Sekta nne zaguswa wabunge wakihitimisha mjadala wa bajeti

Muktasari:
- Baadhi ya wabunge wamesema bajeti ya Serikali inaweza kuwainua na kuwakomboa watu masikini, lakini isaidie kufuta nyumba za tembe na nyasi vijijini.
Dodoma. Wabunge wamehitimisha mjadala kuhusu Mpango wa Taifa wa Maendeleo na mapendekezo ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/26, wakiibua hoja katika sekta nne, ambazo Serikali inatakiwa kuzipatia majawabu.
Watunga sheria hao wametoa hoja wakigusa sekta nne za uchumi, afya, elimu na kilimo, ikiwamo ya kutaka nyumba za tembe na nyasi zifutwe vijijini.
Wabunge wamesema hayo, Ijumaa Juni 20, 2025 wakihitimisha mjadala wa siku ya tano kati ya zilizopangwa katika uchangiaji wa bajeti, iliyowasilishwa bungeni Juni 12, 2025 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba.
Baada ya kuhitimisha mjadala, hatua inayofuata Jumatatu Juni 23, 2025 ni mawaziri kujibu hoja zilizojitokeza kabla ya Bunge kupiga kura ya uamuzi Juni 24, 2025.
Umasikini bado
Katika mchango wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Thea Ntara amesema licha ya kuwapo mipango mizuri, lakini Watanzania wengi bado ni masikini na kundi kubwa hawana nyumba bora za kuishi, kwa kuwa katika maeneo mengi bado zipo zilizoezekwa kwa udongo (tembe) na nyasi, hasa vijijini.

Dk Ntara amesema bajeti bila kuweka mazingira rafiki ya kuwainua wananchi kiuchumi bado haitakuwa na manufaa, kwani maeneo mengine vijijini watu wanaishi maisha duni, hivyo haina ulinganifu na bajeti inayopitishwa.
“Waziri, lazima Serikali ije na mpango wa kuwainua watu wa vijijini, tuhamasishe watu wajenge nyumba nzuri ili Serikali ipeleke mabati watu wakaezeke, hiyo itasaidia kuwakomboa kwenye maisha hayo. Mbona linawezekana kwani shida iko wapi?” amehoji.
Dk Ntara ameorodhesha mikoa ambayo wananchi wanaishi kwenye nyumba za nyasi kuwa ni Lindi, Tabora, Mtwara, Ruvuma na Rukwa wakati mikoa yenye nyumba nyingi zilizoezekwa kwa udongo ni Singida, Dodoma, Shinyanga, Manyara na Simiyu.
Kwa mujibu wa Dk Ntara, maisha ya Watanzania kwenye ujenzi inafaa kuigwa mikoa ya Njombe, Dar es Salaam, Kilimanjaro na Katavi ambako maeneo mengi hata ya vijijini wanaishi kwenye nyumba zilizoezekwa kwa mabati na nyingi zimejengwa kwa ubora.
Amesema bajeti ikipitishwa kwa malengo na kuwekewa utaratibu mzuri, inawezekana kufuta nyasi na tembe katika maeneo mengi na hapo kila Mtanzania atafurahi kuishi kwenye nyumba bora.
Mbali ya hayo, amemtaka Waziri wa Fedha kuangalia namna ya kulipa madeni ya wahadhiri wa vyuo vikuu ambao wanadai fedha nyingi, akitoa mfano wa Chuo Kikuu cha Moshi ambao wanadai takribani Sh1 bilioni.
Mbunge huyo amezungumzia deni lingine ambalo Serikali inapaswa kulipa ni la mkono wa kwaheri kwa wakuu wa mikoa na wilaya ambao amesema wanaidai fedha nyingi kwa kuwa walishapitisha utaratibu huo ndani ya Bunge.
Amezungumzia umuhimu wa kuwepo hospitali kubwa ya kupandikiza mimba bure kwa wanawake wenye uhitaji wa kuzaa, akieleza Sh15 milioni zinazotozwa ni kiwango kikubwa, ambacho wengi hawataweza.
Mbunge wa Mbogwe, Nicodemus Maganga ameitaka Serikali kuwashughulikia haraka iwezekanavyo wenyeviti wa halmashauri ambao maeneo yao yanakabiliwa na hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Maganga amesema wakati wabunge wanapokuwa na shughuli za kitaifa Dodoma, kuna wenyeviti wa halmashauri wanapitisha mambo kinyemela bila kufuata utaratibu, hivyo kuisababishia Serikali hasara kubwa.
“Inapofika hatua hiyo lazima hawa wenyeviti wakamatwe na kufunguliwa kesi kwa mujibu wa sheria, haiwezekani fedha zinatumika vibaya halafu watu wanaendelea kuachwa, hii si sawa ni wakati wa kuamua kuchukua hatua,” amesema.
Kwa upande wake, mbunge wa Viti Maalumu, Husna Sekiboko amelalamikia alichokiita ulanguzi katika vyuo, hasa kwenye usajili.
Sekiboko amesema usajili wa wanafunzi kwa vyuo vingi vya Tanzania hauzingatii ubora wa elimu inayotolewa, badala yake wanatazama mapato ya fedha ndiyo maana kumekuwa na shida maeneo mengi.
Amesema vijana wa Kitanzania wanafundishwa masomo ambayo hayaendani na ajira na wanaowafundisha hawatazami hilo ila wanapenda kuangalia wingi wa wanafunzi na ada wanazotoza pekee.
“Tuchukulie mfano nchi kama Sweden, wenzetu vijana wao wanafundishwa kuajiriwa kutoka masoko ya ndani na nje ya nchi yao, lakini sisi kwetu hakuna kitu cha namna hicho, watu wanamaliza kisha wanakosa mwelekeo,” amesema.
Ameitaka Wizara ya Fedha kuangalia namna nzuri ya kutoa fedha kwenye maeneo ya muhimu kama vile uwekezaji wa elimu kwa kuwa ndiyo sehemu pekee ya mafanikio.
Hata hivyo, amesema haitakuwa na hofu kama mpango uliofanywa kwa kurekebisha mitalaa utasimamiwa kikamilifu, kwani matunda yake yameanza kuonekana ikiwamo vijana waliosoma vyuo vya ufundi Veta.
Amesisitiza vyuo vya kati na vyuo vikuu kuwa na msimamo na mpango kabambe wa kuinua taaluma kwa kuangalia uwezo wa vijana wanaodahiliwa, lakini akaonya vijana kuacha kuogopa baadhi ya masomo na kuchagua yale wanaosema ni rahisi.
Mbunge wa Mchinga, Salma Kikwete ametahadharisha kuwa Tanzania ya kesho huenda haitakuwa salama kutokana na maisha ya vijana kwenye kile alichotaja kujibusti.
Salma emeonya mfumo wa maisha kwa vijana wakiwamo wa umri wa miaka 13 wanaokunywa vinywaji kama energy kwa ajili ya kuongeza nguvu, jambo alilosema ni la hatari kwao.
“Hivi vinywaji vya ‘energy’ jamani lazima tuwe makini, vijana wa kiume miaka 13 wanakunywa kwa ajili ya kubusti nguvu zao, hivi tukienda kwa mtindo huo huko mbele itakuwaje,” amehoji.
Ameitaka Serikali kulisimamia jambo hilo na kutoa elimu kuhusu vinywaji hivyo kwani kwa namna yoyote katika siku za usoni vijana wengi, hasa wa kundi la wanaume watakuwa na matatizo.
Katika hatua nyingine, amemwomba Waziri wa Fedha kupeleka fedha za ufuta mapema iwezekanavyo katika Mkoa wa Lindi na hasa jimbo la Mchinga kwani wananchi wanazisubiri kwa hamu.
Mbunge wa Jang’ombe, Ali Hassan King ameitaka Serikali kutenga fedha katika sekta ya michezo ili kusaidia mafunzo kwa makocha wazawa yatakayowapunguza wale wa kigeni ambao amesema wameweka mizizi katika timu kubwa nchini.