Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasira: Uhuru wa kutoa maoni si kutukana wengine

Muktasari:

  • CCM kupitia kwa Makamu Mwenyekiti Bara, Stephen Wasira, kimesisitiza kuwa demokrasia si ruhusa ya kutoa maneno ya matusi au kutukana wengine, kwamba demokrasia ni haki ya kuzungumza kwa huru na kueleza maoni kwa heshima na adabu.

Songea. Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema kuwa uwepo wa demokrasia na uhuru wa kutoa maoni haupaswi kuchukuliwa kama ruhusa ya kuvunja sheria au kutenda mambo yanayokiuka misingi ya maadili na heshima katika jamii.

Amesema kuwa uwepo wa maridhiano nchini hauwezi kuchukua nafasi ya sheria, na kwamba ni lazima sheria za nchi zizingatiwe na kufuatwa na kila mmoja bila kujali hali ya kisiasa au maelewano yaliyopo.

Wasira amesisitiza kuwa lengo la uhuru wa kutoa maoni ni kuruhusu watu kueleza mawazo yao kwa uhuru huku wakizingatia sheria zilizowekwa, ili kuhakikisha jamii inaishi kwa amani bila bughudha, na kuondoa uwezekano wa mtu mmoja kumdhulumu au kumuonea mwingine.

Wasira ameyaeleza leo Juni 12, 2025 alipokuwa akizungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali wa CCM wakiwemo mabalozi wa shina katika Jimbo la Peramiho, wilayani Songea mkoani Ruvuma.

"Siku hizi ukisoma mitandao eti matusi ndio demokrasia, eti matusi ndio uhuru ah! Uhuru wa kutukanana sasa hapo tumekosea njia, ungekuwa uhuru wenyewe ni wa kutukanana tungeutafuta wa nini, tulitafuta uhuru ili utusaidie kujenga watu pamoja kuleta amani katika nchi na kusimamia maendeleo yao.

"Uhuru ni kutoa maoni, uhuru ni kufuata sheria maana unaweka sheria ambazo zinaifanya jamii iishi pamoja bila ya bughudha ili kuondoa mtu asimuonee mwingine, lakini hata kutukana ni kosa la jinai ukisoma sheria za Tanzania," amesema.

Kiongozi huyo amesema, siku hizi dunia imeanza kutoa tafsiri nyingine ya uhuru, kwamba kutukanana sana kwenye mitandao ya kijamii ndio uhuru.

"Hebu niulize wazee watuambie hivi huku katika mila na utamaduni watoto walikuwa wanatukana baba zao, walizuiwa na nani, walizuiwa na utamaduni si ndio, walikuwa wanamtukana mama yao...walikuwa wamejiwekea utaratibu tofauti na demokrasia ya sasa...

"Mtoto hawezi kusema baba naye amezidi tupige kura kupata baba mwingine, hata akiwa mkorofi wanasema ah! baba naye hata akiwa mlevi wanasema baba naye karudi leo kayanywa, lakini hawasemi uongozi wake unakoma wa ubaba, hapo ndipo tulipoanzia.

"Sasa unapopanua demokrasia, tena unapokuja kwenye kitu kipya kinachoitwa vyama vingi vizuri sana, lakini na vyenyewe vinaweza kuwa tabu sana, lakini hakuna kisichokuwa na tabu jambo kubwa ni kuweka utaratibu ili vyama hivi vifanye kazi kwa kuzingatia katiba na sheria mliyojiwekea," amesisitiza.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Odo Mwisho amesema chama hicho kimejipanga kwa Uchaguzi Mkuu na wanajivunia maendeleo ya mkoa huo chini ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.