Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kero usafiri wa Mwendokasi zifike mwisho

Ulipoanzishwa mwaka 2016, mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam ulileta matumaini makubwa kwa wakazi waliokuwa wamechoshwa na adha ya daladala. Mradi huu ulikuwa mkombozi wa usafiri wa umma kwa lengo la kupunguza foleni, kuboresha harakati za kila siku na kurahisisha maisha ya wakazi wa jiji. Hata hivyo, matumaini hayo yamegeuka kuwa mateso kwa watumiaji wengi.

Changamoto kubwa ya usafiri huu ni uhaba wa mabasi ukilinganisha na idadi ya abiria wanaohitaji huduma. Asubuhi na jioni vituo hujaa watu kupita kiasi, wengine wakilazimika kusimama kwa saa moja hadi mbili wakisubiri usafiri.

Baadhi ya maeneo, kama Kimara, Fire, Kivukoni na Gerezani, yamekuwa na misongamano isiyovumilika, hali inayosababisha abiria kusukumana, kuanguka na hata kujeruhiwa. Wazee, wagonjwa, watoto na wajawazito wako katika hatari kubwa zaidi, huku afya za wasafiri zikiwekwa rehani kutokana na msongamano unaokinzana na kanuni za usalama wa kiafya.

Mbali na hilo, usimamizi wa huduma bado una mapungufu makubwa. Mabasi yanachelewa, mengine huonekana yameegeshwa bila ratiba inayoeleweka. Wananchi wanalazimika kutegemea bodaboda au bajaji ambazo gharama zake ni kubwa.

Kwa wakazi wa Mbezi na Kimara, hali ni mbaya zaidi baada ya kuondolewa kwa daladala za kwenda mjini moja kwa moja, hali inayowalazimu kutumia mfumo wa usafiri wa kuunganisha.

Ahadi za Serikali kuhusu ujio wa mabasi mapya zimekuwa zikijirudia bila matokeo. Mwaka huu pekee, viongozi kadhaa waliahidi mabasi zaidi ya 250 kutoka China, huku wakieleza kuwa yangewasili Machi au Aprili, miezi ambayo tayari imepita.

Mpaka sasa, hali haijabadilika, huku wananchi wakiendelea kutaabika. Msemaji wa UDA-RT, Gabriel Katanga, alikiri changamoto hiyo na kueleza kuwa mabasi yamechoka kutokana na muda mrefu wa matumizi. Aliahidi mabasi mapya 100, lakini Watanzania wamechoshwa na ahadi zisizotekelezwa na hawaelewi kwa nini mabasi ya awali hayakuweza kujizalisha na kuongezeka, ilhali gharama nyingine kama za miundombinu na mishahara zilishabebwa na Serikali.

Wataalamu wa uchumi na usafiri, akiwemo Dk Lawi Yohana wa Chuo Kikuu Huria Tanzania na Dk Mwinuka Lutengano wa Chuo Kikuu Dodoma, wanashauri Serikali kushirikiana na sekta binafsi (PPP) kuongeza ufanisi wa mradi huo.

Wanasema duniani kote imeonyesha kuwa mfumo wa ushirikiano huu hufanikisha huduma bora kwa umma, huku Serikali ikibaki kuwa msimamizi wa sera na miundombinu.

Serikali inapaswa kuweka kipaumbele cha mradi huu sawa kama ilivyofanya kwenye uendeshaji wa reli ya SGR. BRT inahudumia maelfu ya wananchi kila siku; hivyo inahitaji uwekezaji mkubwa wa mabasi mapya, usimamizi madhubuti na ratiba zinazotekelezeka. Wananchi walihitaji msaada wa usafiri bora lakini walichopata ni adhabu ya kila siku.

Ni wakati sasa wa Serikali kuchukua hatua madhubuti, si kwa matamko, bali kwa vitendo. Kwa kuongeza mabasi, kuboresha usimamizi na kuimarisha miundombinu, BRT inaweza kufikia malengo yake ya awali ya kuwa mkombozi wa usafiri wa umma. Kero hizi zisitazamwe tena kama jambo la kawaida, bali kama dharura inayohitaji suluhisho la haraka na la kudumu.