Prime
Wiki ya lala salama bungeni, mawaziri…

Muktasari:
- Juni 27, 2025, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan atalifunga Bunge la 12 ambalo lilizinduliwa Novemba 13, 2020 na Rais wa awamu ya tano, hayati Dk John Magufuli.
Dodoma. Safari ya miaka takriban mitano ya uhai wa Bunge la 12 unafikia tamati siku tano zijazo, huku ikishuhudiwa mawaziri wakiwa katika kibarua cha kupangua hoja zilizoibuliwa wakati wa mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2025/26.
Uhai wa Bunge hilo, lililozinduliwa Novemba 13, 2020 na Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, litahitimishwa Ijumaa ya Juni 27, 2025 kwa hotuba ya kulifunga itakayotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Bunge hili la 12 litahitimishwa likiwa na mambo ya kipekee, lilizinduliwa na Magufuli na linafungwa na Rais Samia.
Aidha, lilianza likiwa na Spika Job Ndugai na linahitimisha uhai wake likiongozwa na Dk Tulia Ackson.

Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 na Samia, aliyekuwa makamu wake, akaapishwa Machi 19, 2021 kuwa Rais. Dk Tulia alichaguliwa kuwa Spika baada ya Ndugai, Januari 6, 2022, kutangaza kujizulu.
Aidha, Rais Samia alipata wasaa wa kulihutubia Bunge Aprili 22, 2021.
Katika wiki ya mwisho ya uhai wa Bunge hilo, kuanzia kesho Jumatatu, Juni 23, 2025, mawaziri wa kisekta watapambana kuzijibu hoja zilizoibuliwa na wabunge wakati wa mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2025/26.
Mjadala huo ulioanza Juni 16, 2025 ulianza baada ya kuwasilishwa kwa mapendekezo ya bajeti kuu ya Serikali na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka huo.
Baada ya mawaziri wa kisekta kujibu hoja, itafuata zamu ya mawaziri waliowasilisha hoja zao Juni 12, 2025, ambao ni Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.
Hitimisho la bajeti kuu litahusisha wabunge mmoja mmoja kupiga kura za uamuzi kuhusu bajeti hiyo Juni 24, 2025, na kisha kufuata Muswada wa Sheria ya Fedha za Matumizi kwa mwaka 2025.
Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, Juni 25, 2025 kutakuwa na Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2025/26, ambao utajadiliwa kwa siku mbili, ukifuatiwa na hotuba ya Waziri Mkuu ya kuliahirisha Bunge Juni 26, 2025.
Kwa wiki nzima iliyopita, wabunge wachache walitumia nafasi hiyo kuwasilisha hoja, huku wengine wakijikita kueleza mafanikio ya miaka mitano na dhamira za kuwania tena ubunge.
Juni 20, 2025, akiahirisha kikao cha 50 cha Bunge, Mwenyekiti wa Bunge, Deo Mwanyika alisema mawaziri wa kisekta watapata nafasi ya kuchangia leo Jumatatu, Juni 23, 2025.
“Tunamatarajio kuwa watajiandaa vizuri kabla ya mtoa hoja hajafuatia,” alisema Mwanyika.
Hoja za wabunge
Kamati ya Bajeti ilipendekeza kuwepo adhabu kwa raia wa kigeni watakaokiuka kanuni za biashara, ikiwemo kufutiwa vibali vya kazi na visa.

Mwenyekiti Oran Njeza alisisitiza Serikali kushughulikia urejeshaji wa mapato kwa kwa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (Tawa), Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Hoja nyingine ni ile ya Mbunge wa Kilombero, Abubakar Asenga aliyetaka kodi ipunguzwe kwa vifaa vya ujenzi vya wananchi wa kawaida kama bati geji 30 na nondo chini ya mm16.
Naye mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Neema Lugangira alitaka likizo ya kodi kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu kwa miaka mitatu ili kuvutia walipa kodi wapya.
Kwa upande wake, mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage alishauri kuondoa kodi kwenye gesi asilia kwa kuwa ni injini ya uchumi.
Hoja nyingine ni ya mbunge wa Vwawa (CCM), Japhet Hasunga alitaka mpango mkakati wa kupunguza umaskini kwa kuwa asilimia 26 ya Watanzania bado ni maskini.
Malalamiko ya wabunge kutaka tozo za miamala ya kieletroniki kwenye benki na simu nazo yaliibuliwa wakitaka zipunguzwe kwa kuwa zinasababisha wengi kutotumia huduma hizo.
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Kilumbe Ng’enda alilalamikia tozo za miamala, akisema zinawafanya wananchi wasitumie benki.
Mbunge wa Biharamulo (CCM), Ezra Chewelesa alitaka ushuru wa asilimia 10 10 katika vichwa vya matrela vinavyoingizwa nchini kwani vitasababisha gharama za kusafirisha mizigo kupanda na hivyo kuwaumiza wananchi.
Kwenye mjadala huo pia kulikuwa na hoja ya kutaka gharama za upandikizaji wa mimba kushushwa, ili kuwawezesha watu wengi wasio na uwezo kunufaika na huduma hiyo.
Hoja hiyo iliibuliwa na mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Dk Thea Ntara aliyetaka gharama za upandikizaji wa mimba zishushwe na watu wa vijijini wawezeshwe kuachana na matumizi ya nyasi.
Wadau wazungumza
Mfanyabiashara maarufu jijini Dodoma, Peter Olomi alisema bajeti hiyo imewajali wafanyabiashara na hakuna sababu ya kuipinga:
“Ushuru wa hoteli umepungua kutoka asilimia 10hadi asimilimia 2, hii ni habari njema. Hakukuwa na ushindani mkubwa katika ku-defend kwa sababu ni bajeti ya mwisho ya uchaguzi,” alisema.
Amesema kwa ujumla, bajeti za kisekta zilizopita hazikuwa na ushindani mkubwa kati ya wabunge na mawaziri hadi kufikia kuondoa shilingi, kwa kuwa zilikuwa zimewajali wananchi, na kuwa ndivyo itakavyokuwa katika upitishaji wa bajeti kuu ya Serikali.
Olomi amesema bajeti inapowajali bodaboda, wakulima na wafanyabiashara, hakuna cha kupinga bali ni kuisindikiza ipite ili wanaoisimamia waitekeleze.
Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulia amesema katika mjadala wa bajeti, alipendekeza fedha ziongezwe kwenye huduma za simu kuchangia Bima ya Afya kwa Wote.
“Kwenye hili, siliungi mkono la kutoza Sh100 kwenye simu. Waache habari za mambo ya simu kwa sababu kwenye simu tayari kuna kodi nyingi. Tusikimbilie kwenye hivi vyanzo ambavyo ni rahisi rahisi tu,” amesema Dk Loisulia.
Amesema kuna maeneo mengi mapya, ikiwemo katika bandari, madini, misitu na rasilimali nyingine za asili ambazo wanaweza kupata fedha za kuchangia bima ya afya kwa wote.
“Kila mwaka, tunakimbilia kwenye vyanzo hivi ambavyo tayari vinajulikana. Twende kwenye mambo makubwa. Yaani, hoja yangu kubwa ni kwamba rasilimali zetu za asili zisaidie kutuondolea adha ya vyanzo vya mapato,” amesema.