Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tamaa zinavyoponza mabinti vyuoni

Muktasari:

  • Uhuru kupita kiasi, tamaa vyatajwa kuwafanya wanafunzi wa vyuo wajiingize kwenye mambo yasiyofaa.

Dar es Salaam. Wakati ikiaminika kwamba vyuo vikuu ndiko wanakopatikana wasomi na watu wanaojitambua, imebainika kuwa vijana wengi wa sasa katika ngazi hiyo ya elimu ya juu hawawajibiki vile inavyostahili hali inayosababisha wasiutimie vyema uwanja huo wa maarifa.

Malezi duni yanatajwa kusababisha hali hii ambapo si wazazi, jamii wala chuo kinachowajibika kusimamia malezi ya vijana hawa wanapokuwa chuoni hatua inayowafanya kufanya vile wanaovyoona ni sahihi kwao bila kujali madhara yake.

Mbali na hilo tamaa ya kupata vitu vya gharama na maisha mazuri, nayo ni mojawapo ya sababu inayofanywa wanafunzi wa vyuo kujiingiza kwenye mambo yasiyofaa.

Haya yameelezwa na wadau mbalimbali  katikati ya wimbi la tukio la wanafunzi wa kike wa chuo kikuu waliomshambulia na kumdhalilisha mwenzao kwa tuhuma za kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume wa mmoja wa waliomshambulia.

Tukio hilo liliibua mjadala uliosababisha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake  na Makundi Maalumu Dk Dorothy Gwajima kuingilia kati na kuvitaka vyombo husika likiwamo  Jeshai la Polisi kuchukua hatua jambo ambalo utekelezaji wake ulianza Aprili 21, 2025.

Akizunguma na Mwananchi,  mkazi wa Ubungo Riverside Rhoda Malya ambaye pia ni mwalimu wa sekondari,  anasema wanafunzi wengi wa vyuo vikuu wanaharibika kwa kuendekeza tamaa.

Anasema kilichotokea kwa wasichana hao waliomshambulia mwenzao,  ni kielelezo kuwa kuna hali mbaya kwenye taasisi za elimu ya juu,  kwa sababu hakuna mwongozo wa malezi kama ilivyo kwa ngazi nyingine za elimu.

“Nafikiri kuna haja ya kuwa na angalau uangalizi kwa hawa vijana wetu, inawezekana kwa sababu wako vyuoni wazazi wameacha kabisa kuwafuatilia na wao wanajua hilo hivyo wanafanya mambo ya ovyo sana. Unakuta mwanafunzi amepanga kwenye nyumba na ana samani za gharama, simu za bei mbaya unajiuliza hivi vitu anatoa wapi.


“Ukiwa unaishi jirani na chuo ndiyo utaelewa ninachokisema,  tunaona magari ya kifahari yanavyopishana kuwafuata mabinti. Kiukweli inasikitisha kwa sababu uwekezaji mkubwa unafanyika kwa ajili yao ili Taifa lipate wasomi,  lakini sidhani kama wao wanaliona hilo. Kwa yanayofanyika mtaani sidhani hata kama hayo masomo wanayazingatia ipasavyo,”anasema Rhoda.

Kwa upande wake,  Hassan Lazio ambaye ni dalali na mkazi wa Mwenge,  anasema wanafunzi wengi huanza vyuo wakiwa vizuri lakini vishawishi na makundi huwafanya kubadili mienendo yao.

“Unakuta mwanafunzi amekuja mwaka wa kwanza hana mambo mengi, hawa tunawajua kuanzia kwenye mavazi yao hadi maisha kwa ujumla kama wanapanga basi watakuwa wawili au watatu lakini kadiri siku zinavyokwenda utaona mambo yanabadilika.

Kila mmoja anataka chumba chake, kwetu sisi ni tunafurahi maana ndiyo tunaingiza hela lakini ukiangalia uhalisia unajiuliza hivi huyu anapata wapi hela za kulipa kodi ya chumba, jiko na choo ndani halafu humo ndani anajaza vitu vya bei mbaya. Ukishaona hivyo hapo hata kusoma kwenyewe kunapungua anakuwa kama raia tu wa mtaani,” anasema Lazio na kuongeza:

“Hapo sasa ndiyo zinaanza anasa kila toleo la simu linapotoka analo, sasa hawa dada zetu ndiyo usiseme mavazi na nywele za bei mbaya kwahiyo ili haya mambo yaendelee kuwepo,  ni lazima atafute wa kumuweka mjini hapo anaweza kuwa mmoja au zaidi, tunayashuhudia sana huku,”.

Hoja hii iliwahi pia kutolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM ) Mwanaid Majaar akibainisha kuwa baraza  linafahamu na linatambua madhara mbalimbali yanayosababishwa na uzembe wa wanafunzi kwa kutotimiza wajibu wao ipasavyo.

Anasema hayo ni matokeo ya wanafunzi wenyewe kushindwa kujisimamia wenyewe kikamilifu huku wazazi nao wakiwa wameacha kuwajibika kwenye malezi wakiamini kwa vijana kufika vyuoni tayari wanaweza kujisimamia.

Kutokana na hilo Mwanaidi anawasisitiza wazazi na walezi kusimamia misingi bora ya malezi kwa watoto hasa katika kipindi hiki cha utandawazi kwani kinyume na hapo tutakuwa tutakuwa tunatengeneza kizazi tegemezi kisicho na uwajibikaji.

“Ninaisihi pia jamii na taasisi mbalimbali zikiwemo za kidini, kurudi kwenye misingi bora ya malezi  kwa kuangalia suala hili kwa jicho la kipekee ili kulinusuru taifa letu la kesho na madhara yanayotokana na kizazi kisichowajibika,”.

Akizungumzia hilo mhadhiri wa chuo kikuu kimojawapo nchini ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini  anasema  kumekuwa na ongezeko wa mienendo isiyofaa ya wanafunzi wa sasa wa vyuo vikuu, ambayo ni kinyume na uhitaji wa taifa wa kuwa na kizazi chenye kuleta ufumbuzi zinazojitokeza kwenye jamii.


"Kuhitimu chuo kikuu ni jambo moja, lakini aina ya nguvu kazi inayoingia kwenye soko la ajira ni changamoto nyingine tunayoiona. Kuna haja ya kuanza kuwapa mwongozo hawa watoto tangu wakiwa huko chini  kabla ya kufika vyuoni, wajitambue na kujua wanatakiwa kuwajibika ipasavyo ili tuzalishe wahitimu wenye tija kwa taifa.

"Kuna wanafunzi tunawaona siku za mitihani, siku nyingine hawajishughulishi na wala hawataki usumbufu. Wanajiona wameshakuwa watu wazima wanaweza kufanya chochote, haya ni mawazo mabaya hususani katika kipindi hiki ambacho dunia imebadilika,”anasema mhadhiri huyo.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Anna Henga amesema licha ya kuwa sheria inamtambua mtu mwenye umri zaidi ya miaka 18 ni mtu mzima hapaswi kufanya mambo yasiyofaa kwa sababu ya kigezo cha umri.


“Wengi waliopo kwenye vyuo vikuu ni watu wazima kwa sababu kisheria mtoto ni yule mwenye umri chini ya miaka 18, lakini utu uzima huu haukupi ruhusa ya kufanya mambo yasiyofaa. Umeenda kusoma basi kafuate kilichokupeleka kwa sababu tunawategemea wasomi katika ujenzi wa Taifa, sasa kama tutakuwa na wasomi wa ovyo sijui tutajenga taifa la aina gani?” anahoji.

Wasemavyo wanafunzi wenyewe

Miriam Robert ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anakiri kuwa wapo wanafunzi wa vyuo wanaoondesha maisha yao kwa njia zisizofaa ikiwa ni matokeo ya kuendekeza tamaa.

“Ni kweli kabisa watu wa aina hii tunao, amekuja kusoma lakini anataka maisha ya kifahari, awe na simu ya bei mbaya, asuke nywele kali na wapo hadi wanaoendesha magari lakini ukifuatilia hana kazi wala biashara.

“Sasa kama hana chanzo cha kumuingizia kipato na anataka maisha mazuri ndiyo wanapokuja masponsa, tamaa inawaponza wasichana wengi chuoni, wanajikuta wakitumia muda mwingi kwenye mambo mengine na kusahau kilichowaleta,”.

Naye Verdiana anasema wakati mwingine mwenendo huo unasababishwa na hali ngumu ya maisha hasa kwa baadhi ya wanafunzi ambao hawana mikopo na wanatoka kwenye familia duni.

“Sio wote walioko vyuoni wana mikopo au familia zao zinaweza kuwapatia mahitaji yote muhimu, sasa ikitokea hivi halafu akawa na makundi yasiyofaa ni rahisi kushawishika na kufanya mambo ya hovyo.

“Halafu hili linaonekana kwa wasichana pekee kwa sababu tumeona hao waliopigana na wengi huwa wanazungumzia zaidi vijana  wa kike lakini ukweli ni kwamba hali ni mbaya hata kwa vijana wa kiume tena hawa ndiyo wengi siku hizi,” anasema na kuongeza

“Haya mambo ya kutaka kumiliki simu za gharama, mavazi ya kisasa, kwenda kwenye starehe kila siku na hauna kazi tunashuhudia kaka zetu wakifanya mambo ya hovyo na hili suala lisipowekewa mkazo hali itakuwa mbaya zaidi,”

Wakati hao wakieleza hivyo Leila Maganga anasema ni dhana potofu kuamini mabinti wote wa vyuoni wana maisha ya hovyo akieleza kuwa wapo ambao wanajua wamefuata nini na wanasimamia misingi ya malezi waliyopewa.

“Nafikiri hao wachache wasiharibu taswira nzima ya wasichana waliopo vyuoni, ni kweli wapo ambao wana mfumo mbaya wa maisha na hiyo huenda ni kutokana na malezi, hali ya uchumi na tamaa. Binafsi naamini kuna kundi kubwa la wasichana wanaofika vyuoni na kuishi vile inavyompasa mwanafunzi na wanajua kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo bila kujiweka hatarini,”anasema Leila.


Mwanasaikolojia

Akizungumzia maisha ya wasichana vyuoni mwanasaikolojia Lindsley Shayo anasema wengi huangukia katika mambo yasiyofaa kwa kufuata mkumbo na tamaa za kupata mafanikio yanayoonekana kwa haraka.

Kwenye saikolojia kuna kitu kinaitwa mob psychology,hii ni ile hali unakuta watu wa rika moja wana tabia zinazofanana, hata kama wametoka kwenye historia tofauti lakini kukaa kwao pamoja kunafanya waigane tabia na mienendo.

Sasa kwa upande wa wanafunzi vyuoni kuna namna wanajaribu kuishi maisha sawa, hii inafanya hata wale wenye mienendo tofauti kushawishika kuwa kama wenzao. Ndio utakuta mtu alikuwa hana tabia ya kwenda disco lakini kwa sababu wenzake wanaenda na yeye anajifunza hadi anazoea kwenda,”

Anasema kwa mtiririko huo wapo ambao wanaweza kumudu maisha wanayotaka lakini wengine hawawezi ndipo wanalazimika kuingia kwenye mahusiano ili kupata fedha zitakazowawezesha kukidhi maisha wanayotaka.