Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sekta binafsi kukakibidhiwa Mwendokasi ya Kimara na Mbagala

Muktasari:

  • Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) ambayo sasa ndiyo inayotoa huduma itahamishiwa katika mradi awamu ya tatu unaokwenda Gongo la Mboto kutokea katikati ya jiji jambo litalokwenda sambamba na kuwaalika wabia wa kimkakati kuuza baadhi ya hisa.

Dar es Salaam.  Wakati kilio cha wakazi wa Dar es Salaam juu ya magari yaendayo haraka kikizidi kushikika kila siku, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema sekta binafsi itakabidhiwa uendeshaji wa awamu ya kwanza na pili ya mradi wa mabasi hayo.

Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) ambayo sasa ndiyo inayotoa huduma itahamishiwa katika mradi awamu ya tatu unaokwenda Gongo la Mboto kutokea katikati ya jiji jambo litalokwenda sambamba na kuwaalika wabia wa kimkakati kuuza baadhi ya hisa.

Mchechu anatoa kauli hii ikiwa ni siku chache tangu Mwananchi kuripoti magumu wanayokutana nayo watumiaji wa usafiri huu jambo linaloondoa maana ya azma iliyokuwapo awali ya uanzishwaji wake.

Kauli hii pia inatolewa wakati ambao kipande cha video kilisambaa katika mitandao ya kijamii kikionyesha watu wakigombania kuingia ndani ya basi hilo huku wengine wakipitia madirishani jambo lililozua mjadala katika mitandao ya kijamii.

Mchechu amesema hayo leo Juni 2, 2025 wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa vyombo vya habari jijini hapa akielezea safari ya mageuzi, mafaniko, mikakati na muelekeo wa ofisi yake.

Amesema kwa sasa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) wanaosimamia miundombinu, wanaendelea kuangalia kampuni nyingine zitakazofanya uwekezaji wakati ambao awamu ya kwanza na pili ujenzi umekamilika na awamu ya tatu ikitarajiwa kukamilika kabla ya mwaka kuisha.

Kukamilika kwa awamu zote za ujenzi zilizopangwa kufanyika, inaweka nafasi ya kuwa na watoa huduma wanne hadi sita badala ya kuwa na mtoa huduma mmoja (Udart).

“Hali hii ilifanya ndani ya Udart kuwa na matatizo yaliyojitokeza, Serikali iliamua kuichukua pamoja na yote yaliyokuwamo ikiwamo ubadhirifu kama ambavyo mlisikia, ndiyo maana hatua za kisheria na Mahakama zilichukuliwa na sasa Serikali inamiliki asilimia 85,” amesema.

Akizungumzia suala la kuongeza ufanisi na kuondoa malalamiko yaliyopo, Mchechu amesema awamu ya kwanza ya mradi inayokwenda Kimara hadi Kivukoni, itakuwa chini ya sekta binafsi, sambamba na awamu ya pili inayotoka Gerezani kwenda Mbagala.

“Awamu ya tatu ndiyo itakuwa chini ya Udart, lakini ile kampuni (Udart) tulikuwa hatujaifanyia mageuzi ya kina, ndiyo maana iko pale na watu wanalalamika haifanyi vizuri ni kwa sababu ilipita changamoto za uongozi mbaya ndiyo maana Serikali iliichukua,” amesema.

“Pia, Udart ili kuwe na governance (uongozi) nzuri tutaalika baadhi ya wabia wa kimkakati na baadhi ya hisa zitauzwa lakini tunahitaji walau miaka miwili ya kufanya mageuzi,” amesema.

Akizungumzia mabasi 100 aliyoahidi kuwa yatanunuliwa alipokuwa akizungumza na wanahabari Julai 15 mwaka jana, Mchechu amesema kwa sababu walihitaji yale yanayotumia gesi asilia tayari moja la mfano limeshakuja nchini na linafanya kazi.

“Tunakamilisha taratibu na watengenezaji wanaendelea na mabasi mengine 99 na tunaamini kuwa yote yatakuja, kwa hiyo mwaka huu mabasi hayo yataingia na mengine 70 yako kwenye maboresho kwa kubadilishwa ili yaweze kutumia gesi asilimia,” amesema Mchechu.

Amesema anaamini mabasi yaliyoahidiwa yatakapoingia,  malalamiko yaliyopo yatatulia lakini pia ili yafanye kazi kwa ufanisi, zinahitajika kampuni nyingine zitazofanya kazi hiyo.

Alipozungumza Julai mwaka jana, Mchechu alisema mabasi hayo 100 yanatarajiwa kununuliwa na kuingizwa kutoa huduma kwenye njia kuu za awamu ya kwanza ya mradi, akieleza mchakato umekwishaanza kwa kushirikiana na Benki ya NMB itakayofadhili kwa kutoa mkopo.

Akizungumza mwaka jana alisema, “Kesho (Julai 16, 2024) nitakuwa na kikao na NMB kwa ajili ya ununuzi wa mabasi 100, hivyo tutatatua changamoto ya uchache wa mabasi.”

Kwa mujibu wa Mchechu, mabasi hayo 100 yatakuwa yamefika ndani ya miezi sita kuanzia siku aliyozungumza, huku njia zingine za mlisho ambazo ujenzi wake unaendelea zikisubiri utaratibu mwingine.

“Nimefanya mikutano na watu wa Dart na Udart pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) na sasa tumeshafikia ukingoni,” alisema.

Hata hivyo, alisema changamoto za mradi huo ni nyingi na zimechochewa zaidi na mwanzo wa safari yake na kwamba, Serikali imeendelea kuzitatua. Miongoni mwa changamoto hizo ni madeni na mabasi mengi kuharibika.

“Tunafahamu umiliki wa kampuni inayosimamia mradi huu, ilianza ikiwa sekta binafsi na sasa Serikali inamiliki asilimia 85, lakini kulikuwa na mambo mengi ambayo tumeendelea kuyatatua taratibu. Ila mwanzo wa safari ya huu mradi imekuwa changamoto,” alisema Mchechu bila kuingia ndani zaidi, akiahidi Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi wa Dart, watapata fursa ya kuja kueleza mikakati inayoendelea.

Wakizungumzia uamuzi wa kuipa sekta binafsi kuendesha mradi huo baadhi ya watumiaji wa usafiri huo wamesema ni jambo ambalo limechelewa.

“Serikali ingebaki kuwa msimamizi tu, kukusanya kodi na kuhakikisha kila kitu kinachofanywa kiko kwa mujibu wa sheria, mambo ya kutoa huduma wangewaachia sekta binafsi tangu mwanzo haya malalamiko yasingekuwapo,” amesema Rebecca Masha mkazi wa Kimara.