Motsepe anastahili pongezi na heshima CAF

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Dk Patrice Motsepe. Picha na Mtandao
Machi 12, 2025, mkutano mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) uliofanyika Cairo, Misri ulimpitisha Dk Patrice Motsepe bila kupingwa kuwa Rais wa shirikisho hilo kwa miaka minne ijayo.
Uamuzi huo unamfanya Motsepe awe na fursa ya kuongoza kwa miaka mingine minne taasisi hiyo ambayo ina mamlaka ya juu zaidi kwa mchezo wa mpira wa miguu Afrika kwani awamu ya kwanza ilianza 2021 na imefikia tamati mwaka huu.
Ni jambo ambalo lilitegemewa na wengi kwa Motsepe kupewa tena imani na nchi wanachama wa CAF kuendelea kuliongoza shirikisho hadi 2029.
Bilionea huyo kutoka Afrika Kusini amefanya mengi katika kipindi chake cha miaka minne ya nyuma ambayo amekuwa Rais wa CAF na hapana shaka yanawapa wengi matumaini kuwa akiendelea kuwepo katika nafasi hiyo, kuna hatua kubwa zaidi ambazo mpira wa Afrika utapiga.
Kwanza ni kupandisha thamani ya mashindano yaliyo chini ya CAF kwa maana ya yale yanayohusu timu za taifa na yale ya klabu.
Kuna mambo kadhaa ambayo uongozi wa Motsepe umeyafanya katika kufanikisha hilo ambayo la kwanza ni kuongeza kiwango cha fedha za zawadi kwa timu kulingana na nafasi ambazo zinamaliza katika zinazoshiriki.
Mfano wakati anaingia madarakani, Motsepe alikuta bingwa wa Fainali za Mataifa ya Afrika anapata kiasi cha Dola 4.5 milioni lakini hivi sasa, timu inayochukua ubingwa inapata kitita cha Dola 7 milioni.
Katika mashindano ya ngazi ya klabu kwa mfano wakati Motsepe anaingia madarakani mshindi alikiwa anapata Dola 2.5 milioni na hivi sasa zawadi kwa timu mshindi ni Dola 4 milioni.
Kuna jambo lingine ambalo Motsepe amelifanya nalo ni kutoa ruzuku kwa klabu zote zinazoshiriki mashindano ya CAF kwa maana ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika ambapo zile zinazoishia hatua za awali kila moja inapata gawio la Dola 50,000 kwa ajili ya kuzisaidia kumudu gharama za safari na malazi.
Tumeshuhudia pia uongozi wa Motsepe ukianzisha mashindano ya soka kwa ngazi ya shule ambayo yanashirikisha timu za wanawake na timu za wanaume chini ya udhamini wa taasisi yake ya Motsepe ambayo inatoa inatoa fedha za uendeshaji katika mashindano ya kufuzu ngazi ya kanda na pia kwa washindi.
Katika fainali zenyewe za shule Afrika, mshindi anapata Dola 300,000, mshindi wa pili anavuna Dola 200,000 na mshindi wa tatu anapata Dola 150,000, fedha ambazo CAF na Taasisi ya Motsepe wameelekeza zitumike katika kuboresha miundombinu ya soka la vijana hasa mashuleni.
Kwenye upande wa utawala, CAF chini ya Motsepe imeongeza fedha kwa nchi wanachama wake, kanda zake sasa zinapata mgawo lakini pia inatoa kitita cha Dola 50,000 kwa mwaka kwa kila mwenyekiti au Rais wa chama au shirikisho mwanachama wake ili kusaidia uendshaji wa ofisi zao.
Upande wa miundombinu, CAF chini ya Motsepe imeonesha kutoa kipaumbele kikubwa kwa kuhakikisha nchi wanachama wake wanakuwa na viwanja bora na vya hadhi ya juu vinavyokidhi vigezo vya kimataifa vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).
Uongozi wa Motsepe umekuwa hauna msamaha kwa viwanja visivyokidhi vigezo ambapo umekuwa ukivifungia visitumike kwenye mashindano yake jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kufanya mpira uchezeke katika maeneo mazuri ya kuchezea na kutoa fursa kwa wachezaji na timu kuonyesha uwezo na hivyo kukuza ushindani wa soka la Afrika.
Kuna uimara wa kiuchumi ambao CAF imekuwa nao chini ya Motsepe mfano wakati anaingia alikuta kiwango cha upotevu wa kiasi cha Dola 28.9 milioni hadi Dola 9.2 milioni na kwa mara ya kwanza ilishuhudiwa CAF ikipata faida ya Dola 11.7 milioni.
Kwa wenye kumbukumbu ya mpira wa Afrika ulipotokea wakilinganisha na hapa ulipo, ni wazi kwamba kuna hatua kubwa ambao umepiga na sasa unakaribia kule ambako mabara mengine yapo hasa Ulaya ambalo linatazamwa kama kioo cha maendeleo ya mpira wa miguu duniani.
Hakuna namna ambayo unaweza kuyaelezea mafanikio haya ya soka la Afrika bila kutambua na kupongeza kazi kubwa ambayo Motsepe na uongozi wake umeifanya katika kuwezesha ufike hapo ulipo.
Ni jambo la kujivunia kuwa na kiongozi mwenye maono ya mafanikio katika soka na anaonyesha juhudi za wazi za kuhakikisha yanapatikana.