Mwendokasi unahitaji usimamizi, thabiti

Mradi wa mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam ulipoanza ulikuwa kivutio kikubwa kwa wakazi na wageni waliotembelea jiji hili la kibiashara nchini Tanzania. Kwa mara ya kwanza, jiji lilionekana kuingia katika hatua ya kisasa ya usafiri wa umma hali ambayo iliwavutia hata wale waliokuwa wamezoea kutumia magari binafsi kuingia na kutoka katikati ya jiji.
Wengi waliamua kuyaacha magari yao, hasa eneo la Kimara, na kutumia usafiri wa mwendokasi ili kuepuka kukwama kwenye foleni ndefu, jambo lililosaidia kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji na kupunguza uzalishaji wa hewa chafu.
Mradi huu uliibua matumaini na matarajio makubwa kwa mustakabali wa usafiri wa umma nchini. Nakumbuka mwaka mmoja baada ya uzinduzi wake, wahariri wa vyombo vya habari kutoka nchi jirani walifika kuutembelea.
Tulikutana nao na hawakusita kuusifia mradi huu huku wakichukua ‘selfie’ na kusambaza picha mitandaoni wakionyesha jinsi walivyofurahishwa na hali ya kisasa ya usafiri wetu.
Hali hii haikuishia kwa wageni pekee. Nilishuhudia wabunge, mawaziri, na maofisa wa Serikali wakitumia usafiri huu kama raia wa kawaida. Ni jambo lililotoa picha ya kuungwa mkono kwa dhati kwa mradi huu.
Mabasi yalikuwa mapya, mfumo wa kulipia nauli ulikuwa wa kidijitali, na ulinzi pamoja na usalama kwenye vituo ulikuwa wa kuridhisha.
Lakini hali hiyo haijadumu. Katika miaka ya hivi karibuni, hali ya mradi wa mwendokasi imekuwa ya kusikitisha. Malalamiko ya abiria yameongezeka. Mabasi yamekuwa machache mno ukilinganisha na idadi kubwa ya watu wanaohitaji huduma.
Hali hii ni mbaya zaidi wakati wa asubuhi na jioni nyakati ambazo watu wanasafiri kwenda na kurudi kutoka kazini. Huu ndiyo wakati ambao huduma ilipaswa kuwa imara zaidi, lakini badala yake, ndiyo wakati wa changamoto kubwa zaidi.
Ukitembelea kituo cha Kimara Mwisho asubuhi, utaona abiria wakisukumana, wakipigana vikumbo ili kuingia kwenye basi. Wengine hulazimika kusubiri kwa zaidi ya saa moja kabla ya kupata basi, na baadhi huchelewa kazini au shuleni. Hali hii siyo tu inadhalilisha hadhi ya mradi huu, bali pia inaathiri uzalishaji wa wananchi ambao hutegemea usafiri huu kila siku.
Ni wazi kuwa hali hii haiwezi kuachwa iendelee. Ni lazima hatua zichukuliwe. Kwa bahati nzuri, Serikali na wadau wake wameanza kuchukua hatua. Hivi karibuni nimesikia Serikali imetangaza kuweka watoa huduma binafsi wawili katika awamu tofauti ili kuimarisha huduma.
Hatua hii ni ya msingi sana. Kwanza, inatoa fursa ya ushindani ambao unaweza kuleta mabadiliko ya haraka. Kwa kuwa na watoa huduma wengi wa sasa watajitathmini na kuboresha huduma zao. Pili, watoa huduma wapya wataleta mabasi zaidi, kuongeza idadi ya safari, na hivyo kupunguza msongamano kwenye vituo.
Ni matumaini yetu kuwa hatua hizi zitabadilisha taswira ya sasa ya mradi. Lakini ni muhimu pia kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mipango hii unafanyika kwani bila shaka vigezo vya kuteua mtoa huduma vimezingatia uwezo wa kifedha, uzoefu, idadi na ubora wa mabasi, pamoja na uwezo wa kiufundi na rasilimali watu.
Kuna haja pia ya kuhakikisha mfumo wa ulipaji wa nauli unaboreshwa zaidi kwa kuondoa changamoto za kadi, mashine kutofanya kazi, na nauli kutoeleweka wazi kwa abiria.
Tukikubali hali ya sasa iendelee kwani, tutakuwa tumepoteza siyo tu fedha nyingi zilizowekezwa kwenye miundombinu ya mwendokasi bali pia imani ya wananchi kwa Serikali yao. Mradi huu ni alama ya maendeleo ya usafiri wa umma Tanzania, na haifai kuiacha idhoofike mikononi mwa uzembe, kutowajibika, au mifumo duni ya usimamizi.
Kwa hiyo, wakati huu ambao Serikali imeamua kufungua ukurasa mpya kwa kuwapata watoa huduma wapya, basi iwe ni fursa ya kurekebisha kasoro zilizopo.
Tusiruhusu tena abiria kupigania nafasi kwenye mabasi, tusiruhusu huduma kudidimia kila siku. Na tusisahau kwamba usafiri wa umma bora ni kiini cha maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na kimazingira kwa jiji lolote linalotaka kustawi.
Bila shaka wanahabari wenzangu tutaendelea tutaendelea kuandika siyo kwa nia ya kubeza, bali kuibua changamoto kwa lengo la kupata suluhisho.
Kama tulivyosifia mwanzoni, basi hatuna budi pia kukosoa na kushauri pale inapobidi. Mradi huu bado unaweza kurudi katika ubora wake wa awali ikiwa tu kila mhusika atawajibika ipasavyo.