Prime
Mapya yaibuka mikutano ya Chadema, CCM

Muktasari:
- Vyama hivyo vimeendelea na ziara zao katika mikoa mbalimbali, Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Stephen Wasira anaendelea na ziara zake mkoani Ruvuma wakati Makamu Mwenyekiti wa Chadema – Bara, John Heche akiwa Tabora.
Mikoani. Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kikieleza kwamba kaulimbiu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya ‘No reforms, no election’ haina tofauti na nyingine zilizopita, Chadema imekumbana na vurugu kwenye mkutano wake wa kwanza mkoani Tabora.
Vyama hivyo vimeendelea na ziara zao katika mikoa mbalimbali huku Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Stephen Wasira akiendelea na ziara zake mkoani Ruvuma na leo Juni 10, 2025 alikuwa Wilaya ya Tunduru.
Kwa upande wa Chadema, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche ameanza ziara Tabora na leo alikuwa Wilaya ya Igunga ambako mkutano wake uliingiliwa na vurugu zilizofanywa na baadhi ya watu.
Jeshi la Polisi Wilaya ya Igunga liliingilia kati kutuliza ghasia hizo na kufanikiwa kumkamata kijana anayetuhumiwa kuwa miongoni mwa vijana walioanzisha vurugu hizo, zilizosababisha baadhi ya wananchi kuumizwa.
Mikutano hiyo imekuwa ni ya majibizano baina ya vyama hivyo.
Wasira awavaa Chadema
Akiwa Tunduru, Wasira amesema kaulimbiu ya Chadema haina tofauti za zingine zilizowahi kutolewa na chama hicho huku akiwahimiza mabalozi wa CCM kuhakikisha wananchi wanashiriki uchaguzi.
Wasira amewataka wananchi kutobabaishwa na No reforms, no election (bila mabadiliko, hakuna uchaguzi) kwa kuwa, ni kawaida ya Chadema kuja na kaulimbiu ikiwamo ya ‘No hate, no fear’ (hakuna chuki, hakuna kuogopa) na ile ya Movement for Change (M4C – Vuguvugu la Mabadiliko) na sasa hazitumiki.
Wasira ameeleza hayo wakati wa ziara yake Tunduru mkoani Ruvuma kupitia mkutano wa ndani wa chama hicho uliowahusisha viongozi wa dini, jumuiya za CCM, wazee, viongozi wa kimila na wanachama wa CCM.
“Kwa sheria gani tuahirishe uchaguzi, kwa sheria gani? Sheria inaelekeza uchaguzi utaahirishwa kama kuna vita na hakuna vita Tanzania, hakuna uwezekano wowote kwa kuzingatia Katiba kuahirisha uchaguzi.
“No Reforms, no election, kwanza ni kaulimbiu, zipo nyingi, zinakuja na kufa. Walikuja na kaulimbiu ya M4C, sasa hivi haipo, wakaja na nyingine ‘No hate, no fear’, sasa hivi ipo baada ya uchaguzi wa chama chao, kaulimbiu ikafa. Kwa hiyo hii ‘No reforms, no election’ isiwazuie kulima korosho, hamna kitu hapa,” amesema Wasira.
Kiongozi huyo wa CCM amesema chimbuko la kaulimbiu ya Chadema ya sasa ni baada ya chama hicho kujitoa kwenye maridhiano wakishinikiza Serikali kutekeleza mambo ambayo yasingewezekana, ikiwamo wabunge 19 wa viti maalumu wa chama hicho kuondolewa bungeni na madai ya Katiba mpya.
Akiwa, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema chama hicho kinajivunia kazi alizofanya Rais Samia Suluhu Hassan na kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, yeye ni karata muhimu ya ushindi wa chama hicho.
Makalla amesema kazi alizofanya Rais Samia zitakifanya chama hicho kisifanye kampeni kubwa kueleza mambo yaliyofanywa kwa kuwa, kazi zinaonekana kwenye ngazi zote kuanzia za chini.
“CCM hatutopata shida, ya kufanya kampeni kubwa kueleza mambo yaliyofanywa kwa sababu tunajivunia kazi zilizofanywa na Samia zinaonekana katika vitongoji, vijiji, kata, mitaa, kila mahali pana alama ya kazi nzuri zilizofanywa na Samia, sekta zote amezigusa, tunapoelekea uchaguzi mkuu, Samia ni karata muhimu ya ushindi wa CCM,” amesema.
Makalla amesema Rais Samia ameweka alama kila mahali kuanzia sekta ya elimu, afya, miundombinu, maji na sekta zingine, akitolea mfano katika mkoa wa Kilimanjaro wenye vijiji 519, vijiji vyote vina umeme na kazi inayoendelea hivi sasa ni kusambaza umeme kwenye vitongoji,” amesema.
Vurugu mkutano wa Chadema
Wakati Chadema ikianza ziara za mikutano yake Tabora, mkutano wa Heche umekabiliwa na vurugu zilizofanywa na vijana ambao hawajatambulika huku mmoja wao akishikiliwa na Jeshi la Polisi.
Kijana mmoja, mkazi wa Kijiji cha Ibuta kilichopo Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani humo kwa tuhuma za kuanzisha vurugu, kushambulia na kujeruhi watu katika mkutano wa hadhara wa Chadema.
Mkutano wa Igunga ulianza kwa amani kwa viongozi kadhaa kuhutubia, lakini hali ilibadilika Mwenyekiti wa Bavicha, Deogratius Mahinyila alipopanda jukwaani, liliibuka kundi la vijana waliokuwa katikati ya umati, wakaanza kupiga kelele na kurusha maneno, hali iliyovuruga utulivu.
Pamoja na kupiga kelele, kundi hilo la vijana wanaodaiwa kutoka Kijiji cha Ibuta, walichomoa vitu kutoka maungoni mwao kwa lengo la kuwatishia walinzi binafsi wa Chadema waliowasogelea kuwasihi waache kupiga kelele.
Wakati baadhi ya vijana walioibua vurugu katikati ya mkutano wakichomoa visu, kundi lingine la vijana lililokuwa pembeni kidogo lilianza kuwarushia mawe kwa waliokuwepo kwenye mkutano, hali iliyoibua taharuki huku walinzi wa Chadema wakiimarisha ulinzi kwa viongozi wao.
Gari la polisi lililosheheni askari waliovaa sare wakiwa wamejihami kwa silaha na mabomu ya kutoa machozi liliwasili eneo la mkutano baada ya kupita dakika 30 tangu vurugu zilipotokea.
Dakika 10 baadaye, Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Igunga, Meshack Sumuni aliwasili eneo hilo akiongozana na askari wengine waliovaa kiraia na kuanza kutoa maelekezo kwa askari kutawanyika kwa kukaa kona zote za uwanja wa mkutano.
Muda mfupi baadaye, askari kanzu walimnyakua kijana aliyekuwa amejificha kwa kujichanganya katikati ya mafundi seremala waliokuwa jirani na uwanja wa mkutano.
Akizungumzia tukio hilo akiwa ofisini kwa Sumuni, Heche amesema: “Tunasikitika kwamba licha ya sisi kutoa taarifa mapema, Jeshi la Polisi halikuchukua hatua za dhati kudhibiti uvunjifu wa amani katika mkutano wetu.
“Vitendo vya aina hii ni hatari siyo tu kwa usalama wetu viongozi, bali pia amani na utulivu iwapo vijana wa Chadema wataamua kuchukua hatua kujibu mapigo.”
Akizungumza na viongozi wa Chadema waliofika Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Igunga, Sumuni amesema polisi inawasaka vijana wawili kuhusiana na tuhuma hizo.
“Kwanza, Jeshi la Polisi tunatoa pole na tunasikitishwa kwa kilichotokea; na tayari tunamshikilia mtu mmoja na tunawasaka wengine wawili kwa mahojiano,” amesema Sumumi.
Kutokana na tukio hilo, Sumuni amesema jeshi hilo tayari limeimarisha ulinzi katika mikutano mengine ya Chadema itakayofanyika wilayani Igunga.
“Tukio hili limetufanya tuongeze tahadhari ya ulinzi katika mikutano yenu yote wilayani Igunga,” amesema Sumuni.