Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasira kuendelea kuinadi CCM Nyasa leo

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira

Muktasari:

  • Katika ziara yake ya siku nne mkoani Ruvuma, leo Wasira anatarajiwa kuzungumza na makundi mbalimbali ya wananchi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Nyasa. Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, anatarajiwa leo, Juni 11, 2025, kuzungumza na makundi mbalimbali ya wananchi pamoja na wanachama wa CCM katika Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, ikiwa ni sehemu ya harakati za kukinadi chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Mkutano huo wa ndani, ambao Makamu Mwenyekiti Wasira atazungumza na wanachama wa CCM, wazee, viongozi wa dini, viongozi wa mila pamoja na viongozi wa chama na jumuiya zake, ni wa pili kufanyika, baada ya kukutana na makundi kama hayo jana katika Wilaya ya Tunduru.

Akizungumza jana na makundi mbalimbali ya wananchi, wanachama wa CCM, viongozi wa dini, wazee na viongozi wa mila wilayani Tunduru, Wasira, alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza kuwa sababu pekee ya kuahirisha uchaguzi ni kutokea kwa vita, na Tanzania haina vita yoyote.

Kauli hiyo ya Wasira inakuja ikiwa ni majibu kwa madai ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho kimependekeza uchaguzi huo uahirishwe kwa angalau miezi sita ili kuwezesha kufanyika kwa marekebisho ya sheria mbalimbali zitakazohakikisha uchaguzi huru, wa haki na wa ushindani kwa vyama vyote.

Licha ya pendekezo hilo, Chadema kimeendelea kusisitiza kampeni yake ya kitaifa ya “hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi” (No Reforms, No Election), huku CCM kikijibu kwa kauli mbadala yenye msisitizo: “Oktoba Tunatiki.”

Katika ziara yake ya leo, Wasira atazungumza na wananchi wa Nyasa kuhusu mambo yaliyofanywa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na sababu za wao kuichagua CCM kwa awamu nyingine ya 2025-2030.

Baada ya mkutano huo, Wasira ataelekea wilayani Mbinga ambako atakutana tena na makundi kama hayo kuendelea kuinadi CCM kupitia mikutano ya ndani.

Tangu alipotua mkoani Ruvuma Juni 9, 2025, Wasira ameendelea kusisitiza kuwa CCM kimejipanga kushiriki uchaguzi, tayari kimemtangaza Rais Samia kama mgombea urais na Dk Emmanuel Nchimbi kama mgombea mwenza, wanaosubiri kupitishwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Bara yupo mkoani Ruvuma kwa ziara ya siku nne ya chama, kuanzia Juni 9 hadi Juni 13, atakapohitimisha ziara hiyo na kuelekea mkoani Mwanza ambako atafanya ziara nyingine kuanzia Juni 15 hadi 18.