Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makalla: Hai msirudie makosa, sumu haionjwi

Muktasari:

  • Jimbo la Hai lilikuwa chini ya Freeman Mbowe wa Chadema, kabla ya CCM kuchukua uongozi mwaka 2020.

Hai/Arusha. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amewasihi wananchi wa Jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro kutorudia makosa ya miaka ya nyuma kwa kuchagua upinzani, akibainisha kuwa tangu jimbo hilo liongozwe na CCM, mafanikio yanaonekana.

Makalla ametoa wito huo leo Jumapili Juni 8, 2025, alipowahutubia wananchi wa Bomang’ombe wilayani Hai, akiwa safarini kutoka Arusha kuendelea na ziara yake katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

Akikumbusha historia ya uongozi wa jimbo hilo, Makalla amesema kwa takribani miaka 20, Jimbo la Hai lilikuwa chini ya Freeman Mbowe wa Chadema, kabla ya CCM kuchukua uongozi mwaka 2020.

Amesisitiza kuwa maendeleo yaliyofikiwa chini ya CCM ni dhahiri, hivyo wananchi wasirudie makosa.

“Nilikuwa Mkuu wa mkoa huu. Wakati jimbo hili lilikuwa chini ya upinzani, maendeleo yalikuwa ya kusuasua. Lakini ndani ya miaka michache ya CCM, mabadiliko ni makubwa. Msirudie makosa, sumu haionjwi mara mbili,” amesema Makalla.

Akigusia sekta ya utalii, amesema ukuaji wa uchumi katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini ukiwamo Kilimanjaro, umetokana na maendeleo ya utalii.

Hivyo, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ubunifu wake uliosaidia kukuza mapato kupitia sekta hiyo.

“Mapato ya utalii yameongezeka sana. Lakini haya yote hayawezekani bila amani. Nawapongeza viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro, hususan Mkuu wa Mkoa, Nurdin Babu kwa kuhakikisha utulivu unaendelea,” amesema.

Akiwa eneo la Usa River mkoani Arusha, Makalla aliwataka Watanzania kujiepusha na viongozi wanaotumia chuki, udini au ukabila ili kupata uongozi, hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.

“Tunapoelekea uchaguzi, kuna maneno mengi na fitina nyingi. Ni muhimu kulinda amani. CCM tunawahakikishia tutashiriki uchaguzi kwa amani. Tukatae viongozi wanaopandikiza chuki au kutaka kuligawa taifa letu,” amesema.

Akizungumzia Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa 2025/2030, Makalla amesema imetokana na maoni ya wananchi na inalenga kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.

“Ilani hii si ya chama tu bali ni ya wananchi. Tumewasikiliza, tumechambua changamoto zao, na tumeahidi kuja na suluhisho. Hii ni ilani bora kuliko zote zilizowahi kuwepo,” amesema.

Katika kuendeleza utalii, Makalla amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kuhakikisha mkoa huo unaendelea kuwa salama ili kuimarisha mapato yatokanayo na sekta hiyo.

“Watalii wakimiminika, mapato yanaongezeka. Na haya yote yanasaidia Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo. Nimeona mwenyewe maonyesho ya utalii yaliyofanyika Arusha, dunia yote ilikuwa pale,” ameongeza.

Amesisitiza kuwa mafanikio ya sasa katika utalii, elimu, afya, miundombinu na maji ni matokeo ya juhudi za serikali katika kutumia rasilimali za nchi kuwanufaisha wananchi.

Mbunge wa Arumeru Mashariki, John Pallangyo amesema zaidi ya Sh51 bilioni zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali jimboni humo katika kipindi cha miaka minne iliyopita, zikiwemo shule mpya 10, madarasa 265 na maboresho katika hospitali ya wilaya na miradi ya maji.

Amesema changamoto kubwa bado ni miundombinu ya barabara, hasa kutokana na jiografia ya eneo hilo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kubainisha kuwa barabara ya njia nne kuanzia Tengeru hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ipo katika mpango wa ujenzi.

Makonda amesema pia kuna mpango wa kuongeza thamani ya mazao ya wakulima na wafugaji wa eneo hilo ili kuhakikisha bidhaa zinazouzwa nje zinatambulika kuwa zimetoka Tanzania.

Kwa upande wake, Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe amesema jimbo hilo limepiga hatua katika sekta za elimu, afya na maji, akitaja mfano wa mradi wa maji wa zaidi ya Sh3.9 bilioni uliosaidia kumaliza uhaba wa maji katika eneo la Bomang’ombe.

“Na ssa tunaendelea na mpango wa kuboresha hospitali ya wilaya, ujenzi wa zahanati nane na shule mpya 10 kwenye jimbo letu,” amesema Saashisha.