Prime
Makalla alivyotumia siku sita kuijibu Chadema Kanda ya ziwa

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla.
Dar es Salaam. Ni mwendo wa kujibu mapigo, ndivyo unavyoweza kusema kuhusu ziara za Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla akiitumia kujibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Ziara hiyo aliyoifanya kuanzia Mei 18 hadi Mei 23,2025 katika mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa (Mwanza, Kagera, Geita, Simiyu na Shinyanga), ilikuja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kifanye ziara yake ya siku 12 kupiga kampeni ya No reforms no Election katika mikoa hiyo pia.
Makalla alifanya ziara hiyo, kwa kupita kila eneo walilopita Chadema kwa lengo la kuweka mambo sawa akitumia msemo wa ‘Ukweli na uongo ni sawa na mafuta na maji, lazima vijitenge.’
Miongoni mwa hoja zilizoibuliwa katika ziara ya Chadema ni Serikali kupuuza mikoa ya kanda ya ziwa, umasikini, wachimbaji madini kutothaminiwa na hawajanufaiki na wananchi wa mikoa yenye dhahabu hawana maisha mazuri.
Hoja nyingine ni ili iliyodaiwa na Chadema kuwa Serikali imeshindwa kuwekeza katika kilimo hasa cha umwagiliaji, jambo linalofanya wakulima wa mikoa ya kanda ya ziwa kutegemea mvua, pia Serikali kuwapuuza wakulima wa mazao ya pamba na kahawa.
Katika ziara hiyo, viongozi Chadema walijigawa katika makundi mawili, kundi la kwanza liliwajumuisha katibu mkuu wa zamani wa chama hicho, Dk Wilbrod Slaa, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha), Suzan Lyimo na kiongozi wao alikuwa Heche (John-Makamu mwenyekiti Bara).
Kundi la pili liliongozwa na Katibu Mkuu, John Mnyika sambamba na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chma hicho, Godbless Lema, huku viongozi mbalimbali wa kanda hizo nao walikuwa wakijigawa kwenye makundi hayo na mikutano ilikuwa ikifanyika kuanzia asubuhi.
Ingawa Makalla alikuwa peke yake katika ziara yake, lakini aliwatumia na kuambatana na makada wapya wa CCM waliokuwa viongozi wa Chadema Kanda ya Victoria (yenye mikoa ya Mwanza, Kagera, Geita), kujibu mashambulizi ya maneno yaliyosemwa na kina Heche, Mnyika na Mahinyila kule walikopita.
Ziara ya Makalla ilianzia mkoani Kagera na kuishia Shinyanga, kama ambavyo Chadema walifanya, ingawa mwenezi huyo wa CCM hakufika mkoani Mara, alisema anauacha kiporo.
Akiwa mkoani Kagera, Makalla alisema Serikali imejitahidi katika kuhakikisha bei ya kahawa inakuwa kubwa akisema hivi sasa inauzwa Sh6,000 kutoka Sh1,000 bei ya awali, akiwataka wananchi wa mkoa kupuuza maneno ya watu wanaosema hakuna kilichofanyika.
“Mtu anakuja hapa, hajui hata shamba au mti wa kahawa unafananaje anakwambia Kagera hakuna maendeleo mmetekelezwa hakuna mtu anayatetea au kuwatafutia soko la kahawa, wapuuzeni hawa,”alisema Makalla.
Kuhusu hoja ya madini, aliwaambia wananchi wa Geita kwamba Serikali inawajali na kuwathamini wachimbaji hasa wadogo, sio kwa mkoa huo bali hata katika mikoa mingine.
“Azma ya CCM ni kuhakikisha kuwajali wachimbaji wadogo kwa kuwekea utaratibu bora ili wawe wachimbaji wakubwa na kukuza uchumi. Mtu asiyekaa Geita, ndio anasema wachimbaji wameachwa si kweli hao, hawana takwimu wapuuzeni.”
“Wengine wanasema Mkoa wa Geita una rasilimali za madini lakini hauna maendeleo, si kweli jambo nyie ndo mashahidi Serikali imefanya mambo makubwa, Geita hii ni tofauti na miaka iliyopita,”alisema Makalla.
Katika ziara hiyo, Makalla aliyekuwa akijifananisha na jeshi la mtu mmoja kwa kujibu mashambulizi ya viongozi wa Chadema, aliwahakikisha wananchi wa Mkoa wa Mwanza kuwa Serikali ya CCM ndio yenye dhamana ya kutatua kero mbalimbali ikiwemo ya miundombinu kwa wananchi.
Alisema changamoto zao zinafahamika na zinafanyiwa kazi awamu kwa awamu wasiwe na wasiwasi, wasisumbuke na maneno ya upinzani wanaosema mikoa ya kanda ya ziwa ukiwemo wa Mwanza umeachwa.
Mwenezi huyo alitolea mfano kukamilika kwa daraja la JP Magufuli ‘Kigongo-Busisi ‘ ambalo liliasisiwa na hayati John Magufuli, lakini chini ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ujenzi huo umekamilika ukitarajiwa kuzinduliwa Juni 19, 2025.
Zao la pamba
Kuhusu zao la pamba, Makalla aliwaambia wananchi wa Simiyu ambao ndio wanaongoza kwa uzalishaji kwamba, Serikali itaendelea kuboresha mazingira yao ili kuhakikisha wanafanya kilimo chenye tija.
“Hao wanaopita hawajui nyinyi ni wachapakazi, wanasema eti ni masikini hamna soko la pamba, msiwasikilize wao ndio masikini kwa sababu wakimaliza mikutano yao wanaendesha ‘tone tone’ (harambee ya kuchangia chama),” alisema kiongozi huyo.
Makalla alisema miaka mitatu iliyopita, bei ya kilo moja ya pamba ilikuwa ikiuzwa Sh800, sasa hivi bei imepanda na kufikia Sh 1,200 kwa kilo moja, hatua ambayo ni ongezeko la kuwajali wakulima wa zao hilo.
Amewataka wananchi wa Simiyu na Shinyanga kuwapuuza wapinzani kwa sababu CCM inatambua kuwa mikoa hiyo inapiga hatua kubwa za maendeleo, ndiyo maana Serikali imetoa fedha za kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo uwanja wa ndege na bonde la mpunga la Masela ili kuwezesha kilimo cha umwagiliaji.
Alichokisema mchambuzi
Akizungumzia mwenendo kati ya CCM na Chadema, mchambuzi wa siasa Dk George Kahangwa amesema sio mara ya kwanza kutokea kwa chama kimoja kufanya mikutano ya hadhara kisha kingine kwenda kujibu mapigo ili kuweka mambo sawa.
“Unapokuwa na mshindani au yanapotokea matukio fulani yanayoathiri taasisi, kuahiribu taswira ya taasisi yako unawajibu kuhakikisha unalinda taasisi yako. Inawezekana CCM wanahisi Chadema wamekwenda wamezungumza, hivyo watu wa maeneo hayo wamepata mtizamo fulani kuhusu chama tawala.
“Ndio maana sasa CCM imekwenda kufanya ziara huko, ili kuweka mambo sawa, ingawa haina uhakika sana kwamba itafanya kazi kwa muda gani, unaweza ukafanikiwa au usifanikiwe. Lakini inawezekana ukafanikiwa kwa kiwango fulani,” amesema Dk Kahangwa.
Amefafanua kuwa kupita na kufanya ziara haimzuii yule aliyeamua kuendelea kushikilia msimamo wake, lakini si njia pekee inayotosha bali kinachoweza kusaidia ni kuonyesha kwa ushahidi kwamba kilichosemwa kipo tofauti, huku ukionyesha ukweli.