Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wajitokeza kumuaga Charles Hilary Unguja

Wananchi mbalimbali ambao wameshawasili Kisonge kwa ajili ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Charles Hilary. Picha na Zuleikha Fatawi

Muktasari:

  • Licha ya mvua kubwa, wananchi na viongozi wajitokeza kumuaga marehemu Charles Hilary.

Unguja. Licha ya mvua kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mjini Unguja, wananchi na viongozi kutoka sehemu mbalimbali wamejitokeza kwa wingi katika eneo la Kisonge kwa ajili ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Zanzibar na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, marehemu Charles Hilary.

Shughuli hiyo ya kutoa heshima za mwisho inatarajiwa kuongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi.

Hilary alifariki dunia Mei 11, 2025, katika Hospitali ya Mloganzila, jijini Dar es Salaam, na mwili wake uliwasili Zanzibar jana kwa ajili ya maziko.

Viongozi mbalimbali wa dini wakiwa wamewasili katika viwanja vya Kisonge kwa ajili ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar, Charles Hilary. Picha na Zuleikha Fatawi

Enzi za uhai wake, alitambulika kwa mchango mkubwa katika sekta ya mawasiliano serikalini, ambapo alitumikia kwa weledi, nidhamu na uzalendo mkubwa.

Wawakilishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari tayari wamewasili Kisonge kushiriki zoezi hilo la kuaga, wakiongozwa na viongozi wa Serikali pamoja na watu wa kada tofauti walioguswa na msiba huo mkubwa kwa taifa.


Wananchi wakumbuka ucheshi, upendo

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi Digital wamesema watamkumbuka marehemu Hilary kwa haiba yake ya ucheshi, upole na upendo kwa watu wa rika zote licha ya wadhifa wake mkubwa serikalini.

Viongozi mbalimbali wa dini wakiwa wamewasili katika viwanja vya Kisonge kwa ajili ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar, Charles Hilary. Picha na Zuleikha Fatawi

Mohammed Mussa, mmoja wa waombolezaji, amesema: "Nimefika kumuaga kwa sababu nimeguswa sana na kifo chake. Alikuwa mtu wa watu, mwenye upendo wa dhati. Nisingeweza kubaki nyumbani bila kushiriki kumuaga."

Kwa upande wake, Kulpara Ahmed maarufu kama DJ Kulpara amesema Hilary alikuwa rafiki yake wa karibu na kwamba leo amevaa fulana na kofia aliyozawadiwa na Hilary kutoka nchini Cuba kama njia ya kumuenzi.

"Charles alinipa zawadi hii na kuniambia nikivaa nitamkumbuka. Nimevaa leo kumuenzi kwa heshima ya kipekee," amesema kwa hisia.


Sifa, maono ya Hilary

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amemwelezea marehemu Hilary kama kiongozi mwenye maono mapana, mpenda ushirikiano na mwenye moyo wa huruma kwa watu aliowatumikia na waliomzunguka.

Maandalizi mbalimbali yakiendelea katika Viwanja vya Kisonge, Mjini Unguja kwa ajili ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar, Charles Hilary. Picha na Zuleikha Fatawi

"Licha ya nafasi yake kubwa serikalini, alikuwa mnyenyekevu sana. Alikuwa hachoki kushauriana na wenzake, hata mimi mara kadhaa alinitafuta kwa ushauri. Hili ndilo lililomfanya awe bora na tofauti," amesema Msigwa.

Ameongeza kuwa Hilary alikuwa kielelezo cha mchanganyiko wa weledi na ucheshi, hali iliyomfanya afanye kazi kwa ufanisi huku akiwa na mahusiano mazuri na watu wote.

"Alijua kuburudisha na kuelimisha kwa wakati mmoja. Alikuwa si mtu wa kufanya kazi kwa mkazo wa ofisini pekee bali aliweka mazingira rafiki kwa kila mtu aliye karibu naye," amesema.

Msigwa ametoa wito kwa waandishi wa habari kuendeleza misingi ya uandishi uliolenga kuelimisha na kuburudisha jamii, jambo ambalo Hilary alilisimamia kwa dhati enzi za uhai wake.