny John yeye akisema ongezeko ni zuri, lakini bado mshahara haukidhi mahitaji kutokana na kupanda kwa gharama za bidhaa na huduma.

Kutoka wilayani Simanjiro, Mwalimu wa Shule ya Msingi Edonyongijape, Alexander Njau, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza mshahara wa watumishi wa kima cha chini hadi Sh500,000, akisema ahadi hiyo imekamilika na inawafaidisha sana.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji wilayani Babati, Ally Omary, amesema ongezeko hilo ni muhimu kwa watumishi wa kima cha chini, likiwaongezea morali ya kazi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, akihutubia sherehe za Siku ya Wafanyakazi, ameagiza taasisi zinazohusika na usimamizi wa masilahi ya wafanyakazi kutoa taarifa ya kina ndani ya siku saba kuhusu hatua zitakazochukuliwa kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi, hasa katika sekta binafsi.

"Leo tunaposherehekea sikukuu hii, watumishi tukumbuke kuwa tunabeba taswira ya Serikali. Hivyo, tuendelee kufanya kazi kwa moyo wa kujitolea na kwa ajili ya maslahi ya umma," amesema Chalamila.


Imeandikwa na Christina Thobias (Iringa), Seif Jumanne (Njombe), Samwel Mwanga (Simiyu), Hawa Kimwaga (Tabora), Hawa Mathias (Mbeya), Hellen Mdinda (Shinyanga), Sanjito Msafiri (Kibaha), Joseph Lyimo (Manyara) na Nasra Abdallah (Dar es Salaam).