Wadau watoa mapendekezo Sheria ya kupinga na kuzuia rushwa

Wanamtandao wa kupinga na kupambana na rushwa ya ngono nchini wakiongozwa na mwenyekiti wake Profesa Ruth Meena(katikati) wakati wakitoa tamko lao jana jijini Dar es Salaam
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiwa kwenye mchakato wa kuifanyia maboresho sheria ya kupambana na kuzuia rushwa, wanamtandao wa kupinga na kupambana na rushwa ya ngono nchini wametaka kuondolewa kwa kipengele cha 25 kifungu cha pili kinachomhukumu mtu aliyetendewa udhalilishaji huo kwa kigezo cha kushawishi.
Akitoa tamko la wanamtandao huo, mwenyekiti wake, Profesa Ruth Meena amesema kipengele hicho kitaendelea kuwalinda watu wanaofanya vitendo hivyo na kuwaathiri zaidi wanawake ambao ndio waathirika wakubwa.
Profesa Ruth amesema kipengele hicho kitapelekea kunyamazisha sauti za wahanga ambao wataogopa kutoa ushahidi kwa kuogopa kuadhibiwa na kusabaisha dhidi ya vitendo vya rushwa ya ngono na kusababisha wanawake kuendelea kuathirika bila hatua kuchukuliwa kwa wahusika.
“Tunaviomba vyombo vyote vinavyohusika na mabadiliko ya sheria ikiwemo Bunge kutokubaliana na pendelezo la kubadilisha kipengele hicho kwani kitapelekea uwepo wa sheria itakayo endeleza utumiaji mbaya wa mamlaka,"amesema.
Kwa upande wake Msafiri Mwajuma ambaye ni mjumbe wa mtandao huo ametoa wito kwa wanaume nao kuungana pamoja na wanawake kupinga kupitishwa kwa kipengele hicho kwani kinaweza kupelekea kurudi nyuma kwa mapambano dhidi ya rushwa ya ngono.