Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kishindo mkutano mkuu maalumu wa CCM

Muktasari:

  • CCM inatarajia kufanya Mkutano Mkuu Maalumu Mei 29-30, 2025 jijini Dodoma, ambapo itazindua Ilani mpya ya Uchaguzi 2025–2030, kufanyika marekebisho ya Katiba na kuwekwa jiwe la msingi la jengo jipya la makao makuu. Wajumbe 2,700 wanatarajiwa kuhudhuria, huku nafasi ya Katibu Mkuu mpya ikisubiriwa.

Dodoma. Chama cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kufanya Mkutano Mkuu Maalumu wa Taifa kuanzia Mei 29 hadi Mei 30, 2025, jijini Dodoma, ambao pamoja na mambo mengine, utahusisha uzinduzi wa Ilani mpya ya Uchaguzi ya mwaka 2025–2030, sambamba na kufanya marekebisho muhimu ya Katiba ya chama.

Akizungumza leo, Jumamosi Mei 24, 2025, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, amewataka wananchi kutumia fursa ya uwepo wa watu zaidi ya 2,700 jijini Dodoma wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho kujipatia kipato.

"Iwapo wewe ni bodaboda, mama lishe, mmiliki wa hoteli, mtoaji wa huduma za vinywaji, au mfanyabiashara wa sare za chama, kila mmoja ana nafasi ya kufaidika na uwepo wa mkutano huu. Kuanzia Mei 29 hadi 30, tunakwenda kusimamisha nchi.

"Wote tutakuwa hapa Dodoma, ninawakaribisha wote, usipite, nchi itakuwa hapa, Tanzania yote itakuwa hapa kwa hiyo ni fursa kwa Wanadodoma kutumia mkutano huu,” amesema.

Makalla amesema mkutano huo utatanguliwa na vikao vya juu vya chama, ambapo Kamati Kuu ya CCM itakutana Mei 26, 2025, ikifuatiwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kitakachofanyika Mei 28.

Amesema miongoni mwa ajenda kuu za mkutano huo utakaohudhuriwa na wajumbe wapatao 2,700 ni kupokea na kujadili utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya miaka mitano kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020–2025 inakaribia kumaliza muda wake, hivyo mkutano huo utakuwa fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana chini ya ilani hiyo pamoja na kuwasilisha dira mpya ya maendeleo ya Taifa kwa miaka mitano ijayo.

“Hiki ndicho kitendea kazi na mkataba wa chama cha siasa kinapoingia katika kampeni za uchaguzi, kinawaahidi wananchi ili kitakapochaguliwa basi ilani hiyo ndiyo mkataba na wananchi,” amesema.

Amesema wameanza kwa kufanya tathmini ya nini walichoahidi katika ilani iliyopita na vitu vilivyotekelezwa.

Makalla amesema katika kutengeneza ilani mpya wamefanya utafiti kwa kuhusisha maoni ya asasi za kiraia, wananchi na watu mbalimbali kuona vipaumbele, mahitaji ya wananchi kwenye ilani hiyo.

“Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025 itakayozinduliwa, itaenda kukonga nyoyo za Watanzania na kwamba kwa lugha rahisi yajayo yanafurahisha,” amesema.

Pia, amesema mkutano huo utafanya marekebisho madogo ya Katiba ya chama hicho, na sambamba na hilo, utafanyika uwekaji wa jiwe la msingi la jengo jipya la makao makuu ya CCM, hafla iliyopangwa kufanyika Mei 28.

“Tunajenga jengo la makao makuu ya CCM upande wa pili wa jengo hili, chama chetu ni kikubwa kinaendelea kukua siku hadi siku, sasa kina wanachama milioni 11,” amesema.

Amesema ili kuwa na uwezo wa kuhudumia vizuri wameona kuwa jengo la makao makuu ya CCM maarufu kama ‘White House’ ni dogo, hivyo wameona ni vyema wawe na jengo la kisasa lenye hadhi ya chama kikubwa cha kisiasa.

Mkutano huo unafanyika wakati CCM imeongeza idadi ya wajumbe watakaoshiriki katika kura za maoni za uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi.

Marekebisho hayo yanahusisha nafasi za ubunge, udiwani, wawakilishi pamoja na nafasi za viti maalumu vya wanawake, kwa lengo la kuongeza uwakilishi na ushiriki wa wanachama katika mchakato wa kidemokrasia ndani ya chama.

Pia, mkutano huo unafanyika katika kipindi ambacho CCM tayari imepitisha wagombea wake wa nafasi za juu za uongozi kwa uchaguzi mkuu ujao. Rais Samia Suluhu Hassan, ameteuliwa tena kuwania urais kwa tiketi ya CCM, akiwa na mgombea mwenza Dk Emmanuel Nchimbi. Dk Nchimbi ni Katibu Mkuu wa CCM.

Kwa upande wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameidhinishwa tena kuwania nafasi ya urais kwa kipindi kingine.


Nafasi ya Katibu Mkuu

Kwa sasa, CCM hakijatangaza hadharani jina la mtu atakayechukua nafasi ya Dk Nchimbi kama Katibu Mkuu wa chama hicho, baada ya uteuzi wake kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu Oktoba, 2025.

Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa mgombea mwenza na Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, baada ya Makamu wa Rais Dk Philip Mpango kuwasilisha ombi la kupumzika kutokana na umri wake.


Maandalizi ya Mkutano Mkuu

CCM imesema ‘itasimamisha’ shughuli za nchi kupitia Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho, utakaofanyika Mei 29 na 30, mwaka huu, katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.

Katika barabara inayoelekea kwenye ukumbi wa mkutano, bendera za CCM zimepambwa kwa wingi, zikipeperushwa kandokando ya njia, huku ndani ya ukumbi viti vikiwa vimefunikwa kwa vitambaa vyenye rangi za chama hicho pamoja na maandishi ya CCM, yakiongeza haiba ya tukio hilo maalumu.

Ukumbi huo pia umepambwa na mabango yenye kaulimbiu mpya ya chama hicho inayosema: "Kazi na utu, tunasonga mbele."