Dk Mwinyi ataja anachojutia kutomueleza Charles Hilary

Muktasari:
- Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema haitakuwa vyema viongozi kusubiri hadi mtu afariki ndipo wamzungumzie kwa sifa, bali wawapongeze wakiwa bado hai kwa kazi nzuri wanazozifanya.
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema msiba wa Charles Hilary umemfundisha umuhimu wa kuwatambua na kuwapongeza wafanyakazi wakiwa bado hai.
Amesema anajutia kutomweleza marehemu Charles Hilary kuwa alikuwa mfanyakazi mzuri, mzalendo na mwajibikaji.
Dk Mwinyi ameeleza kwa masikitiko majuto yake kwa kutomwambia mapema marehemu Charles Hilary jinsi alivyokuwa akimthamini na kuvutiwa na utendaji wake wa kazi, na kwamba alikuwa mmoja wa wafanyakazi mahiri na wazalendo kwa Taifa.
Akizungumza leo Jumatano Mei 14, 2025, katika hafla ya kuuaga mwili wa marehemu Charles Hilary iliyofanyika katika viwanja vya Mapinduzi Square, Dk Mwinyi ametumia jukwaa hilo kutoa wito kwa waajiri wote nchini kuwatambua na kuwasifu wafanyakazi wao wanapofanya vizuri wakiwa hai.
“Ndugu zangu katika msiba huu kuna fundisho tunalipata. Fundisho lenyewe ni kwamba tuwe tayari kuwasifu na kuwaambia wafanyakazi wetu wakifanya vyema palepale wanapofanya vema. Tusingoje mpaka mtu ameshatangulia mbele ya haki, ndio tutoe sifa zake,” amesema Dk Mwinyi.
Amesisitiza kuwa haitakuwa vyema viongozi kusubiri hadi mtu afariki ndipo wamzungumzie kwa sifa, bali wawapongeze wakiwa hai kwa kazi nzuri wanazozifanya.

Mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Charles Hilary ukitolewa Kanisa Kuu la Kristo Mkunazini kupelekwa Katika makaburi ya Mwanakwerekwe kwa ajili ya maziko. Picha na Zuleikha Fatawi
Pia, Dk Mwinyi ameahidi kuendelea kumuenzi marehemu Charles kwa kutimiza ahadi na maombi aliyomwachia juu ya familia yake, akisisitiza kuwa uhusiano wao haukuishia kazini bali ulihusu pia mawasiliano ya karibu kuhusu maisha ya kifamilia.
“Kwenye eneo la familia, sikupata nafasi ya kukutana na mke wake wala watoto wake lakini nilikuwa nawajua sababu alikuwa anazungumzia kuhusu wao.
“Naomba nisiseme hapa lakini alinipa ombi linalohusiana na familia yake, tutakuja kuzungumza mimi na ninyi. Lakini ninalipokea, nataka niwahakikishieni kwamba nitaenzi kazi aliyonifanyia kwa kutimiza yale ambayo aliyataka juu ya familia yake,” amesema Dk Mwinyi.
Charles aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu na Msemaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alifariki dunia Mei 11, 2025, jijini Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa Charles alikuwa mchapakazi, mcheshi na mwenye kujitoa kwa kazi, na kwamba Taifa limepoteza mtu muhimu ambaye mchango wake ulikuwa mkubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Kama kuna jambo ninalolijutia, ni kutomwambia Charles mapema. Tumeondokewa na mtu mzuri, mtu mchapakazi, mtu hodari wa kazi yake. Lakini hii ni mapenzi ya Mungu, na sote tupo katika njia hiyo,” amesema Dk Mwinyi.
Dk Mwinyi amesema licha ya changamoto za kazi katika ofisi yake, uwepo wa Charles ulileta utulivu kwa sababu ya ucheshi na ushirikiano wake na wafanyakazi wenzake.
Ameongeza kuwa alimpigia simu mwenyewe Charles Hilary na kumwomba akubali kushika wadhifa wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar, pamoja na kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa upande wake, Msemaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Gerson Msigwa, akitoa salamu kwa niaba ya Serikali, amesema Charles alikuwa mfano bora wa mfanyakazi aliyejitoa bila kujali umri wala hadhi yake kazini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Hamad asema Charles alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha matumizi ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania.
Naye Msaidizi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar, Rakiy Mohammed amesema ofisi hiyo imepoteza mtu muhimu sana kutokana na umahiri, ucheshi na moyo wa kusaidia aliokuwa nao.
“Charles alikuwa mcheshi hata nje ya mazingira ya kazi. Alikuwa akisisitiza kupendana na kuwa wazi, badala ya kuficha mambo moyoni,” amesema Rakiy.
Akitoa salamu kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Mshauri wa Siasa wa Rais, Haji Omar Kheri amesema wanaungana na Rais Mwinyi katika kipindi hiki kigumu, kwani msiba huo ni pigo kubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, aliongeza kuwa viongozi na wanachama wa CCM watamkumbuka Charles kwa umahiri wake katika kusimulia miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali katika kipindi chake cha utumishi.
Nyongeza na Faraja Masinde (Dar es Salaam)