Prime
Joto la majimbo juu bungeni, Zungu awatuliza akitoa mbinu

Muktasari:
- Baadhi ya wabunge wanatumia fursa za kuchangia mjadala bungeni kujinadi kuomba kuchaguliwa tena.
Dodoma. Kadri Bunge la 12 linavyoelekea ukingoni, joto la Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 linazidi kupanda, hali inayosababisha baadhi ya wabunge kutumia jukwaa la mjadala wa bajeti kujinadi kwa mafanikio ya kazi walizofanya majimboni mwao.
Wengine, wakitambua ushindani unaotarajiwa, wanatumia fursa hiyo kutoa mbinu na ushauri kwa wenzao kuhusu namna ya kukabiliana na mchakato wa uchaguzi.
Hayo yamejitokea wakati wabunge wanachangia mjadala wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026, hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2024 pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa, ambao utafungwa Juni 24, 2025 kwa kupigia kura ya kupitisha bajeti hiyo.
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kulihutubia Bunge Juni 27, 2025, kabla ya kutangaza rasmi kupitia Gazeti la Serikali tarehe ya kulivunja Bunge, ili kupisha uchaguzi mkuu.
Hayo yanajiri bungeni wakati ambao baadhi ya vyama vya siasa vimeanza kutoa fomu za kuwania nafasi za urais, ubunge na udiwani, huku Chama cha Mapinduzi (CCM), chenye wabunge wengi, kikitangaza kuanza mchakato huo kwa ngazi ya ubunge na udiwani Juni 28, 2025.
Naibu Spika, Mussa Zungu leo Ijumaa Juni 20, baada ya kipindi cha maswali na majibu alipokuwa akiwatambulisha wageni, amesema hatakuwapo Juni 27, hivyo akatumia fursa hiyo kuwashukuru watu kadhaa, akihitimisha miaka mitano ndani ya Bunge la 12.
Mbali ya hayo, amewatajia wabunge mambo matano yatakayowarudisha tena katika nafasi zao ambayo ni adabu, heshima, uvumilivu, kuwajali yatima na wenye kipato cha chini na kutembea na takwimu.
“Kikubwa namshukuru sana Spika wa Bunge (Dk Tulia Ackson) namna tulivyofanya kazi pamoja, nilijitahidi kutii maelekezo yake na kazi zikaenda, lakini nawashukuru ninyi wabunge jinsi mlivyokuwa pamoja nasi, maana bila ninyi mambo hayaendi,” amesema.
Zungu amewataka wabunge kuwa watulivu na wasishindane na watu aliosema wanatukana na kufanya fujo, bali walio madarakani wasifanye hivyo, kwani wana kiongozi ambaye ni nusu mtu na nusu chuma, hivyo watarudi naye.
“Kasemeni mazuri ya Mama na kama hamna takwimu nendeni kwa mawaziri watawapeni hizo takwimu, ili mkazisemee kwa wananchi, jalini yatima ili mpate pepo,” amesema.
Zaidi ya hayo, amewapongeza wananchi wa jimbo la Ilala akisema wamekuwa watu wema kwake na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akiomba Rais atambue kuwa Ilala inatembea na wako pamoja.
Zungu amezungumzia uchaguzi mkuu akisema ni muhimu watu waende na uchaguzi wa mafiga matatu – Rais, wabunge na madiwani.
Zungu amekuwa miongoni mwa wa wabunge ambao kwa kipindi cha karibuni uchaguzi mkuu umekuwa vinywani kwenye mijadala, wakijinadi kwamba wao wanatosha majimboni, hivyo wengine wanaojipitisha huko hawana sababu za kufanya hivyo.
Wengine wamekuwa wakitoa tuhuma za vitendo vya rushwa kufanyika majimboni mwao kwa minajili ya kuwashawishi wapigakura.
Sawa na alivyofanya Zungu, Mbunge wa Viti Maalumu, Husna Sekiboko naye ametoa shukrani kwa viongozi wa juu wa Serikali na wabunge kwa ushirikiano walioupata katika Bunge hilo na kuomba Mungu awasaidie kuwarejesha ili waendelee na kazi hiyo.
“Nilizunguka katika kata, kina mama wametuombea, wamefanya dua, wamefanya matambiko na hii ni ishara kwamba bado wanatamani kuendelea kuwa na mimi binti yao, Husna Sekeboko,” amesema.
Amewashukuru na kutaka waendelee kuwa na moyo huo, akisema katika miaka mitano (ijayo) atakuwa na mwendo wa 5G kama ambavyo amekubaliana na wanawake hao.
Wakati Sekeboko akisema hayo, Mbunge wa Iramba Mashariki, Francis Mtinga anasema yeye pekee ndiye anayejua viporo viko wapi ili kwenda kuvipasha, hivyo wananchi wa Mkalama wahakikishe mtu anayejua viporo vimebaki wapi ndiye wanamrudisha katika uchaguzi huo.
“Hakikisheni mnamrudisha mtu anayejua viporo viko wapi na si hawa wanaojidai wanawapenda wana Mkalama lakini leo hii hawapo bungeni, wameweka kambi huko wanagawa Sh50, 000 kununua wajumbe, wakati wanajua anayewapigania yuko jimboni,” anasema.
Upepo huo haukumwacha Saasisha Mafuwe, mbunge wa Hai aliyewashukuru wananchi jimboni humo akiwakumbusha kuwa yeye bado ni kijana mwenye nguvu na ana ari kubwa ya kuwatumikia.
“Oktoba kama ambavyo nitarudi hapa kuendelea na haya ambayo tumepanga kuyafanya, ninajua nimebakiza kiporo …nimebakiza kiporo cha baadhi ya maeneo ya kujenga barabara na maeneo mengine niko tayari kuwatumikia kama ilivyo kawaida yangu,” amesema.
Kwa upande wake Jacqueline Ngonyani, mbunge wa viti maalumu, yeye ametumia karata ya Rais Samia akisema Oktoba 2025 wanakwenda kuwapigia kura Rais Samia, wabunge na madiwani na anaamini CCM itaibuka na ushindi wa asilimia 100 kwa Mkoa wa Ruvuma.
“Naomba mnipe mitano tena, haki ya Mungu nitafanya zaidi ya hapo nilipofanya. Asanteni sana, namshukuru pia kaka yangu Joseph Mhagama na wabunge wenzangu wengine wote kwa ushirikiano mkubwa walionipa,” amesema.
Ombi kama hilo limetolewa na mbunge wa Buhigwe, Felix Kavejuru kwa wakazi wa jimbo hilo akiwaomba wamwongeze miaka mingine mitano kutokana na kazi walizofanya kwa pamoja.
“Nimekuwa pamoja nanyi, tumefanya kazi kwa pamoja, wasafiri huwa wanaanza safari kwa pamoja, tumelala kwa pamoja tumefanya kazi kwa pamoja, wanaotafuta kuni ndio wanaoota moto pamoja,” amesema na kuongeza:
“Ndugu zangu wakati umefika tena wanasema chanda chema kinatunzwa. Anayefanya vizuri huongezwa, ninaomba mniongeze tena nitaendelea kuwa mwaminifu mbele yenu na mbele ya Mungu,” amesema.
Vilevile, Mbunge wa Mbagala, Abdallah Chaurembo anasema kwa kazi kubwa zilizofanywa na Serikali ya awamu ya sita anaamini wabunge wote watarejea bungeni katika uchaguzi huo.
Hata hivyo, anasema watakaoshindwa kurejea ni wale ambao wana roho mbaya.
“Bunge letu sisi sote tuliokuwapo hapa, kwa kazi kubwa tulizozifanya naamini watakaobaki ni wale wenye roho mbaya kwa sababu roho mbaya haina dawa,” amesema.
Nicodemus Maganga, mbunge wa Mbogwe amewaasa wananchi jimboni humo kuchagua madiwani waaminifu, huku yeye akijisifia kwa kuongeza mapato ya halmashauri hiyo.
“Wananchi wa Mbogwe mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, niwaombe kama mlivyonizaa, mlivyonilea kati ya vitu ambavyo sitavifanya ni kuwa na kundi. Nitaendelea kuwa na misimamo yangu kwa sababu namwamini Mungu, kupitia Mungu haina haja hata kutengeneza safu,” amesema.
Amewataka kuchagua madiwani watakaokuwa wanawafaa na kwa kuwa wanaishi nao wanawafahamu vyema.
“Mnawajua, maana nishasikia maneno maneno mara huyu hatakiwi na mbunge, mimi sina mtu, sina mambo hayo, kwa hiyo chaguaneni kwa kufahamiana na mkiona mtu si mwaminifu hamna sababu ya kumwingiza kwenye siasa za nchi yetu,” amesema.
Mbunge huyo amesema wanaomba Mungu na hata watumishi wa Mungu wawasaidie kuomba ili kupata viongozi waaminifu.
Amesema ameingia katika ubunge Halmashauri ya Mbogwe ikiwa inakusanya mapato ya Sh700 milioni lakini sasa inakusanya Sh3 bilioni. Amewaomba wananchi wachague madiwani waaminifu ili kuwezesha nchi kuendelea kupiga hatua ya maendeleo.
“Hakika mimi sikuwa chawa, nimefanya kazi hii kwa uaminifu mkubwa na sikutaka kuwa chawa wa mtu. Pale ambapo kuna ubaya nilisema kuna ubaya palipokuwa pazuri nilisema hivyo,” amesema.
Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba hakubaki nyuma amewaombea wabunge wote waliofanya kazi iliyotukuka ambao wamesababisha mafanikio makubwa ya uchumi wa Taifa, Mungu awajalie warudi.
“Naona Kinondoni mimi nipo ndugu yenu Tarimba Abbas mwananchi wa Tanzania, nitakuwa pamoja na ninyi Mwenyezi Mungu akijalia katika kipindi kingine cha miaka mitano,” amesema.