Prime
UCHAMBUZI WA MJEMA: Tunahitaji mfumo kupima uwajibikaji wa wabunge, madiwani wa viti maalumu

Uwepo wa Bunge ni matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 (Ibara ya 62(1) na kadhalika, majukumu ya Mbunge yameainishwa ndani ya Katiba Ibara ya 63(1) kuwa ni pamoja na kuuliza swali lolote kwa waziri yeyote lenye masilahi kwa wananchi.
Wajibu mwingine ni kushiriki katika mjadala wa utendaji wa kila wizara na bajeti ya Serikali, kujadili mipango na Serikali ya muda mrefu na mfupi, Kutunga sheria, kujadili na kuridhia mikataba ya kimataifa hushiriki pia kumchangua Spika na naibu wake.
Kuna makundi matatu ya wabunge yakijumuisha wale wa kuchaguliwa kutoka kwenye majimbo ya uchaguzi, wanaoteuliwa na Rais kwa mujibu wa Katiba pamoja na wa viti maalumu. Wabunge wote hawa wawapo bungeni hufanya kazi kwa pamoja.
Wabunge na madiwani wa viti maalumu wanapoingia kwenye vikao wanatakiwa kuongeza uwakilishi wa makundi ambayo pasipo utaratibu huu yatabakia pembezoni pasipo masilahi yao kuingizwa kwenye mipango iwe ya Serikali Kuu au serikali za mitaa.
Hata hivyo, kumekuwepo na sintofahamu miongoni mwa umma wa walipa kodi kwamba, wabunge wa viti maalumu na madiwani, uwajibikaji wao kwa umma ni changamoto kubwa kwani hailingani na mapesa walipa kodi wanayochota.
Wakati wa viti maalumu ambao wanalipwa sawa na wa majimbo na kata, wale wa kuchaguliwa wanakumbana na kibano cha wapiga kura wao wakati wa uchaguzi, ndio maana nauliza hawa wa viti maalumu utendaji wao unapimwa na chombo gani?
Ni lazima kuwe na mfumo wa kupima uwajibikaji wao kwa sababu wanalipwa fedha za umma, ambazo ni kodi yangu mimi na wewe hivyo jimbo lao linapaswa kuwa na wanawake au watu wenye mahitaji maalumu bila kujali itikadi ya chama kilichomteua.
Mbunge analipwa mshahara wa karibu Sh4.8 milioni kwa mwezi, anaingiziwa mshahara wa msaidizi (Katibu) na dereva wake na kama kuna vikao, basi ukichanganya mshahara wake, wasaidizi wake na mafuta analipwa Sh14 milioni kwa mwezi.
Kinachotofautiana kati ya mbunge wa jimbo na wa viti maalumu ni kwamba wa jimbo anapewa fedha za mfuko wa jimbo, lakini mshahara, posho na stahiki zingine wanalingana kwa viwango licha ya majukumu mazito ya mbunge wa jimbo.
Kwa upande wa diwani, ninaambiwa analipwa posho ya Sh350, 000 kwa mwezi na katika kila kikao analipwa posho ya Sh70, 000 na madiwani wanakuwa na vikao vya kamati za kudumu angalau kila baada ya miezi mitatu.
Fedha hizi ni za umma, tunawezaje kulipa fedha nyingi hivi kundi la viti maalumu hasa lile la ubunge ilihali hakuna mfumo wa kufuatilia wanavyowajibika kwa umma kwa sababu ndio waajiri wao wanaowalipa mishahara.
Mbunge au diwani akishachaguliwa anakuwa mbunge au diwani wa wote bila kujali anatoka chama gani, hivyo wananchi wana haki ya kumuhoji asipotimiza wajibu na majukumu yake ya kibunge na wanaweza kumwajibisha kupitia sanduku la kura.
Makala hii inaweza kuonekana ikiwazungumzia zaidi wabunge na madiwani wa viti maalumu kutoka CCM, hii ni kwa sababu ndio ambao ni zaidi ya asilimia 95, lakini ukweli ni kwamba dhamira ya makala hii iwaguse wote na wa vyama vya upinzani.
Kwa bahati mbaya, kinachotokea huku majimboni na kwenye kata hivi sasa ni kwamba baadhi ya wabunge na madiwani wa viti maalumu wanahangaika na wapiga kura wao tu ambao ni wanawake wa CCM kupitia Jumuiya ya Wanawake (UWT) au wenye nasaba na CCM pekee.
Mbunge viti maalumu akifika jimboni ataonana na Katibu wa UWT), anamuambia naomba niitie wajumbe (wapiga kura), ambalo ni kundi la watu 200 au 300 kana kwamba yeye anawajibika kwao tu, ni wabunge wachache sana wanaohudumia wanawake bila kujali itikadi za vyama.
Tunachokiona sasa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, ni kwa baadhi ya wabunge wa viti maalumu kuwakusanya wanawake kwa mwavuli wa wanawake, lakini hawa wote ni wapiga kura katika kura za maoni viti maalumu ili wawarejeshe tena.
Tena wanazunguka huku na huko wakigawa mashuka, vitenge au khanga na wapo wanaogawa vyote viwili pamoja na fedha taslimu Sh50,000 kwa waalikwa. Ndugu zangu, tunapimaje mchango wao bungeni katika kuisemea jamii ya wanawake?
Kwa CCM maelezo yatakuwa hao wabunge wanawajibika kwa UWT, kama hivyo ndivyo je, wale wabunge 19 waliokuwa wanatokana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) uwajibikaji wao unapimwaje? Hawa nao wanapokea fedha za umma.
Hii ndiyo sababu ya kuja na pendekezo la kuwapo kwa mfumo mahususi wa kupima uwajibikaji wa wabunge na madiwani wa viti maalumu kwa sababu hawa wanalipwa mishahara na posho kwa kodi za Watanzania bila kubagua itikadi zao za vyama.
Ninatamani, iwe kama ambavyo Rais anagombea kupitia chama kimoja lakini pindi anapoingia Ikulu anakuwa wa wote bila kujali itikadi. Hivi ndivyo inavyotakiwa kwa wabunge na madiwani wa viti maalumu, wasijielekeze kwa wapiga kura wao pekee, walenge wanawake.
Wakati umefika wa kuachana na dhana kwamba ubunge na udiwani wa viti maalumu ni zawadi anayopewa mtu bila kuhojiwa ataitumiaje. Hawa wanalipwa fedha za umma sawa na wale wa majimbo ya uchaguzi na madiwani wa kata ambao wanawajibishwa kupitia sanduku la kura.
Ni kutokana na ukosefu wa mfumo wa uwajibikaji ndio maana mwaka 2013 aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samwel Sitta (marehemu), alitamani viti hivyo vifutwe na hata ukiwahoji Watanzania leo, baadhi wataungana na Sitta.
Sitta alibainisha kuwa wengi hawachangii lolote bungeni na hawana yeyote kwa kuwahoji na kuwapima kama ilivyo kwa wabunge wa majimbo, na akatamani viti hivyo vifutwe kwani ni mzigo kwa Taifa. Inawezekana mawazo yake yanawagusa pia madiwani.
Ni kweli kuna umuhimu wa uwepo wao kutokana na mfumo dume, mila na tamaduni ambazo zinamfanya mwanamke asiweze kugombea kushindana na wanaume. Sina tatizo na hilo kwa sababu zimewafanya wengi washindwe kujiamini kugombea jimbo.
Ni utaratibu unaopatikana katika nchi mbalimbali za Afrika na Asia na hadi mwaka 2013, nchi 36 za Afrika zilitumia mfumo huo. Hata hivyo, kuna nchi zingine huko duniani wananchi hupiga kura mbili, moja ya mbunge wa jimbo na ya pili ya viti maalumu.
Lakini kuna mkataba wa Haki za Kisiasa kwa Wanawake uliopitishwa na mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) wakati wa kikao chake cha 409 kilichoketi Desemba 20,1952 na unalenga kuhakikisha haki za kisiasa kwa wanawake.
Hiyo ni njia mojawapo ya kuingiza bungeni au kwenye udiwani makundi ambayo ni vigumu kuingia kwa njia ya kisiasa, kwa mfano watu wenye ulemavu.
Binafsi natamani tuendelee kuwa na viti maalumu vya wabunge na madiwani ili kuwajengea uwezo wa kwenda kugombea majimboni, lakini pamoja na dhamira hiyo njema, basi tuwe na mifumo itakayowafanya wawajibike kwa umma unaowalipa mishahara na posho.
Ni kweli ibara ya 66(1(b) ya Katiba ya Tanzania inasema kutakuwa na wabunge wanawake wa idadi inayoongezeka, kuanzia asilimia 20 ya wabunge waliochaguliwa kuwakilisha majimbo watakaochaguliwa na vyama vya siasa. Sina tatizo kwani ndio utaratibu ulivyo.
Siamini kama tuliamua kuanzisha viti maalumu vya ubunge au udiwani ili anayeteuliwa ahudumie wale tu wanaompigia kura za maoni ama ashirikiane na makundi yale tu yenye nasaba na chama kilichomteua, la hasha anapaswa ahudumie wanawake wote bila itikadi.
Pamoja na kutumia mamlaka yale ya Ibara ya 63 ya Katiba ya kuishauri na kuisimamia Serikali katika masuala ya wanawake kijimbo na kitaifa, lakini yeye anapaswa kuwa mbunge wa wanawake wote bila kujali itikadi ya chama.
Kipimo kizuri ni kupata kura ya maoni ya kundi husika na siyo chama cha siasa. Mbunge au diwani viti maalumu aulizwe ni mara ngapi amefanya mikutano ya kwenye jimbo au kata kujua na kutatua kero na changamoto za kundi analoliwakilisha.
Ndio maana nasema ni muhimu sana tukatafuta mfumo wa kupima uwajibikaji wa wabunge na madiwani wa viti maalumu na ni kwa njia hiyo pekee, wananchi wataona mchango wao katika jamii badala ya hali ya sasa baadhi wanaona ni kuchezea pesa za walipa kodi.
Tunaona michango yao bungeni (kwa wale wanaochangia), tunaona maswali yao lakini baadhi yao tunaona wanavyotumia vibaya Bunge na kuligeuza kama kijiwe cha mipasho, kejeli na vijembe, badala ya kutumia muda huo adhimu kuwasemea Watanzania bila kuingiza itikadi za vyama.
Ninatamani kuwepo kipimo cha kupima walivyotumia ubunge wao kuhudumia jamii bila kubagua kulingana na itikadi maana pesa hizi ni za Watanzania wote.