Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wazawa wakabidhiwa Mwendokasi Mbagala, mabasi 255 kutua, ajira 2,000

Muktasari:

  • Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) awamu ya pili kati ya Gerezani- Mbagala umekamilika zaidi ya mwaka mmoja na kilichokuwa kinasubiriwa ni mabasi ili wananchi waanze kunufaika na uwekezaji huo wa mabailioni ya fedha.

Dar es Salaam. Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Dk Athuman Kihamia amesema mradi wa mabasi yaendayo haraka awamu ya pili utaendeshwa na wazawa ambao wanatarajia kushusha mabasi 255.

Dk Kihamia amesema hayo siku moja baada ya Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu kusema sekta binafsi itakabidhiwa uendeshaji wa awamu ya kwanza na pili ya mradi wa mabasi hayo.

Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) ambayo sasa ndiyo inayotoa huduma, itahamishiwa kwenye awamu ya tatu kutoka katikati ya jiji hadi Gongo la Mboto, jambo litalokwenda sambamba na kuwaalika wabia wa kimkakati kuuza baadhi ya hisa.

Mpango huo ulioelezwa kwa nyakati tofauti Dk Kihamia na Mchechu, unalenga kumaliza kilio cha wakazi wa jiji hilo kuhusu adha wanazopata katika huduma hiyo.

Jana Jumatatu, Juni 2, 2025, Mchechu akizungumza na wahariri jijini Dar es Salaam, alisema Dart wanaosimamia miundombinu, wanaendelea kuangalia kampuni nyingine zitakazofanya uwekezaji, wakati ambao awamu ya kwanza na pili ujenzi umekamilika na awamu ya tatu ikitarajiwa kukamilika kabla ya mwaka kuisha.

Kukamilika kwa awamu zote za ujenzi zilizopangwa kufanyika, kunaweka nafasi ya kuwa na watoa huduma wanne hadi sita badala ya kuwa na mtoa huduma mmoja ambaye ni Udart.

Akizungumzia suala la kuongeza ufanisi na kuondoa malalamiko yaliyopo, Mchechu alisema awamu ya kwanza ya mradi –Kimara hadi Kivukoni, itakuwa chini ya sekta binafsi, sambamba na awamu ya pili –Gerezani hadi Mbagala.

Leo Jumanne, Juni 3, 3035, Dk Kihamia akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu akiwa nje ya nchi, amesema wameingia mkataba na Mofat Company Limited: “Kuanzia Juni na ni mkataba wa miaka 12 ili kuendesha mradi wa njia ya Mbagala.”

Amesema kampauni hiyo ni ya wazawa ambao wanatarajia kuanza Agosti 2025: “Wataingiza mabasi 255 yanayotumia gesi,” amesema.

Hata hivyo, hakueleza inamilikiwa na nani lakini amesema ni wazawa walioungana na wamehakikisha hakutakuwa na tatizo.

Dk Kihamia amesema awamu ya kwanza njia ya Kimara- Morocco- Kivukoni na Gerezani itaendeshwa na Kampuni ya Emirates National Group (ENG) kwa kipindi cha miaka 12 na anatarajia kushusha mabasi 177.

Mbali na mabasi hayo yanayofika Agosti, Dk Kihamia amesema Septemba kuna mabasi mengine 200, Novemba 200 na baadaye 100 kwa njia zote.

Akijibu swali aliloulizwa thamani ya mkataba, Dk Kihamia amesema: “Kila awamu ni Sh750 bilioni kila mkataba – yaani miundombinu na mabasi.”

Alipoulizwa kwa nini kumekuwa na ahadi nyingi zinazotolewa lakini utekelezaji unasuasua, Dk Kihamia amesema wananchi wasubiri kuona mabadiliko makubwa ya kiutendaji na usafiri kwani Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuboresha huduma ya usafiri katika jiji hilo.

“Suala la hali ya usafiri wa kugombania au kusubiria muda mrefu sasa litakuwa historia,” amesema Dk Kihamia.

Aidha, amewataka wazawa wenye uwezo wa kimitaji na kiuendeshaji, “wachangamkie zabuni hizi kwani bado zinaendelea kwa barabara za Mwenge hadi Tegeta na zile za Gongo la Mboto hadi mjini na pia na nyinginezo kadri zitakavyotangazwa.”

Amesema hivi sasa hawazungumizii ahadi tena, bali ni utekekelezaji baada ya mikataba kusainiwa.

“Ni hivi, mwanzo tulikuwa tunazungumzia matamanio au matarajio ila sasa ni mikataba ambayo imeshasainiwa. Hawa wazawa wameungana kwa hiyo tumesaini nao mkataba baada ya kuonyesha uhakika wa kupata mtaji. Ni kiasi kikubwa cha fedha,” amesema.

Mathalani, amesema mwekezaji katika awamu ya kwanza anahitaji kuleta mabasi yenye thamani ya zaidi ya Sh150 bilioni

“Hii kampuni ya wazawa inahitaji mtaji wa zaidi ya Sh250 bilioni ili kuleta mabasi hayo 255. Unaweza kuona ukubwa wa mtaji. Mwanzo hata sisi tulikuwa na wasiwasi na uwezo wa wazawa wa kuutekeleza mradi huo, ila baada ya kuungana wameweza kuleta uthibitisho wa benki kwamba na sasa tunakwenda vizuri,” amesema.

Kupitia miradi hiyo, jumla ya ajira 2,100 zinatarajia kutengenezwa wakati wa utekelezaji wa awamu hizi mbili za mradi.

“Tumekubaliana madereza wanaoendesha daladala katika njia hizo kwa sasa ndiyo wafundishwe ili wapate sifa za kuendesha mabasi ya mwendokasi,” amesema Dk Kihamia akisisitiza kwa sasa yeye na wenzake wapo China ambako wanaangalia utengenezaji wa mabasi hayo kiwandani.

Mabasi ya awamu ya kwanza yatatumia dizeli. Yale ya awamu ya pili yatatumia gesi asilia.

Ujio huo wa mabasi ni miongoni mwa ahadi alizotoa Rais Samia katika salamu zake mwaka mpya Desemba 31, 2024 aliposema katika mwaka 2025 miongoni mwa miradi itakayotekelezwa kwa njia ya ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) ni wa BRT.

Alieleza Serikali itatoa kipaumbele kutekeleza miradi ya kupunguza msongamano katika majiji likiwamo la Dar es Salaam, kwa kutekeleza awamu ya tatu na ya nne ya miundombinu ya barabara za Mwendokasi na kuanza huduma kwenye awamu ya pili kwa njia ya Mbagala.