Makalla awajibu Chadema akianza ziara ya siku saba Kaskazini

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla
Muktasari:
- Akiwa wilayani Babati, Mkoa wa Manyara leo Jumatano Juni 4,2025, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema uchumi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini umekua kutokana na sekta ya utalii.
Babati. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla ameanza ziara ya mikoa ya kanda ya kaskazini kwa lengo kujibu kile alichokiita upotoshaji wa uliofanywa na viongozi wa Chadema waliofanya ziara hivi karibuni.
Hivi karibuni Chadema kupitia viongozi wake wakuu wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti hicho (Bara) John Heche na Kaimu Katibu Mkuu wake John Mnyika wakiwa mikoa kaskazini ikiwemo Manyara walisema kuwa licha ya Taifa kuwa na rasilimali nyingi bado wananchi ni maskini.
Akiwa wilayani Simanjiro, Manyara Heche alisema Chadema wakiingia Ikulu watavunja ukuta unaozunguka mgodi wa madini ya Tanzanite kwani hauna faida kwa watu wanaoishi eneo hilo zaidi ya kuwatesa.
Hata hivyo, leo Jumatano Juni 4,2025 ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Manyara, Makalla amedai si kweli kilichosemwa na Chadema bali uchumi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini umezidi kukua kutokana na sekta ya utalii.

Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi CCM, Amos Makalla akielekea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Babati Mkoa wa Manyara leo Jumatano Juni 4, 2025 ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara katika mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro.
Amesema filamu ya utalii ya Royal Tour, iliyoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeweza kuongeza mapato ya utalii na mzunguko wa fedha katika mikoa hiyo.
“Mikoa ya Kaskazini jambo kubwa lililofanywa ni kukuza utalii, Royal tour imefanya kazi kubwa katika mikoa ya Manyara Arusha, Kilimanjaro na mapato ya utalii yameongezeka nyie mnafaidika nayo,” amedai Makalla akiwaambia wananchi waliohudhuria mkutano huo.
“Watalii wanavyokuja mzunguko wa fedha unaongezeka yote haya ni jitihada za Rais Samia aliyekuja na ubunifu aliyetumia muda mwingi kuigiza royal tour kuitangaza Tanzania leo tunafaidika na mapato ya utalii.”
Makalla amesema mambo yanayoendelea yanachagizwa kutokana na wananchi kuendelea kuwa na imani na CCM, akisema ahadi ya chama hicho tawala ni watumikia Watanzania kwa kuwaletea maendeleo.
“Natambua yamefanywa mambo mengi yawezekana yakawa yamebaki kidogo nataka niwahakikishie CCM ndiyo mwenye kumaliza changamoto hizo, hakuna chama mbadala,”
“Katika vyama vyote vya siasa Tanzania ni CCM pekee ina wajibu na dhamana ya kuwaletea wananchi maendeleo,”amesema.
Mwenezi huyo amewahakikishia wananchi wa Manyara kuwa mwaka huu CCM kitasimamisha wagombea safi na atakayeshinda atatangazwa mshindi.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye amesema kutokana na juhudi za na uchapakazi wa Rais Samia, wajumbe wa CCM hawakuwa na wasiwasi kumpitisha awe mgombea urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba.
“Ametekeleza yote mpaka leo watu wanafungua biashara hakuna anayenyang’anywa wala kudhulumiwa na Serikali, amerudisha utulivu amani na tumaini kwa Watanzania.”
“Tulikuwa tumefungiwa milango nje hakuna mwekezaji aliyekuwa anakuja nchi hii, ila hali imerejea na kumekuwa na uhusiano mzuri kimataifa,” amesema.
Naye Mchungaji Peter Msigwa amesema Tanzania ipo salama chini ya CCM na kuwataka wawapuuze wapinzani, akidai ni wababaishaji walioshindwa kujenga hoja.
“Wamepoteza dira ni kama chombo kilichopo angani kisichojua kinaenda kutua wapi, CCM inashughulika kutatua matatizo ya watu kuanzia Rais hadi wasaidizi wake,” amesema Mchungaji Msigwa.
Mwenyekiti wa wabunge mkoa wa Manyara na Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amewataka wapinzani kutambua kuwa siri ya CCM kushinda ni moja tu ambayo ni kuendelea kuwa mtetezi wa kuaminika wa haki za wanyonge.
Amesema Serikali imetekeleza mradi wa maji Sh42 bilioni kutoka Mto Ruvu kwa ajili ya wafugaji ambao unahudumia kata sita zilizopo wilayani Simanjiro na kupunguza changamoto kwa wafugaji wa ukanda huo.