Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Unyanyasaji, rushwa ya ngono kitanzi kwa wanasoka wanawake

Dar es Salaam. Unyanyasaji wa kingono, kipato duni, kazi zinazokinzana na maadili ya mpira wa miguu ni moja ya mizigo wanayobeba wanasoka wengi wanawake nchini, utafiti uliofanywa na Mwananchi hivi karibuni umebaini.

Utafiti huo uliowahusisha wachezaji 15 wa soka la wanawake, makocha wanne na viongozi wa watano, umebaini kuwa licha ya kukithiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa kingono ili kupata nafasi ya kucheza, wengi wao wamekuwa wakisajiliwa kwa kiwango kidogo mno cha fedha cha hadi Sh30,000 au wakati mwingine kwa kupigiwa simu tu lakini pia wengine wanafanya kazi za uhudumu wa baa, nyumba za wageni na kazi za ndani ili kujipatia kipato.


RUSHWA YA NGONO

Wachezaji tisa kati ya 15 waliohojiwa walisema kwamba wamekumbana na vitendo vya unyanyasaji wa kingono kwa njia moja au nyingine hususan katika kupata nafasi nafasi ya kucheza. Mmoja wa wachezaji ambaye hakutaka jina lake liandikwe anasema ili kupata nafasi katika kikosi cha kwanza, wakati mwingine kigezo cha uwezo uwanjani hakiwezi kuwa sababu, bali ‘ukaribu wako na kocha.’

“Nikisema ukaribu na kocha nadhani naeleweka, kwa sababu tunafundishwa na makocha wa kiume baadhi wamekuwa wakitutumia kimwili ili kutuhakikishia nafasi. Mchezaji anataka kutengeneza CV nzuri ya kutafuta nafasi ya kucheza soka la kulipwa hapo kuna mawili kutumika kimwili au kutoa hongo ya fedha ili apatiwe nafasi ya kucheza,” anadai mchezaji huyo.

“Wapo baadhi (ya makocha) wanatoka na wachezaji tena zaidi ya mmoja. Yaani kwenye timu mmoja unakuta anatoka na wachezaji wawili na kuibua chuki.”

Mchezaji huyo anasema tatizo hilo haliishii kwa makocha pekee, “pia wachezaji wenyewe kwa wenyewe wanaweza kuwa na mahusiano wa kimapenzi na pale kocha anapoingia katika mapenzi na mmojawapo, basi vita haiwezi kuwa ya kawaida. Mchezaji anaweza akacheza chini ya kiwango kwa lengo la kumharibia kocha, kwa vile tu anatoka na mpenzi wake.”

Kauli hiyo inaungwa mkono na mwanasoka wa Zanzibar, Fatma Hashim ‘Faa’ ambaye anasema, “wakati mwingine unakuta mchezaji anakutumia meseji za kukutongoza, unajiuliza anatania au anamaanisha? Akiwa na uso mkavu anakwambia kuwa anamaanisha kuwa ana upendo na wewe.

“Unajua sisi ni wachezaji, huwezi kumchukia mtu tunapendana sana, hivyo hutokea mmoja anakuomba namba unajua anaomba tu kwa ajili ya mawasiliano ya kirafiki, lakini ukiwa upo zako nyumbani unakutana na ujumbe wa kutongozwa. Hapo ndio akili inakuwa kichwani mwako kujua namna ya kumjibu kwa upande wangu nimekutana na tatizo hili,” anasema Faa.

Mshambuliaji wa zamani wa timu ya New Generation ya Zanzibar Riziki Abubakar Islah anasema aliamua kustaafu soka na kugeukia ukocha kutokana na unyanyasaji wa kingono.

“Hiyo imenifanya nistaafu mapema soka kwani unakutana na viongozi na makocha hawathamini uwezo wako wanataka wakutumie ndio upate nafasi, hicho kitu sikukikubali.”

Riziki anasema, “Ni changamoto mabinti kufundishwa na makocha wa kiume, kwa sababu wanaingia katika vishawishi kwa kulazimishwa mapenzi na kwa vile nao wanataka kuonekana na wanapenda kucheza unakuta wanajiachia na kocha. Kwenye kikosi kimoja anaweza kutoka na wachezaji zaidi ya watatu, hii inachangia kudidimiza kipaji,” anasema Riziki.

Kocha huyo anasema vitendo hivyo vya baadhi ya makocha vinachangia kupotea kwa vipaji vingi. Kwani baadhi ya wachezaji wanaoingia kwenye mtego huo huvimba vichwa na kujiona wanajua zaidi.

Mtazamo wa Riziki unafanana na ule wa Kocha wa Temeke Sisters, Fatuma Gotagota ambaye anasema amekuwa akipokea malalamiko ya baadhi ya wachezaji kutoka nje ya timu yake ambao wameamua kuhama timu zao kukimbia unyanyasaji wa kingono.

“Sijawahi kukutana na hali hiyo kwa sababu mimi ni kocha wa kike. Kwenye timu yangu wachezaji wangu hawajawahi kunipa malalamiko ila nje ya Temeke Siters kuna wachezaji wamewahi kunifuata na kuniambia kuwa wamekuwa wakisumbuliwa na walimu wao wa kiume kuwataka kingono,” anasema Fatuma na kuongeza, “Mchezaji ambaye amekuwa akimkataa mwalimu basi kwake ni ngumu kupata nafasi ya kucheza kitu ambacho kinawafanya baadhi waachane na mpira na wengine kuhama kutoka timu moja kwenda nyingine.”

Lakini mchezaji wa zamani wa Tanzanite, Misky Siraji ana mtazamo tofauti kidogo, “Suala la kutongozwa lipo sana kwasababu tunakutana jinsia mbili tofauti sio rahisi kukubali au mtu kutoka kuzungumza mbele ya jamii kwa sababu ni hulka ya mtu kuamua kukubali au kukataa sio suala la kulazimishana lakini kuna wengine wanajikuta wanaingia kwenye vishawishi na baada ya hapo wanashindwa kufikia malengo;

‘’Nimeshakutana nalo mara nyingi lakini haikuniharibu kisaikolojia kwa sababu nilikuwa naamini katika kipaji changu uwezo wangu ulikuwa unanipa nafasi ya kucheza licha ya kumkataa (kocha) lakini hakuwahi kunikalisha benchi kwani nilikuwa nacheza kutokana na uwezo mkubwa niliokuwa nao. Sijisifii, nilikuwa nacheza kila timu ikipata mechi ya kucheza nayo.”

“Sio kweli kwamba wachezaji ambao hawapati nafasi au wanaopata nafasi ni kwa sababu ya kupendwa na makocha hakuna kocha ambaye anaweza kumpanga mchezaji asiye na uwezo eti kwa kuwa tu amemtaka kimwili na kama kuna wachezaji wanaamini hivyo basi hawana uwezo.”

Misky anasema mbali na makocha pia viongozi wamekuwa wakiwasumbua wachezaji kutokana na mionekano yao. Wamekuwa wakiwapa baadhi ya wachezaji nauli tofauti na wenzao wengine lakini anasisitiza kuwa kukaa benchi kwa upande wake hakukuwahi kusababishwa na kumkataa kocha.

‘’Sio makocha tu ambao wanaotuingiza kwenye changamoto ya rushwa ya ngono hadi viongozi na mashabiki pia wanatutaka kingono hivyo akili binafsi ndizo zinasababisha wengine kuingia huko,” anasema.

Mchezaji wa zamani wa Dyoc, Rehema Mtimbuka anaungana na Misky akisema haya yeye hajawahi kusumbuliwa kwa sababu aliingia kwenye soka akiwa tayari na mtoto hivyo alikuwa anacheza kwa malengo ili kuendesha maisha yake.

“Kuna kocha alikuwa ananipenda kipindi hicho nakumbuka tulikuwa tukicheza mechi tunapewa nauli. Huyo kocha akifutwa na wachezaji wengine mimi sipo jibu lake lilikuwa ni hakuna nauli leo lakini nikienda mimi alikuwa anatoa na ili kuepusha maneno alikuwa ananiambia niwagawie na wenzangu;

“Nilikuwa namtumia kwa manufaa yangu nikiwa nimeishiwa viatu vya mazoezi namwambia bila kusita ananinunulia lakini ukifika muda wa kunitaka kimwili nilikuwa na sababu zangu ambazo zilikuwa hazimpi nafasi ya kunitumia. Nilikuwa nimekomaa kiakili baada ya kuzaa nikiwa nyumbani hivyo ilikuwa ni ngumu lakini kwa wachezaji mbao ndio kwanza wanaanza ni rahisi kushawishika,” anasema.

Kocha Msaidizi wa Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, Hilda Masanche anasema, “mchezaji wa kike kutongozwa ni kawaida kwa sababu ni mtoto wa kike lakini suala ni mapokeo. Kwa mfano, mimi nikiwa Sayari nakumbuka nilikuwa nasoma chuo nilikuwa nakutana na meseji nyingi za kutakwa kimapenzi lakini huo muda nilikuwa sina na sio makocha tu, hadi viongozi wa mpira pia walikuwa na usumbufu huo. Hilo suala sina uhakika kama limeisha, siwezi kulizungumzia sana kwa sababu mimi sifundishi soka la wanawake katika klabu, ninapata wakati wa kukaa nao nikiwa timu ya taifa.”

Mchezaji wa zamani wa Evergreeen Queens ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema amepitia changamoto nyingi za kutakiwa kimapenzi lakini hilo halikumuondoa kwenye soka hadi hapo alipoamua kuachana na mchezo huo kutokana na changamoto za fedha.

“Kutongozwa ni suala ambalo lipo na linafanywa sana na makocha hii ni kutokana na kufanya kazi na jinsia tofauti hivyo kila mmoja anatakiwa kuzingatia nini anatakiwa afanye ili kufikia malengo,” anasema.

Kuhusu upendeleo anasema, “hakuna kocha ambaye anaweza kumuacha mchezaji mwenye uwezo benchi kwa chuki zake za kukataliwa na ikitokea hivyo lazima viongozi na wadau watahoji pia kocha anajishushia CV kwani timu yake inaweza kukosa matokeo huku wachezaji wenye uwezo kawaweka benchi.”

“Mimi niliacha mpira baada ya kuona hakuna ninachonufaika nacho, nacheza siingizi fedha familia ilinisusa wakaniambia nikiumia natakiwa kujitibia mwenyewe nikaona sina sababu ya kutengwa kwa kitu ambacho hakinipi faida.”

Katibu Mkuu wa JKT Queens, Beno Duncan anasema hawajawahi kukutana na kesi ya namna hiyo. “Tunawalea vizuri kuanzia kielimu na kimichezo. Changamoto ya kushawishiwa kingono kwa upande wa wachezaji wetu sio rahisi. Tumekuwa tukiwajenga na kuwapa muda mwingi wa kuwaelimisha.”

Kauli kama hiyo inatolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Soka la Wanawake Zanzibar, Khatma Khamis ambaye anasema hajawahi kupokea malalamiko kama hayo, “Ni taarifa ambayo naisikia kutoka kwako. Haijawahi kufika katika ofisi yangu kama ipo basi inaishia huko bila kutufikia tukaifanyia uchunguzi ili kuhakikisha watoto wa kike wanafanya majukumu yao bila ya kukutana na vikwazo kama hivyo.”


NINI KIFANYIKE

Ili kukabiliana na changamoto hizo Kocha Fatuma anashauri kwamba ni vyema timu kuwa na mchanganyiko wa makocha. Kama mkuu ni wa kiume basi msaidizi awe wa kike ili kupata sehemu ya kukimbilia kuzungumzia changamoto zao na ikiwezekana makocha wanawake wazalishwe kwa wingi ili waweze kuzisimamia timu hizo.

Lakini baadhi ya malalamiko yanatiliwa shaka kama Kocha wa zamani wa Simba Queens, Juma Mgosi anavyosema kwamba kwa miaka mitatu aliyofundisha soka la wanawake alikuwa akikabiliwa na tuhuma hizo kutoka kwa wachezaji waliokuwa wanakosa nafasi na ambao alikuwa anawakata kupisha usajili mpya. Kisingizio chao kikubwa kilikuwa wameachwa au hawapati nafasi kwa sababu wamemkataa.

“Mpira wa wanawake bado hujakua, tunapambna kuukuza sasa changamoto iliyopo kuanzia wachezaji na mashabiki wamekuwa na fikra potofu mchezaji humpangi, yeye akiulizwa kwa nini hachezi majibu yake hapendwi ndio maana anakosa nafasi lakini hataki kukubali kuwa amezidiwa uwezo na anayecheza.

“Pia mashabiki wamekuwa na fikra potofu wanakuja uwanjani wakiangalia mechi mbili wakamuona mchezaji kafanya vizuri na baada ya muda hawajamuona wanaanza mawazo potofu kuwa hapangwi kuna kitu kimetokea baina yake na kocha kitu ambacho sio kweli kwa sababu sisi ndio tunakaa muda mwingi na wachezaji tunafahamu uwezo wao,” anasema.

Mgosi ambaye alikuwa mshambuliaji wa zamani wa Simba anasema wachezaji wanatakiwa kukubali uwezo wa wenzao wanaowazidi na kujitambua ili waweze kufikia malengo. Anawataka pia kujifunza kutoka kwa anayepata nafasi badala ya kuamini kuwa hawapendwi ndio maana wananyimwa nafasi. Anasema hakuna kocha anayetamani mafanikio anayeweza kuthubutu kumuacha mchezaji mzuri bora nje na kumpang ambaye hayupo fiti.

“Timu inasajili wachezaji 30 kati ya hao, 11 wanaanza na saba wanakaa benchi mimi kama kocha nitawatongoza wangapi na kuwacha hao 12? Wanatakiwa kukubali kuwa wanazidiana uwezo wanatuharibia japo siwezi kuwasemea makocha wote kama wapo, basi pia hawawezi kufanikiwa kwani kumtongoza mchezaji wa kike ambaye ni mvivu wa mazoezi anaweza kukuharibia kazi na utakuwa umekiuka maadili ya kazi.

Hata hivyo, Mgosi anabainisha: “Unajua katika majukumu ya wanawake na wanaume ni lazima kutokee kutamaniana, hivyo mchezaji ili kukwepa changamoto hiyo sambamba na kocha ni kila mmoja kutimiza wajibu wake bila kuingiza mambo ambayo hayapo kwenye maadili. Vyuoni, makazini mambo ya kutongozana pia yapo sio michezoni tu. Hadi kwa upande wa wanaume yapo madai kwamba mchezaji wa kiume ili acheze ni lazima amhonge kocha, lakini si kweli. Nidhamu na kujituma ndiyo siri pekee ya kucheza.”

Kocha aliyewahi kuzifundisha Simba na Yanga, Sebastian Nkoma anasema suala la kocha kuwa na matamanio na mchezaji wake ni tabia ya mtu na inategemea na umri pia.

“Mfano kwa makocha vijana wanakutan na wachezaji wa rika lao, sio rahisi suala hilo lisitokee. Sasa hapo ni uamuzi wa mchezaji mwenyewe kukubali au kukataa na kama wanakutana na hizo changamoto wanatakiwa kuripoti kwa viongozi wao.

“Mtoto wa kike mwenye mwenyewe anatakiwa kujichunga ili aweze kufikia malengo yake bila kutafuta sababu za kutongozwa na makocha, anatakiwa kupambana uwanjani ili aonekane huko na sio kuulizwa kwa nini hachezi ndipo atoe visingizio visivyokuwa na ukweli wala maana yeyote.”

 

MBINU YA MBADALA

Riziki anasema katika kukabiliana na vitendo hivyo, baadhi ya wachezaji hubadili muonekano na kujifanya wanaume ili kujilinda kuingia katika vishawishi.

“Wachezaji wengi wamekuwa wakilaumiwa kuwa wanajibadilisha kimuonekano wakijiweka kama wanaume. Sina hakika kama kuna watu wameuliza sababu inayowafanya wawe hivyo. Mie nafahamu kuwa kuna wanaofanya hivyo ili kujilinda. Hakuna kocha au kiongozi anayeweza kumfuata na kumrubuni kutokana na namna anavyojiweka,” anasema Riziki.

Hata hivyo, mtazamo wa Riziki unapingwa vikali na beki wa Fountain, Gate Princess Agness Pallangyo ambaye anasema, “tumekuwa tukibadilika mwonekano hadi maumbile yetu kutokana na mazoezi tunayoyafanya japo kuna wengine ni hulka zao wenyewe kuamua kuonekana wa kiume, inatakiwa kuzingatiwa kuwa sio wote tunajifanyisha kuwa wanaume.

“Mazoezi tunayoyafanya muda mwingine tunajikuta tunabadili mizunguko yetu ya hedhi wakati mwingine hatuingii huenda ndio sababu ya wengine kujiona wanaume lakini mimi kwa upande wangu nafurahi kuwa binti na ndoto yangu ni kuja kuwa mama na mke wa mtu,” anasema.

Wakati Agness akisema mazoezi ndicho chanzo cha kubadilika kwa mwonekano, Rukia Juma wa timu ya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), anasema ni utashi wa wachezaji wenyewe kuamua kuingia kwenye muonekano huo na kwamba mazoezi hayawezi kuwa sababu ya kuwa na mwonekano wa kiume.

“Mimi ni mchezaji niliyepita JKU, nimebebeshwa sana zege kwenye ujenzi wa majengo ya Serikali nimefanyishwa mazoezi magumu, lakini sina huo muonekano na sasa ni mchezaji ninayefanya hayo mazoezi na naingia kwenye siku zangu kama kawaida, kilichobadilika ni maumivu makali niliyokuwa nayasikia sasa hakuna.

“Hivyo hali ya watoto wa kike kujiweka kwenye muonekano wa kiume ni matakwa yao wenyewe hadi huku Zanzibar wapo na ongezeko limekuwa kubwa kila msimu wanaongezeka ninaamini wanaiga tu sina uhakika kama mazoezi yanaweza kuwa chanzo mbona mimi sipo hivyo.” anasema.

Lakini Rukia Mohamed, anayecheza timu ya New Generation anasema hali hiyo ya kujibadili mwonekano inazidi kuongezeka na kuharibu vizazi kwani wachezaji sasa wanaona kuwa ni fasheni.

“Hali hii ikikemewa wanaweza kubadilika na kuachana na tabia ambazo sio nzuri.  Ni kumkufuru Muumba, wamezaliwa wanawake wanatakiwa kuishi kwa kujiweka kwenye muonekano wa uanamke.” anasema mchezaji huyo.

“Pia makocha wamekuwa wakiwafanyisha mazoezi magumu wakiamini soka ni mpira wa kiume na kuwafanya wakomae na wengine kujiona kama madume, ila ukweli tunawaona wachezaji Ulaya wanaocheza soka la wanawake lakini wapo kwenye muonekano mzuri kwa vile wanafanyishwa mazoezi ya kawaida.

“Tofauti na huku kwetu, wachezaji wanafanyishwa mazoezi magumu kama wanaume na mwishowe kuwafanya wachezaji wanakuwa na sura ngumu, kusema kweli wanawakosea wanatakiwa kuwafanyisha kwa uwezo wao kama mabinti,” anasema.

Mgosi anasema suala la mabadiliko ya muonekano kwa wachezji wa kike inasababishwa na mambo mawili; wanawake wenyewe huamini kuwa ili uwe mchezaji wa mpira wa miguu lazima uwe na muonekno wa kiume na pili ni makocha kushindwa kutambua ni mazoezi gani wanatakiwa kuwafanyisha wanawake.

"Nimefundisha soka la wanawake miaka mitatu, lakini jukumu kubwa lililonitesa ni pamoja na kuwaaminisha kuwa mionekano ya kiume si uchezaji kinachotakiwa ni mazoezi. Unakutana na mchezaji hajui kama anatakiwa kuvaa vitenge au magauni anavaa nguo za kiume tu hivyo napambana kumwaminisha kuwa mavazi siyo kucheza. Hata kocha wa timu ya taifa pia alikuwa anatoa elimu hiyo lengo lilikuwa ni kuwabadilisha.”

Mgosi anasema makocha wengi wanaofundisha soka la wanawake hawana uelewa wa aina ya mazoezi ambayo wanatakiwa kuwapa wachezaji wa kike.

"Nawapongeza viongozi w TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kuwaongezea elimu makocha na sasa kuna ongezeko la wanaostahili kufundisha ligi ya wanawake,” anasema

Kuhusu mazoezi, Nkoma ameungana na makocha wengine akisema mazoezi magumu yanachangia kubadili muonekano wa wachezaji wanawake.

"Mchezaji akiwa na programu maalumu ya mazoezi mepesi hawezi kukutana na changmoto kama hiyo. Mfano mazoezi ya 'Gym' kwa wanawake kuna aina maalumu ili kutafuta pumzi akizidisha anaingia kwenye mabadiliko. Mazoezi ya 'Gym' yanasaidia kuongeza nguvu lakini haina maana kwamba wakienda huko wakafanye yote ambayo yanafanywa na wanaume. Wao ni tofauti,” anasema Nkoma.

Mkufunzi wa mazoezi katika 'Gym' ya Kevoo iliyopo Tabata Kimanga, Dar es Salaam Calvin Mawalla anasema mazoezi magumu ni chanzo cha kubadili muonekano na kwamba kuna aina ya mazoezi wakifanyishwa ni rahisi kubadilika.

''Gym kuna mazoezi ya aina nyingi lakini mengi ni bora kwa wanaume. Kwa miaka ya sasa wanawake pia wamekuwa wakijihusisha na mazoezi ili kutengeneza mionekano mizuri ya miili yao lakini kuna baadhi wanafanya kwa ajili ya kuongeza nguvu kutokana na kazi yao ya soka. Kuna umuhimu wa kutambua aina ya mazoezi wanayotakiwa kufanya ili kukwepa changamoto ya mabadiliko ya kimaumbile.

"Kuna wachezaji wamekuwa na mionekano ya kiume, hii ni kutokana na mazoezi magumu ambayo wamekuwa wakifanya tofauti na aina ya mazoezi yanayotakiwa. Kwa mfano ‘push up’ si mazoezi sahihi kwao yapo mengi, lakini ushauri ni kufuata maelekezo na sio kuamini kila mazoezi ya Gym yanaongeza nguvu,” anasema.

Mkufunzi wa mazoezi katika 'Gym' ya JSP Maeketing Link Fitness iliyopo Mbezi Beach, Dar es Salaam, Emmanuel Mazare anasema mazoezi wanayotoa yanachangia kuwabadilisha wachezaji kuwa imara.

''Tayari umeshasema ni wachezaji sio rahisi kuwafanyisha mazoezi mepesi hawawezi kuwa timamu lakini mazoezi yao hayawezi kuwa sawa na wachezaji wa kiume, hii ni kutokana na maumbile pia kuwa tofauti. Mwanamume amezaliwa kuwa mgumu na mwanamke ni laini hivyo kunakuwa na utofauti kidogo lakini wao pia ni lazima wawe na mabadiliko.

''Moja ya mabadiliko ni mazoezi ya miguu. Ili mchezaji awe fiti anaanza kutafuta nguvu za miguu, mazoezi ambayo hadi wanaume wanafanya utofuti ni muda wanaotumia.”

Daktari wa Kagera Sugar, Abel Shindika pia anasema mazoezi magumu kwa wanawake ni changamoto kwa sababu yanaweza kubadili tarehe zao za hedhi kwa kuwahi au kuchelewa.

"Mazoezi magumu yana madhara kwa wanawake. Mchezaji anaweza kuingia kwenye siku zake akiwa katikati ya mchezo na kumsababishia kushindwa kuendelea wakati huohuo anaweza asiingie kabisa," anasema.

Kauli hiyo inaungwa mkono na daktari wa Simba Queens, Lanina Hasadi ambaye anasema mazoezi magumu yanaweza kukatisha hedhi kwa wachezaji wa kike.


KUHAMA KWA SIMU MOJA TU, MSIMU MZIMA SH30,000

Kama nilivyodokeza awali, wanasoka wengi wanawake wanakabiliana na changamoto nyingi nje ya uwanja, kuanzia usajili, kazi na mikataba mambo ambayo yanawafanya washindwe kuupa mchezo huu kipaumbele.

Kutokana na hali hiyo, wapo walioamua kukomaa kwa maana ya kujitafutia shughuli nyingine za kufanya huku wakisakata kabumbu lakini kazi wanazofanya haziendani na miiko ya mchezo huo.

Kutokana na usajili kufanyika bila malipo, Rukia Mohammed anasema ni rahisi sana kwa mchezaji kuhama kutoka timu moja kwenda nyingine, “mimi ni mfano wa wachezaji ambao wamehama kutoko Green Queens na sasa nacheza New Generation.

Anasimulia, “nilisajiliwa misimu misimu miwili Green Queens, lakini nimeitumikia msimu mmoja na msimu ulioisha nimecheza New Generation. Sijapewa fedha yoyote ya usajili nilitaka kubadili mazingira tu na kujaribu changamoto nyingine nje ya timu iliyonikuza.

“Nafikiri viongozi wa New Generation ndio waliomalizana na Shirikisho la Soka (ZFF), kwani baada ya kunipigia simu kuwa wanataka niwachezee msimu ujao nilichokifanya ni kumuomba kocha kuwa naenda kujaribu changamoto mpya katika timu nyingine na nikahamia upande wa pili na tumetwaa ubingwa msimu huu,” anasema.

Lakini cha kushangaza ni kwamba anasema hakujua kama amechukuliwa bure, alidhani uongozi wa New Generation ungefanya mawasiliano na timu iliyomkuza lakini ilikuwa tofauti.

Kama unashangaa jinsi Rukia alivyohama bure kuna hili la wachezaji kuambulia Sh30,000 baada ya kuvuja jasho kwa msimu mzima. Tena hao ni wale ambao wamefikia kilele cha mafanikio sikuambii walioshika nafasi za chini.

Msimu uliopita ambao Worrious ilitwaa ubingwa inaelezwa kuwa ilipata kiasi cha Sh1 milioni moja na kiongozi mmoja wa timu hiyo alisema waliamua kuzigawa fedha hizo kwa wachezaji na hivyo kila mmoja kuambulia Sh30,000.

“Huwezi kuamini gharama tulizotumia msimu mzima hazifiki hata robo na fedha tuliyopewa. Kwa kuwa hakuna tunachowalipa wachezaji, tuliamua kugawa kiasi hicho kidogo kilichopatikana msimu ujao tutaumiza kichwa namna ya kuandaa kikosi.” anasema kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake liweke wazi.


KAZI ZAO SASA…

Ukiwauliza wachezaji wengi wa soka la wanaume ambao wanacheza katika madaraja ya juu hasa Tanzania Bara, watakuambia kuwa mpira ndio kazi yao na kama kuna shughuli nyingine ya kuwaingizia kipato hiyo ni ya ziada tu.

Lakini kwa soka la wanawake hususan visiwani Zanzibar, mambo ni tofauti kabisa.

Mchezaji wa Green Queens ya visiwani humo, Annastazia Desmon anasema soka la wanawake Zanzibar ni la kujitolea na kama mwanasoka hana kitu kingine cha kufanya anaweza kujikuta anashindwa hata kufanya mazoezi.


Imeandikwa kwa kushirikiana na Bill & Melinda Gates.