CCM yazidi kutikisa Kilimanjaro, zamu ya Rombo leo

Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa CCM,Amos Makalla akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Manyema, Moshi Mjini jana Jumapili Juni 8,2025 akiwa anaendelea na ziara yake katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Muktasari:
- Katika ziara hiyo pamoja na masuala mengine Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa CCM,Amos Makalla,amesisitiza juu ya kulinda amani kuelekea uchaguzi mkuu huku akisema ilani ya chama hicho ya mwaka 2025/2030 ni ilani ya wananchi inalenga kujenga uchumi wa wananchi
Rombo. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla anaendelea na ziara yake mkoani Kilimanjaro na leo atafanya mikutano ya hadhara wilayani Rombo.
Makalla alianza ziara ya siku saba katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini kuanzia Juni 4, 2025, alianzia mkoani Manyara alikofanya mkutano wa hadhara wilayani Babati kisha akaelekea mkoani Arusha.
Ziara hiyo yenye lengo la kujibu kile alichokiita upotoshaji uliofanywa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, John Heche ambao hivi karibuni walifanya mikutano yao ya kunadi kampeni ya chama hicho ya No reform No Election kwenye mikoa hiyo ya Kanda ya Kaskazini.
Kwa mujibu wa ratiba, leo Katibu huyo atafanya mkutano mmoja wa hadhara eneo la Tarakea wilayani Rombo.
Jana Juni 8, 2025 Makalla aliingia mkoani Kilimanjaro akitokea Mkoa wa Arusha na alisimama na kusalimia wananchi wa eneo la Usariver (Arusha), Bomang'ombe wilayani Hai kisha kufanya mkutano wa hadhara Moshi Mjini.
Katika maeneo ambayo ameshapita, miongoni mwa masuala aliyozungumzia ni pamoja na kusema si kweli kinachosemwa na Chadema kuwa licha ya rasilimali zilizopo nchini bado wananchi ni maskini na kuwa, uchumi wa mikoa hiyo umezidi kukua kutokana na sekta ya utalii.
Amesema filamu ya utalii ya Royal Tour iliyochezwa na Rais, Samia Suluhu Hassan, imechangia kuongezeka kwa mapato ya utalii na mzunguko wa fedha katika mikoa hiyo.
Makalla amesema mambo yanayoendelea yanachagizwa kutokana na wananchi kuendelea kuwa na imani na CCM, akisema ahadi ya chama hicho tawala ni kuwatumikia Watanzania na kuwaletea maendeleo.
Jambo kingine ambalo kiongozi huyo amekuwa akilisisitiza kwenye mikutano yake ni pamoja na kuwataka Watanzania kuwaepuka viongozi wanaotaka kuwapandikizia chuki kwa lengo la kuligawa taifa kwa misingi ya udini au ukabila hasa kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumzia ilani ya chama hicho ya 2025/2030, Makalla alisema ni ya wananchi kwa sababu inalenga pamoja na masuala mengine, kujenga uchumi wao.
Akiwa Moshi Mjini jana, pamoja na masuala mengine alisema wanaotekeleza kampeni ya 'No reforms, No election' wanajifurahisha kwa sababu uchaguzi uko palepale.
"Hata mngepost comments mamilioni na mamilioni ya ' No reforms, No election' uchaguzi uko palepale, haisaidii hata wewe njoo pale tukiweka post wewe njoo weka haisaidii, uchaguzi hausogezwi utafanyika kama ulivyopangwa,” alisema.
Kesho ziara hiyo itaendelea wilayani Same ambako ataanza kwa kusalimia wananchi eneo la Same Mashariki kisha kufanya mkutano wa hadhara Same Mjini.