Vurugu zaibuka mkutano wa Chadema Igunga, mmoja mbaroni

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche akisisitiza wakati akizungumzia tukio la kundi la vijana kuvamia na kufanya vurugu wakati wa mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika mjini Igunga. Picha na Peter Saramba
Muktasari:
- Viongozi wa Chadema wako katika ziara ya kampeni ya No reforms, no election katika mikoa ya Kanda ya Magharibi inayoundwa na mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi.
Igunga. Kijana Lufigo Bundala, mkazi wa Kijiji cha Ibuta kilichopo Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani humo kwa tuhuma za kuanzisha vurugu, kushambulia na kujeruhi watu katika mkutano wa hadhara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) uliofanyika leo Jumanne Juni 10, 2025.
Akizungumza na viongozi wa Chadema waliofika Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Igunga, Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Igunga, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Meshack Sumuni amesema polisi inawasaka vijana wawili kuhusiana na tuhuma hizo.
Bundala pamoja na wenzake waliofanikiwa kukimbia wanatuhumiwa kuanzisha vurugu kwa kupiga kelele, kurusha mawe na kujeruhi watu wakati wa mkutano wa hadhara wa Chadema uliofanyika Uwanja wa Sokoine mjini Igunga.
“Kwanza, Jeshi la Polisi tunatoa pole na tunasikitishwa kwa kilichotokea; na tayari tunamshikilia mtu mmoja na tunawasaka wengine wawili kwa mahojiano,” amesema Sumumi.
Kutokana na tukio hilo, OCD Sumuni amesema jeshi hilo tayari imeimarisha ulinzi katika mikutano mengine ya Chadema itakayofanyika wilayani Igunga.
“Tukio hili limetufanya tuongeze tahadhari ya ulinzi katika mikutano yenu yote wilayani Igunga," amesema Sumuni.
Hata hivyo, maelezo hayo ya OCD Sumuni hayakuwaridhisha viongozi wa Chadema ambapo Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila amehoji kwanini askari polisi hawakuwepo eneo la mkutano wakati wa vurugu.
Akijibu swali hilo, OCD Sumuni amesema ofisi yake iliwatanguliza askari kanzu ambao ndio walifanikiwa kuwanasa kumkamata mmoja wao na kutiwa mbaroni.
“Kwa mbinu na taratibu zetu za kiintelijensia, tuliwatanguliza askari waliovaa kiraia pale uwanjani ambao ndio wamefanikisha kuwatambua na wahusika ambao mmoja tunamshikilia na wengine tunaendelea kuwasaka,” amesema Sumumi.
Kauli ya Heche
Akizungumzia tukio hilo akiwa ofisini kwa OCD, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche amesema chama hicho kilipata taarifa za uwepo wa njama za kuvuruga mkutano wa Igunga na ilitimiza wajibu kwa kuzifikisha polisi, hivyo wanasikitika kitendo cha Jeshi la Polisi kutochukua hatua madhubuti hadi watu wamejeruhiwa.

Mzee ambaye jina lake halikufahamika mara moja akiwa amefungwa bendera ya Chadema kuzuia damu iliyokuwa inavuja baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa jiwe na vijana walioanzisha vurugu wakati wa mkutano wa Chadema mjini Igunga.
“Tunasikitika kwamba licha ya sisi kutoa taarifa mapema, Jeshi la Polisi halikuchukua hatua za dhati kudhibiti uvunjifu wa amani katika mkutano wetu; vitendo vya aina hii ni hatari siyo tu kwa usalama wetu viongozi, bali pia amani na utulivu iwapo vijana wa Chadema wataamua kuchukua hatua kujibu mapigo,” amesema Heche.
Tukio lilivyotokea
Mkutano wa Igunga ambao ni wa kwanza kwa Mkoa wa Tabora ulianza kwa amani kwa viongozi kadhaa kuhutubia, lakini hali ilibadilika mara Mwenyekiti wa Bavicha, Deogratius Mahinyila alipopanda jukwaani ili amkaribishe Heche kuhutubia, ndipo kundi la vijana waliokuwa katikati ya umati kuanza kupiga kelele na kurusha maneno, hali iliyovuruga utulivu.
Pamoja na kupiga kelele, kundi hilo la vijana wanaodaiwa kutoka Kijiji cha Ibuta, walichomoa vitu kutoka maungoni mwao kwa lengo la kuwatishia walinzi binafsi wa Chadema waliowasogelea kuwasihi waache kupiga kelele.
Wakati baadhi ya vijana walioibua vurugu katikati ya mkutano wakichomoa visu, kundi lingine la vijana lililokuwa pembeni kidogo lilianza kuwarushia mawe kwa waliokuwepo kwenye mkutano, hali iliyoibua taharuki huku walinzi wa Chadema wakiimarisha ulinzi kwa viongozi wao akiwemo Heche aliyekuwa ameketi jukwaa kuu.
Watu wawili ambao majina yao hayakupatikana kwa haraka, walijeruhiwa kwa kupigwa ngeu na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Gari la polisi lililosheheni askari waliovaa sare wakiwa wamejihami kwa silaha na mabomu ya kutoa machozi liliwasili eneo la mkutano baada ya kupita dakika 30 tangu vurugu zilipotokea.
Dakika 10 baadaye, OCD Sumuni naye aliwasili eneo hilo akiongozana na askari wengine waliovaa kiraia na kuanza kutoa maelekezo kwa askari kutawanyika kwa kukaa kona zote za uwanja wa mkutano.
Muda mfupi baadaye, askari kanzu walimnyakua kijana Bundala aliyekuwa amejificha kwa kujichanganya katikati ya mafundi selemara waliokuwa jirani na uwanja wa mkutano.
Msimamo wa Bavicha
Akizungumza muda mfupi baada ya vurugu kutulizwa na walinzi wa Chadema, Mwenyekiti wa Bavicha, Deogratius Mahinyila amewagiza vijana wa Chadema kote nchini kulinda mikutano na kuwalinda viongozi wa chama hicho ili kuwahakikishia usalama katika mikutano na shughuli zote za kisiasa.
“Chadama hatutakuwa waanzilishi wa vurugu wala fujo, lakini hatutakuwa wanyonge pale tunapochokozwa, tutajilinda, tutawalinda viongozi na kukihami chama chetu kwa wivu mkubwa,” amesema Mahinyila
Njama za vurugu
Akizungumza ofisi kwa OCD Igunga, Mahinyila amesema chama hicho kilianza kukumbana na vikundi vya vijana wanaoandaliwa kufanya vurugu kwenye mikutano yake baada ya mkutano wao mjini Dodoma uliohudhuriwa na umati wa watu.
"Baada ya mkutano wetu wa Dodoma, washindani wetu wameingiwa hofu na sasa wameanza kuandaa vijana wa kufanya vurugu kwenye mikutano yetu. Tunaiomba Jeshi la Polisi watimize wajibu wa ulinzi na usalama kwenye mikutano yetu," amesema Mahinyila
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Magharibi, Dickson Matata amesema uongozi wa kanda hiyo tayari imechukua hatua za dharura kuimarisha ulinzi katika mikutano iliyosalia kwenye mikoa ya Tabora, Kigoma na kativi zinazounda kanda hiyo.