Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasira: Umoja wa Taifa si mali ya CCM bali ni kwa Watanzania wote

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira

Muktasari:

  • Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira amesema umoja wa Taifa si mali ya CCM bali ni wa Watanzania, huku akidokeza mabadiliko ya sheria ya uchaguzi yaliyofanyika kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.

Mwanza. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema umoja uliopo nchini si mali ya chama hicho pekee, bali ni wa Watanzania wote, hivyo anayejaribu kuuvuruga anapaswa kutafuta shughuli nyingine kwa kuwa hatavumiliwa.

Akizungumza wakati wa ziara yake mkoani Mwanza leo Jumapili Juni 22, 2025 kukagua uhai wa CCM na kuzungumza na viongozi wa chama hicho pamoja na wananchi, Wasira amesisitiza kwamba ni lazima viongozi wa Wilaya ya Ukerewe washughulikie kero zinazolalamikiwa na wananchi ikiwamo ya upatikanaji wa matibabu bure kwa wazee.

Amesema hakuna sababu yoyote ya wazee kushindwa kupata huduma hizo.

Mkutano huo ni mwendelezo wa vikao vinavyofanywa na Wasira tangu Juni 10, 2025 alipoanza ziara mkoani Ruvuma, Geita na sasa Mwanza.

Kote huko anafanya kazi ya kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wanachama na wananchi sambamba na kuzitafutia ufumbuzi, na wakati huohuo akikinadi chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

“Duniani kuna mambo yasiyopaswa kuchezewa. Mojawapo ni tunu za Taifa letu ambazo ziliasisiwa na vyama vilivyopigania uhuru wa Taifa hili. CCM itahakikisha tunu hizo hazivurugwi na yeyote,” amesema Wasira.

Ameonya kuwa atakayeona kuuvunja umoja huo ni kazi, anapaswa kuachana nao na kufanya shughuli nyingine badala ya kutaka kuwavuruga Watanzania.

Amesema jukumu la CCM ni kulinda umoja, maendeleo na amani na pale penye viashiria vya uvunjifu wa amani, chama hicho hakitamvumilia mtu, kitachukua hatua.

Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao, Wasira amewataka wajumbe watakaoshiriki mchakato wa uchaguzi kutenda haki, akisisitiza kuwa CCM haiuzi nafasi za uongozi.

“Tunataka mtuchagulie watu wanaokubalika na wananchi. Atakayenunua nafasi mnaamini ataweza kuwatumikia wananchi?” amehoji.

Ameongeza kuwa, kupitia mabadiliko ya sheria za uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 na zile za Serikali za Mitaa zimefutwa na sasa kuna Sheria mpya ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.

Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, wakurugenzi ambao awali walilalamikiwa wamesitishwa kusimamia uchaguzi na jukumu hilo limekabidhiwa kwa wasimamizi watakaoteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Changamoto za wananchi
Viongozi wa CCM na wanachama wa Wilaya ya Ukerewe wameibua changamoto nne wakati wa kikao hicho, ikiwamo ya wazee kutopata matibabu bure.

Deogratius Misambu, akiwawakilisha wazee wenzake wa Ukerewe, amemuomba Wasira kushughulikia kero hiyo ya wazee kushindwa kupata matibabu bure, licha ya sera ya Afya ya 2007 kuelekeza huduma bure kwa wazee, wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Balozi wa CCM wa Tawi la Bogome naye ameiomba Serikali ijenge barabara kwa kiwango cha lami ili kumaliza kero ya vumbi wilayani Ukerewe.

Naye Mzee Festus Mayunga ameomba Serikali ifikirie kutoa mikopo nafuu kwa wanaume wazee, huku akisema kwa sasa wanufaika wa mikopo hiyo ni wanawake na vijana jambo linaloibua maswali mengi.

Majibu ya Wasira
akijibu maombi hayo,Wasira amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Emmanuel Sherembi kuhakikisha wazee wanapatiwa vitambulisho na huduma bora za matibabu bila malalamiko.

Akizungumzia ujenzi wa barabara, Wasira amesema Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), inashughulikia, huku suala la mikopo akiahidi kulifikisha sehemu husika kwa hatua zaidi ya ufumbuzi.