Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makalla abadili upepo Kaskazini akisisitiza amani, apangua hoja za Chadema

Muktasari:

  • Aendelea na ziara yake mikoa ya kaskazini kukanusha kile alichokiita upotoshaji uliofanywa na viongozi wa Chadema waliofanya ziara hivi karibuni katiba mikoa hiyo ambapo mbali na kujibu baadhi ya hoja hizo suala la amani ni moja ya masuala amekuwa akisisitiza.

Arusha. Ni mwendo wa bandika bandua, ndivyo unavyoweza kusema kuhusu ziara ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, aliye ziarani mikoa ya Kaskazini ambaye anaitumia kujibu sehemu ya hoja zilizoibuliwa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Ziara ya Makalla imeanza kuanzia Juni 4 na inatarajiwa kukamilika Juni 11, ambapo hadi sasa ameshapita katika Wilaya za Babati (Manyara) na Arusha katika Wilaya ya Karatu, Arumeru na Arusha Mjini alipohitimisha kwa mkutano wa hadhara kabla ya kuelekea Kilimanjaro.

Makalla anatarajia kuendelea na ziara hiyo kesho Juni 8 ambapo atasalimia wananchi wa Usariver (Arusha) kisha kufanya mikutano wa hadhara Moshi Mjini, Tarakea (Rombo), Same Mashariki, Same Magharibi na kumalizia kwa mkutano wa hadhara eneo la Himo (Kilimanjaro).
Lengo la ziara hiyo ni kujibu kile alichokiita upotoshaji uliofanywa na viongozi wa Chadema waliofanya ziara hivi karibuni katiba mikoa hiyo, ambapo mbali na kujibu baadhi ya hoja hizo suala la amani ni moja ya masuala amekuwa akisisitiza.

Hivi karibuni Chadema kupitia viongozi wake waakuu wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti (Bara), John Heche, wakiwa katika mikoa ya kaskazini ikiwemo Manyara, walisema licha ya Taifa kuwa na rasilimali nyingi bado wananchi ni maskini.
Akiwa wilayani Simanjiro, Manyara Heche alisema Chadema wakiingia Ikulu watavunja ukuta unazunguko mgodi wa madini ya Tanzanite kwani hauna faida kwa watu wanaoishi eneo hilo zaidi ya kuwatesa.

Hata hivyo Juni 4, 2025 Makalla akiwa ziarani siku ya kwanza wilayani Babati alidai siyo kweli kilichosemwa na Chadema bali uchumi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini umezidi kukua kutokana na sekta ya utalii.

Amesema filamu ya Royal Tour, iliyoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeweza kuongeza mapato ya utalii na mzunguko wa fedha katika mikoa hiyo.

“Mikoa ya Kaskazini jambo kubwa lililofanywa ni kukuza utalii, Royal Tour imefanya kazi kubwa katika mikoa hii na mapato ya utalii yameongezeka nyie mnafaidika nayo,” amedai Makalla akiwaambia wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Makalla amesema mambo yanayoendelea yamechagizwa kutokana na wananchi kuendelea kuwa na imani na CCM, akisema ahadi ya chama hicho tawala ni kuwatumikia Watanzania kwa kuwaletea maendeleo.

Akiwa wilayani Karatu, alisema upatikanaji wa maji Karatu Mjini ni asilimia 79 tofauti na miaka 25 ya nyuma ambayo maendeleo katika jimbo hilo yalisuasua,wakati linaongozwa na Chadema.

Kupitia mkutano huo, alimuomba Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kwenda wilayani huyo kushughulikia masuala mawili ambao ni bwawa pamoja na kutatua changamoto iliyopo katika kuruhusu maji ili kusaidia wananchi wa eneo hilo.

Kabla ya kufanya mkutano wa hadhara Karatu, Makalla alisimama na kusalimia wananchi katika eneo la Mto wa Mbu (Monduli) ambapo pamoja na masuala mengine alieleza kuwa ilani mpya ya CCM ya mwaka 2025/30 waliyoizindua hivi karibuni imebeba matumaini kwa Watanzania.

Amesema ilani hiyo imebeba masuala muhimu yanayowagusa Watanzania kwani imetokana na tathmini ya ilani iliyopita kwa kufanya utafiti na ushirikishwaji wa wananchi na wadau mbalimbali ili kujua vipaumbele vya Watanzania.

Makalla alieleza ilani hiyo inakwenda kushughulika na suala la ajira, kuimarisha uchumi, miundombinu na changamoto mbalimbali zinazokabili wananchi.

“Ilani hii inaenda kushughulikia na maisha ya Watanzania kwa hiyo ahadi yetu muda utakapofika tutakwenda kuinadi ilani hii ambayo imebeba mustakabali wa watanzania na hakuna chama chenye ilani nzuri zaidi ya CCM,” amesema.

Pamoja na masuala mengine Katibu huyo aliwaomba Watanzania kuendeleza mshikamano na kulinda amani nchini kwani mafanikio yaliyopatikana nchini siri yake ni msingi wa amani.
“Wapo watu wangependa kwa vurugu zao, chuki zao Tanzania isiwe na amani,nataka niwahakikishie nchi yetu iko mikono salama chini ya uongozi wa Rais Samia, mafanikio haya katika utalii ni matokeo ya amani na usalama wa Tanzania,” amesema.

Makalla akizungumza na wananchi wa eneo la Kisongo (Arumeru), amewataka Watanzania kuwakataa wanasiasa wachochezi wasiopenda amani na kutambua kuwa chama hicho ndiyo mwasisi wa amani na kitaendelea kulinda amani nchini kwa wivu mkubwa.

“Muwakatae wanasiasa wachochezi wasiopenda Mkoa wa Arusha usiwe na amani na CCM ndiyo mwasisi wa msingi wa amani na tunaahidi tutailinda amani kwa wivu mkubwa,”

Akizungumzia miradi mbalimbali ya maendeleo, Makalla amesema katika Jimbo la Arumeru Magharibi, miradi mbalimbali imetekelezwa kupitia ilani na kuwa katika maeneo yaliyobakia yataendelea kutekelezwa ikiwemo sekta ya maji.
Akiwa jijini Arusha, Makalla amemtaka Heche kuacha kuhoji mambo ya ndani ya CCM.

“Nimesoma katika mtandao Heche yuko Morogoro anasema hawa CCM wametoa ratiba yao ya uchukuaji fomu hadi kwenye Tume, walijuaje..Hee! Wewe hugombei, chama chako hakiko kwenye mchakato, unafuatilia ratiba ya ndani ya CCM inakuhusu nini?
“Kila chama inatoa ratiba yake ya ndani na kuweka maoteo kwamba ikitokea wakati huu mpaka huu lakini ni ratiba ya ndani ya chama chetu, haikuhusu wewe Heche kaa upumzike tukutane 2030,”amesema.

“Na taarifa nilizonazo wamefanya uamuzi wa kutoshiriki uchaguzi lakini wanahangaika kweli,na wenyewe wafunguliwe washiriki uchaguzi,walidhani wanatania imekuwa kweli imekula kwao,” amesema Makalla.

Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye alisema kutokana na juhudi za uchapakazi za Rais Samia, wajumbe wa CCM hawakuwa na wasiwasi kumpitisha awe mgombea urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba.

“Ametekeleza yote mpaka leo watu wanafungua biashara hakuna anayenyang’anywa wala kudhulumiwa na Serikali, amerudisha utulivu, amani na tumaini kwa Watanzania,” amesisitiza.

Mchungaji Peter Msigwa amesema Tanzania ipo salama chini ya CCM na kuwataka wawapuuze wapinzani, akidai ni wababaishaji walioshindwa kujenga hoja.

Kesho Juni 8, Makalla ataendelea na ziara yake mkoani Kiliamanjaro hadi Juni 11, 2025 atakaophitimisha.

Awali, Chadema wakiongozwa na Heche na Katibu Mkuu wa Chama hicho, John Mnyika na viongozi wengine walikuwa katika ziara mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga katika operesheni ya ‘No Reforms, No Election’, iliyoanza Mei 28 hadi Juni Mosi, 2025.