Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasira arusha jiwe gizani wanaosema wanamdai Rais Samia

Muktasari:

  • Amesisitiza kuwa kwa kazi nzuri na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, anastahili pongezi.

Geita. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema si sahihi kumtarajia Rais Samia Suluhu Hassan kumaliza matatizo yote ya wananchi, akisisitiza kuwa anayefikiri hivyo anajidanganya.

Akizungumza leo Alhamisi Juni 19, 2025 kwenye mkutano wa ndani na wanachama wa CCM mjini Geita, uliolenga kukiimarisha chama, Wasira amesema kauli ya kumwambia Rais ‘tunakudai’ haina maana.

Hata hivyo, bila kumtaja jina, kauli hiyo imeonekana kumlenga Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, ambaye katika ziara ya Rais Samia mkoani Simiyu, alimtaka Rais kuangalia zaidi jimbo lake kwa maelezo kuwa bado linamdai miradi ya maendeleo.

“Nimemsikia rafiki yangu mmoja akimwambia Rais sisi tunakudai. Wenzake wanampongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa muda mfupi. Hiyo haimaanishi kuwa matatizo yote yamemalizika, kwa sababu matatizo hayawezi kuisha yote. Akimaliza yote sasa, tutamchagua Rais mwingine wa nini? ” amesema Wasira.

Amesisitiza kuwa kwa kazi nzuri na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia,  anastahili kupewa muda zaidi wa kuiongoza nchi.

Amesema kama matatizo yote yangekuwa yanamalizika, kusingekuwa na maana ya kuandika Ilani ya Uchaguzi mpya mfano ya mwaka 2025-2030.

Akiendelea kufafanua, Wasira amesema hata wabunge na madiwani waliowahi kushika madaraka, hawakuwahi kumaliza matatizo yote ya wananchi waliowawakilisha.

“Kwa hiyo anayemlaumu Rais kwa kutomaliza kila tatizo, ajitazame naye alifanya nini wakati alipokuwa na nafasi,” ameongeza.

Akizungumzia mbunge huyo bila kumtaja jina moja kwa moja, Wasira amesema licha ya kuwa ni rafiki yake, lakini ameingia choo si chake kwa kauli yake.


Kuhusu uchaguzi

Akigusia Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, Wasira ameeleza nia yake ya kufanya ziara katika majimbo ya Mkoa wa Geita ni kutaka kufanya tathmini, kutokana na viashiria vya matumizi makubwa ya fedha (rushwa) wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya chama.

“Tunahitaji viongozi waadilifu na wanaoaminiwa na wananchi. Kuna mchezo wa kusambaza fedha kama kwamba watu wananunua mazao. Haiwezekani ukatumia fedha za mbunge pekee kuhonga wajumbe bila kuwa na shughuli nyingine halali ya kiuchumi,” ameonya.

Wasira amesema matumizi ya fedha nyingi kwa ajili ya kununua uongozi ni ishara ya hitilafu ya kiakili.

“Kama mtu anatoa Sh1 bilioni kupata ubunge, anahitaji matibabu ya akili. Unaenda kufanya nini bungeni kwa gharama hiyo? Kama una fedha, fanya biashara siyo kununua ubunge,” amesema kwa msisitizo.

Kauli hiyo ilishangiliwa kwa nguvu na wanachama waliokuwepo kwenye mkutano huo wa ndani, huku Wasira akieleza kuwa CCM haipingani na watu wenye uwezo, bali inapinga matumizi ya fedha kama njia ya kupata madaraka.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicolaus Kasendamila akizungumza kwenye mkutano huo, amesema Serikali imefanya kazi kubwa mkoani humo ikiwamo ujenzi wa vituo vya afya, barabara, miundombinu ya elimu na maboresho ya huduma za kijamii.

Kasendamila amesema mafanikio hayo ni sababu tosha kwa wananchi kuendelea kumpatia Rais Samia ridhaa ya kuongoza kwa muhula mwingine.

Wasira anaendelea na ziara yake ya kukiimarisha chama kwa kuzungumza na wanachama na wananchi kupitia mikutano ya ndani na ya hadhara aliyoanza Juni 10, 2025 mkoani Ruvuma na leo amemalizia mkoani Geita na kesho atakuwa mkoani Mwanza.