Waliokuwa 'team' Mbowe watema nyongo, wawashangaa waliojiengua

Muktasari:
- Wanawashangaa wenzao wanaojiengua Chadema wakidai kubaguliwa ndani ya chama.
Dar es Salaam. Usemi wa "ukimwaga mboga, namwaga ugali" unaonekana kuchukua sura halisi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kufuatia kuibuka kwa kundi la makada waliowahi kumuunga mkono aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kipindi cha uchaguzi mkuu ndani ya chama hicho, ambao sasa wanawashangaa wenzao wanaojiondoa kwa madai ya kubaguliwa.
Kwa wiki kadhaa zilizopita, Chadema imekumbwa na mfululizo wa wanachama na viongozi kujiondoa, wakiwamo akina Benson Kigaila, John Mrema, Julius Mwita, Salum Mwalimu na Catherine Ruge huku wakitoa sababu mbalimbali ikiwamo ya kudai kubaguliwa kwa sababu walimuunga mkono Mbowe.
Miongoni mwa hoja za kujiengua kwa makada hao ni madai ya kubaguliwa, baadhi wakihusisha makovu ya uchaguzi uliomweka Tundu Lissu madarakani akimshinda Mbowe aliyekuwa akitetea nafasi aliyokuwa akiishikilia ya mwenyekiti.
Fukuto la kujiengua kwa makada.
Wakizungumza na vyombo vya habari leo Jumanne Mei 13, 2025 jijini Dar es Salaam, baadhi ya makada hao wamedai kuwa hakuna ukweli wowote juu ya madai hayo ya kubaguliwa kama wanavyoeleza.

Mwenyekiti wa Wilaya ya Ilala Chadema, Nice Gisunte akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, kuhusu viongozi na wanachama wa chama hicho waliojivua uanachama. Picha na Michael Matemanga
Wamesema hakuna mwanachama anayebaguliwa ndani ya chama hicho, huku wakisema madai hayo ni ya uongo.
Wamesema makada wanaojiengua wanapotosha ukweli na kuendeleza ajenda ya kutaka kukidhoofisha chama chao.
“Hakuna ubaguzi ndani ya Chadema kinachoonekana ni baadhi ya wanachama kushindwa kukubali matokeo ya uchaguzi,” amesema Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Kanda ya Pwani, Evangelina Michael.
Amesema madai ya ubaguzi yanayotolewa na waliokihama chama hayana msingi, kwa sababu hata yeye ambaye alikuwa upande wa Mbowe hajawahi kubaguliwa baada ya uchaguzi kwisha.
“Mimi ni miongoni mwa wanawake waliomuunga mkono Mbowe, lakini sijawahi kubaguliwa. Haya madai si ya kweli. Kinachoendelea ni kiburi na kutokubali matokeo,” amesema Michael.
Ameongeza kuwa hoja nyingine zilizotolewa na waliokihama chama kuwa chama kimeyumba kutoka kwenye misingi yake, si za kweli pia.
Amesema kwani kwa mujibu wa katiba, Chadema bado kinasimama kwenye misingi yake imara iliyojijengea tangu kuanzishwa kwake.
Akitolea mfano wa kampeni ya No Reform No Election, Michael amesema baadhi ya waliotoka kwenye chama ndio waliokuwa mstari wa mbele kuiandaa ajenda hiyo, hivyo si sahihi kwao sasa kuipinga.
“Wengi wao walikuwa kwenye sekretarieti. Walishiriki kuandaa na kuiwasilisha ajenda hiyo kwenye Kamati Kuu na hatimaye kupelekwa kwenye Mkutano Mkuu. Leo kwa sababu hawapo madarakani wanaigeuka, hii haofai,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Ilala, Nice Gisunte ambaye pia alikuwa miongoni mwa waliomuunga mkono Mbowe, amesema hatua ya baadhi ya wanachama kujiondoa inahusishwa na kile alichokiita mradi wa kukidhoofisha chama chao.
“Nilimuunga mkono Mbowe hadharani, niliongoza uchangishaji wa fedha kumlipia fomu, niliratibu kampeni zake miongoni mwa vijana, lakini sijawahi kubaguliwa. Madai ya ubaguzi ni kisingizio tu cha watu wenye nia ya kukihujumu chama,” amesema Gisunte.
Amesisitiza kuwa hoja zinazotolewa na waliokihama chama hazina uzito, na kwamba, wanaoendelea kujiengua walishindwa kukubali kushindwa katika uchaguzi.
Elizabeth Mambosho, kada mwingine aliyemuunga mkono Mbowe, amesema baadhi ya waliokihama walijiona kama viongozi wa kudumu ndani ya chama, hali ambayo sasa inawaumiza baada ya kutopitishwa tena kwenye nafasi walizotaka.
Makada hao wamesisitiza kuwa Chadema ni taasisi inayoongozwa kwa mujibu wa Katiba na si kwa matakwa ya mtu mmoja au kikundi.
Wanaoendelea kuachia ngazi na waliojivua tayari uanachama kuacha kuwapotosha Watanzania na badala yake waseme ukweli wa sababu za kujiondoa kwao.