Makalla awasihi Watanzania kuwakataa wanasiasa wachochezi

Muktasari:
- Makalla amewaomba Watanzania kuendelea kudumisha amani ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kukuza sekta ya utalii hasa katika mikoa ya kanda hiyo ya Kaskazini.
Arumeru. Kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, utakaofanyika Oktoba 2025, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amewataka Watanzania kuwakataa wanasiasa wachochezi wasiopenda amani.
Pia, amesema kwa kutambua umuhimu wa amani, chama hicho ndiyo mwasisi wa amani na kitaendelea kulinda amani nchini kwa wivu mkubwa.
Makalla ameyasema hayo leo Ijumaa Juni 6, 2025 wakati alipopita kusalimia wananchi katika eneo la Kisongo, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, akiwa njiani kuelekea mjini Arusha kwa ajili ya mkutano wa hadhara, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika mikoa ya Kaskazini ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro.
Akizungumza na wananchi hao, Makalla amewaomba Watanzania kuendelea kudumisha amani ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kukuza sekta ya utalii hasa katika mikoa ya kanda hiyo ya Kaskazini.
“Muwakatae wanasiasa wachochezi wasiopenda Mkoa wa Arusha usiwe na amani na CCM ndiyo mwasisi wa msingi ya amani na tunaahidi tutailinda amani hii kwa wivu mkubwa.
“Maendeleo hayana itikadi, iwe miradi ya maji, umeme na zahanati au nyingine, ukienda kupata huduma huulizwi wewe ni Chadema au CCM. Niwaombe kuelekea uchaguzi huu, tuendelee kudumisha amani.
Akizungumzia miradi mbalimbali ya maendeleo, Makalla amesema katika Jimbo la Arumeru Magharibi, miradi mbalimbali imetekelezwa kupitia ilani na kuwa katika maeneo yaliyobakia yataendelea kutekelezwa ikiwemo sekta ya maji.
“Utekelezaji mzuri wa ilani ndiyo uliwafanya mchague CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa japo yapo mambo yaliyoelezwa na mbunge, kuna alama katika elimu, maji, japo changamoto zipo,” amesema.
“Kuna changamoto ya maji hapa, Waziri wa Maji atakuja katika jimbo hili kuangalia wapi kuna changamoto ya maji, akitoka Karatu atakuja hapa. Ni kijana wenu mchapakazi, mwelekezeni wapi kuna changamoto za maji ili zitatuliwe. Niwaombe wana Arumeru tuendelee kushirikiana, tuna safari ndefu ya kushughulika na changamoto za wananchi,” ameongeza.
Awali, Mbunge wa Arumeru Magharibi, Noah Lembris amesema katika kipindi cha miaka mitano, jimbo hilo limepata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo katika sekta ya afya, elimu na maji.
“Kwa mfano, katika hospitali yetu ya wilaya, tumepata Sh900 milioni kwa ajili ya ujenzi wa majengo manne, likiwemo jengo linalohudumia wagonjwa kutoka nje na maabara. Serikali imefanya kazi kubwa sana kiasi kwamba katika uchaguzi huu, Rais Samia Suluhu Hassan hana sababu ya kutopata kura, utekelezaji wa ilani ni mkubwa katika jimbo hili,” amesema.