Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasira awang’ata sikio wakazi wa Geita kuhusu ardhi

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitashinda uchaguzi mkuu mwaka huu kwa kishindo katika mazingira huru na haki.

Geita. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Geita, kuitumia ardhi yao yenye madini kujinufaisha huku akiwataka kutothubutu kuiuza kwa wanaokuja kama wawekezaji, bali waingie nao ubia.

Wasira ameyasema hayo leo Juni 17, 2025, wilayani Geita, alipozungumza na wananchi na wanachama wa chama hicho kwenye mkutano wa hadhara.

Amesema Serikali imewapa wananchi wa kawaida maeneo ya kuchimba madini na si wawekezaji wa kigeni.

"Tuna changamoto ndogondogo katika uchimbaji wa madini, kuna watu wenye ardhi ambayo ina madini, sheria inasema ukitaka hilo eneo lazima mzungumze na mwenye ardhi na mkubaliane, kama mwenye ardhi hataki fidia au kutoka, basi wakubaliane,” amesema Wasira na kuongeza;

“Sasa kama mtaona mimi ni mshauri wenu, msikubali fidia kwa sababu fidia mtakwenda kunywea pombe mkalala porini, ni bora mshirikiane, yeye anapata na ninyi mnapata," amesema.

Akizungumzia uchaguzi mkuu, makamu mwenyekiti huyo amesema chama hicho kimejiandaa kushinda uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu katika mazingira huru na ya haki.

"Tunawaambia macho kwa macho kuwa tuko tayari kuwashinda, waje wote tutawashinda katika mazingira ya uchaguzi huru na haki," amejigamba Wasira.

Amesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP ) Reli ya Kisasa (SGR), vituo vya afya, hospitali, uboreshaji wa sekta ya elimu pamoja na ujenzi wa daraja la JP Magufuli, utamuwezesha Rais Samia Suluhu Hassan kushinda kwa kishindo Oktoba.

Katika mkutano huo, Rhobi Chacha mkazi wa Katoro, amemuomba makamu huyo kuwasaidia wajane kwa kuwapatia mikopo kwa kuwa waume zao wamepoteza maisha migodini.

"Wanaume wamekuwa shida. Ukibeba mwanaume wa mtu ni shida, lakini ukijiendeleza mwenyewe ni safi. Tunaomba Serikali itusaidie," amesema.


Wasira akiwa Bukombe

Akiwa wilayani Bukombe, Wasira amewaambia wananchi kuwa chama hicho hakitavumilia jaribio lolote la kuvunja umoja wa nchi, na kwamba wanaojaribu kufanya hivyo wamekosea namba.

"CCM kazi yetu moja ni kuendeleza umoja wa Watanzania katika hili hatuna msalie mtume kwa sababu hii ndiyo kazi yetu ya kudumu umoja wetu ndiyo unaotupa amani," amesema.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Wasira amesema CCM itaendelea kutetea wananchi na kuwaletea maendeleo yanayogusa maisha yao.

Makamu huyo Mwenyekiti wa CCM amesema jambo kubwa linalofanywa na chama hicho ni kuleta sera bora za maendeleo ili rasilimali zilizopo nchini ziwanufaishe wananchi wote.

Katika hatua nyingine, Wasira amewatahadharisha wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge waliochaguliwa katika awamu iliyopita kujipima iwapo waliwatumikia wananchi kabla ya kurudi tena kuomba nafasi hizo.

Amesema kama kuna mbunge au diwani ambaye wananchi hawajawahi kumuona jimboni, basi apime kina cha maji, kwani CCM sasa inahitaji wagombea wanaokubalika na wananchi na si wanaotegemea kutoa rushwa.

Akizungumzia suala la rushwa, amewashauri wote wanaotarajia kugombea kuepuka rushwa, kwani hata wakitoa fedha zao hawatapewa nafasi. Badala yake, fedha walizonazo wawekeze kwenye sekta ya kilimo.

Akizungumzia mafanikio ya Wilaya ya Bukombe kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohamed amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan, shule mpya za msingi 20 zimejengwa na sasa wilaya hiyo ina shule 100.

Kwa upande wa madarasa, amesema awali yalikuwepo 600, lakini sasa yamefikia 876, pia, hospitali mpya pamoja na vituo vinne vya afya na majengo ya watumishi yamejengwa.

Wasira yupo mkoani Geita kwa ziara ya siku nne kuanzia Juni 16 hadi 19 akitokea mkoani Ruvuma, ambako nako alifanya ziara kuzungumza na wanachama na viongozi wa CCM kupitia mikutano ya ndani akiinadi CCM kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.