Viongozi wengine Chadema Dar watimka, watangaza kugombea ubunge

Muktasari:
- Viongozi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameendelea kutangaza kujiondoa ndani ya chama hicho na sasa ni baadhi ya viongozi wa kanda ya Pwani na Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Bado hamahama ya wanachama ndani ya Chadema imeendelea kushika kasi baada ya makada wengine watano kujiondoa huku wakisema wanakwenda kutafuta majukwaa mengine ili wapate nafasi ya kuwawakilisha wananchi wao kwenye vyombo vya kufanya uamuzi.
Wanachama waliojiengua leo Jumatano, Mei 14, 2025 ni Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa kichama Kinondoni, Henry Kilewo na Mweka Hazina wa chama hicho kanda ya Pwani, Patrick Assenga ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Segerea.
Wengine ni aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Moza Ally na miongoni mwa waasisi wa Chadema Digital ambaye alikuwa mgombea wa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bawacha-Bara, Glory Tausi na Asha Abubakari ambaye alikuwa Katibu wa Chadema Wilaya ya Segerea.

Waliokuwa wanachama wa Chadema wakiwa wameshikana mikono baada ya kutangaza kujitoa katika chama hicho leo Jumatano Mei 14, 2025 baada ya mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Katika maelezo yao, Kileo na wenzake wamesema wanakwenda kugombea ubunge kwenye maeneo yao katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Uamuzi wa kujiondoa ndani ya chama hicho ni mwendelezo wa kufanya hivyo kuanzia Mei 7, 2025 kwa waliokuwa wajumbe wa sekretarieti iliyokuwa chini ya utawala wa uenyekiti wa chama, Freeman Mbowe.
Utawala wa Mbowe wa miaka 21 uligota Juni 22, 2025 baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi yakimpa ushindi Tundu Lissu.
Miongoni mwao ni waliokuwa naibu katibu wakuu, Benson Kigaila (Bara), Salumu Mwalimu (Zanzibar), katibu wa sekretarieti, Julius Mwita na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema.
Tangu siku waliyotangaza kina Mrema kujivua uanachama, makada na viongozi mbalimbali wa kanda, mikoa na wilaya wamekuwa wakitangaza kujivua uanachama kwa maelezo yaleyale kwamba Chadema imepoteza mwelekeo, huku tetesi zikieleza huenda Mei, 18, 2025 watatangaza kujiunga na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).
Ingawa mara kadhaa makada hao wanaohama wamekuwa wakijibiwa na uongozi uliopo madarakani kwamba hawana hoja za msingi za kufanya hivyo bali wanaondoka kwa lengo la kusaka vyeo.
Makada wengine wametangaza kujivua uanachama wakisema kitendo cha chama hicho kutokuweka dhamira ya kushiriki uchaguzi mkuu kimeondoka kwenye msingi wa lengo mama la kupigania haki za wananchi.
"Chama chetu kimepoteza uelekeo, demokrasia hakuna na yote yanakuja baada ya G55 kutoa maoni yetu ya kushauri tusisusie uchaguzi, lakini walitupuuza na kutupa majina mbalimbali ya usaliti," amesema Kilewo.
Amesema kwa kuwa wamekuwa tofauti wamekuwa wakitumia matawi kuondoa viongozi ingawa walionya mfumo huo ambao unavuruga katiba ya chama hicho.
"Chuki imekuwa kubwa na inaendelezwa na viongozi wakuu wa chama. Chama hiki kipo kwa ajili ya kusaidia Watanzania na si kunufaisha baadhi ya watu au kuwawekea mabando watu waliopo nje kutukana wanachama," amesema.

Kilewo amesema mambo hayo ametafakari kwa kina baada ya kuona ile dhana ya kujiunga na chama hicho haipo ameona bora kujivua uanachama na kwenda kujiunga na jukwaa lingine.
"Najiondoa uanachama rasmi, naenda kwenye jukwaa lingine la kisiasa na kwenda kugombea ili kuwatumikia wananchi wengine wa Mwanga na tunakoenda hatuendi kuanza upya tunachofanya ni kubadili tu jukwaa kwani mizizi yetu ni ileile, lakini kuanzia sasa si mwanachadema tena," amesema.
Naye Assenga amesema wamefanya kazi kubwa kukipigania Chadema na wamekwepa mishale mingi lengo kuiondoa CCM madarakani.
"Chama hiki kilikuwa cha kidemokrasia lakini baada ya uongozi mpya kuingia hawaruhusu tena watu kuhoji au kushauri, tunaokuja na mawazo ya kushauri tusiwaogope CCM twende kwenye uchaguzi na si kuwakimbia tunapuuzwa," amesema Assenga.
Assenga amesema Chadema imepoteza uelekeo na amefikiri kwa ufasaha hakiwezi kwenda mbele.
"Natangaza rasmi kujivua uanachama na nafasi zangu zote naenda kwenye jukwaa lingine na kuna wenzetu wako nyuma yetu wanakuja, naenda kujiunga na jukwaa lingine la kisiasa," amesema.
Kwa upande wake, Moza Ally amesema akiwa kama kijana mwenye maono chanya na kuzingatia hali ya kimaisha na Katiba inayoruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa: "Nimetafakari kwa kina baada ya kutoka hadharani kuunga mkono waziwazi msimamo wa chama wa No reforms, no election nimeona kimeshindwa kunipa mbinu ya kuzuia uchaguzi.
“Nikaona nisisaliti dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania kwenye vyombo vya maamuzi."
Moza amesema shabaha yake ni kugombea na kuwatumikia wananchi wa Kinondoni hivyo ameamua kwenda kwenye jukwaa lingine ili awatumikie katika uchaguzi ujao.
"Nitakapokwenda kwenye jukwaa lingine bila kujali naomba mkaniunge mkono nahitaji kwenda kupaza sauti kwa kuwawakilisha kwenye vyombo vya uamuzi ili niwatumikie," amesema.
Mwanzilishi wa Chadema Digital, na mtia nia wa Ubunge Morogoro Kusini, Grory Tausi amesema suala la kuzuia uchaguzi kwake anaona halijakaa sawa kwani wanawanyima raia haki kuchagua au kuchaguliwa.
"Siko tayari kushiriki dhambi ya kuzuia haki ya kuchaguliwa, kuchagua na kugombea, nimeona nijivue uanachama na kwenda kwenye chama kingine kitakachotoa nafasi ya mimi kutimiza ndoto yangu," amesema.
Asha Abubakari amesema anaondoka ndani ya chama hicho kwenda kwenye jukwaa lingine linalofuata taratibu na katiba yake.
"Chadema imeacha utaratibu na kuzingatia matakwa ya katiba, chama kinaongozwa kwa matamko zaidi, wanaendesha No reforms, no election lakini hawajawahi kusema hasara za kutokushiriki uchaguzi," amesema Asha
Amesema Chadema kimepoteza dira hakiwezi kuzuia uchaguzi wanawezaje kwenda kwenye vita wakati hata silaha hawana.