Trafiki wawili wafariki dunia kwa kupigwa na radi

Muktasari:
- Trafiki wawili wa usalama barabarani wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi katika mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara.
Mirerani. Askari wawili wa usalama barabarani kutoka Kituo cha Polisi Mirerani, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara, wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi wakiwa kazini.
Tukio hilo limetokea wakati askari hao wakiendelea na majukumu yao ya kudhibiti usalama wa barabarani, ambapo ghafla mvua iliyokuwa ikinyesha iliambatana na radi iliyosababisha vifo hivyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Ahmed Makarani akizungumza na Mwananchi Digital leo, Jumatano, Mei 14, 2025, amethibitisha tukio hilo, ambapo askari wawili wa usalama barabarani wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi.

Askari Issa Masud wa kituo cha Polisi Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, aliyefariki dunia kwa kupigwa na radi.
Kamanda Makarani amesema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 13, 2025, katika mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro.
“Askari waliofariki dunia ni Joseph Nyamoko na Issa Masud, ambao walikuwa wakiendelea na majukumu yao ya kusimamia usalama barabarani wakati walipopigwa na radi,” amesema.
Amesema kuwa askari hao walikuwa wakitekeleza majukumu yao ya kawaida ya kazi, lakini walijikuta katika hatari ya maafa wakati hali ya hewa ilivyokuwa mbaya.
Kwa mujibu wa Kamanda Makarani mipango ya kusafirisha miili ya askari wawili inaendelea, ambapo mwili wa Issa Masud utasafirishwa kwenda Pemba na mwili wa Joseph Nyamoko utasafirishwa kwenda Mwanza.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kilimahewa, Andrew Nyambo amesema kuwa askari hao walikuwa wakifanya kazi katika eneo lake na walijulikana kama watu wa kijamii, waliokuwa wakishirikiana na jamii katika masuala mbalimbali.
Nyambo amesema kuwa askari hao walikuwa na uhusiano mzuri na wananchi na hawakuwa na migogoro yoyote na jamii wakiwa nje ya majukumu yao ya kazi.

Joseph Nyamoko askari wa kituo cha Polisi Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, aliyefariki dunia kwa kupigwa na radi.
Amesema kuwa Nyamoko ameacha mke na watoto wawili na Issa ameacha mke na watoto wawili.
Sheikh wa Wilaya ya Simanjiro, Ramia Isanga ameungana na jamii katika kutoa wito wa kuishi maisha yanayompendeza Mungu, akisema kuwa hakuna ajuaye atakufa lini na hivyo ni muhimu kuishi maisha ya huruma na upendo.
"Ndugu zetu hawa wamefariki wakiwa kazini, ghafla tukapokea habari kuwa hawapo nasi tena. Tujitahidi kufuata mafundisho ya Mungu ili tuwe na mwisho mwema," alisema Isanga.
Mkazi wa Mji Mdogo wa Mirerani, Ernest Lukumay, amesema kuwa Nyamoko alikuwa muumini mzuri wa Kanisa Katoliki na atakumbukwa kwa kumcha Mungu, akisema kuwa walishiriki naye katika shughuli za kanisa na harusi yake.
John Daniel, mkazi wa Mtaa wa Kilimahewa, amesema alimfahamu Issa mwaka mmoja uliopita alipohamia kutoka Lindi.
"Issa alikuwa mtu mwema, mpole na mwenye utu. Tunamshukuru Mungu, kwani kifo ni sehemu ya maisha yetu," amesema Daniel.
Elias Sayore, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, amesema kuwa kabla ya askari hao kufariki, mvua ya wastani ilikuwa inanyesha na walikuwa wakimudu kuendelea na kazi zao kando ya mti.
"Radi ilipiga ghafla na kuwadhuru. Awali walikuwa watatu na dada mmoja askari ambaye aliondoka kwenda kutekeleza majukumu mengine," amesema Sayore.