Wasira- CCM ipo tayari kukosolewa lakini...

Muktasari:
- Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara Stephen Wasira, amewataka wanachama wa chama hicho kutokubali rushwa za wagombea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, kwani kiongozi mtoa rushwa siyo muwajibikaji.
Mbogwe. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kipo tayari kukosolewa kinapokiuka kanuni za utawala bora huku kikionya wakosoaji kutotumia njia za kuondoa amani na umoja miongoni mwa wananchi.
Kauli hiyo ya CCM imetolewa leo Juni 16, 2025 na Makamu wake Mwenyekiti Bara, Stephen Wasira alipozungumza na wananchi na viongozi wa CCM Jimbo la Mbogwe mkoani Geita kupitia mkutano wake wa ndani.
"Nawaambia chama chetu kinasimamia amani na kipo tayari kukosolewa ikiwa wanasema tunavunja kanuni za utawala bora, lakini wao wanaotukosoa tunawaambia wasitumie njia haramu kuvuruga amani na kuvunja haki za watu wengine," amesema.
Wasira amesema suala la uchaguzi mkuu lipo kikatiba, hivyo ni lazima ufanyike kulingana na matakwa ya sheria zilizopo akisisitiza utawala bora ni pamoja na kuufuata bila kuvunja amani.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira akizungumza na wanachama CCM na wananchi wa Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita kupitia mkutano wa ndani
Akisisitiza kuhusu uchaguzi, Wasira (bila kutaja mtu) amesema hakuna anayeweza kuzuia uchaguzi kwa kuvuruga amani kwani gharama ya kufanya hivyo ni kubwa.
"Amani ikikosekana watakaoathirika ni wazee, wanawake na watoto, sasa akija kiongozi wa kisiasa akawaambia uchaguzi unaahirishwa, utaahirishwa kwa sheria gani? Kwanza hawana uwezo wa kuzuia ila hawana aibu ya kusema uchaguzi watauzuia," amesema.
Mbali na hayo, Wasira amewataka wananchi na wanachama wa CCM kutompa nafasi mgombea yeyote anayepenyeza rushwa kupata madaraka kwani kiongozi wa namna hiyo hatakwenda kuwatumikia.
Wasira yupo mkoani Geita kwa ziara ya siku nne kuanzia Juni 16 hadi 19 akitokea mkoani Ruvuma, ambako nako alifanya ziara kuzungumza na wanachama na viongozi wa CCM kupitia mikutano ya ndani akiinadi CCM kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.

Baada ya Wasira kuhitimisha mkutano wake mkoani Geita Juni 19, 2025, atarejea mkoani Mwanza kufanya mikutano ya ndani na kumalizia mkutano mmoja wa hadhara lengo kuu kuwaomba wananchi na wanachama wa CCM kukiamini kwa mara nyingine chama hicho.
Kauli ya viongozi wengine
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicolaus Kasendamila amesema tayari chama hicho mkoani hapo kimewaandaa wananchi kwa ajili ya uchaguzi mkuu na wapo tayari kupiga kura.
"Niliwaambia viongozi wajitahidi kuleta wagombea wazuri. Tulianza mwaka jana na hakika walifanya hivyo kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa tukashinda.
"Sasa niwaombe wagombea wanaokuja tuwasikilize hoja zao na uzalendo wao bila kutegemea rushwa. Tunakwenda kwenye uchaguzi, nyie ndiyo chanzo cha kuleta wagombea wazuri," amesema.
Kutenga wagombea wenye ushawishi umeshapitwa na wakati, wapeleke wagombea wanaokubalika.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohamed amesema tangu mwaka 2021 hadi sasa miradi ya maendeleo ya Sh76 bilioni imetekelezwa wilayani hapo chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ikijumuisha sekta za elimu, barabara na umeme.
Balozi wa shina namba nane Kata ya Masumuni Wilaya ya Mbogwe, Rehema Kasudi ameiomba CCM kiendelee kuwapata kipaumbele mabalozi kwa nyakati zote hata baada ya uchaguzi mkuu.