Mnyika: Chadema hatuna timu Mbowe wala timu Lissu

Muktasari:
- Umoja na mshikamano umetetereka ndani ya Chadema tangu kumalizika kwa uchaguzi wa ndani wa chama hicho uliofanyika Januari 21, 2025 ulioshuhudia aliyekuwa mwenyekiti wake, Freeman Mbowe akiangushwa na aliyekuwa makamu wake, Tundu Lissu.
Mwanza. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amesema makundi yote yaliyoundwa kuunga mkono wagombea wakati wa uchaguzi wa ndani wa chama hicho yalivunjwa baada ya mchakato wa uchaguzi kukamilika.
Akihutubia mkutano wa hadhara eneo la Igoma jijini Mwanza jana, Mei 12, 2025, Mnyika amekana chama hicho kugawanyika katika makundi mawili, moja likimuunga mkono Mwenyekiti Tundu Lissu na lingine lililo upande wa mwenyekiti mstaafu, Freeman Mbowe.
“Makundi yote ya uchaguzi wa ndani wa chama yaliisha baada ya mchakato wa uchaguzi kukamilika; na sasa kuna timu moja pekee ambayo ni timu Chadema,” amesema Mnyika.
Amesema kuna baadhi ya watu wanatumia madai ya makundi ya uchaguzi kujivua uanachama wao wa Chadema, akifafanua kuwa siyo ya kweli kwa sababu chama hicho kimeshachukua hatua kadhaa kushughulikia matatizo yaliyotokana na uchaguzi.

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akihutubia mkutano wa hadhara eneo la Igoma jijini Mwanza. Picha na Peter Saramba
Mtendaji mkuu huyo wa chama amesema kuna vikao na jitihada kadhaa zimeshafanyika ikiwemo kukutana, kuwasikiliza, kujadiliana na kushauriana na waliokuwa na hoja zilizotokana na mchakato wa uchaguzi, lengo likiwa ni kuondoa makundi ndani ya chama hicho.
“Kuna mambo ambayo siwezi kuyaweka wazi hadharani, lakini itoshe tu kusema kazi kubwa imefanyika kupitia taratibu za kiutendaji ambazo pia zimeshirikisha Baraza la Wazee wa chama,” amesema Mnyika.
Bila kuingia kwa undani, Katibu Mkuu huyo amesema; “Wazee wamekutana na Mwenyekiti Tundu Lissu na Mbowe, lengo likiwa ni kutafuta namna bora ya kukiunganisha chama.”
Amesema chama hicho hakitaruhusu mtu au watu kutumia kisingizio cha majeraha ya uchaguzi kuyumbisha umoja na shughuli za chama.
Mnyika amesema ni haki ya kikatiba mtu kujiunga na chama chochote cha siasa na hata kujivua uanachama, hivyo Chadema haina nongwa na makada wake wanaojivua uanachama, lakini siyo sawa wao kutoa madai ya uwepo wa makundi ndani ya chama kuwa ndiyo sababu inayowaondoa.
Amesema Chadema itaendelea kusimamia na kutekeleza kampeni ya kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uongozi utakaorejesha mamlaka ya maamuzi katika sanduku la kura mikononi mwa wapigakura.
“Akitokea mtu miongoni mwetu akitaka kututoa kwenye malengo yetu ya kudai marekebisho ya sheria na mfumo wa uongozi unaotoa haki sawa kwa wote, basi huyo tumweke pembeni sisi tusonge mbele,” amesema Mnyika.
Hata hivyo, mtendaji mkuu huyo amesema iwapo mtu au watu waliowekwa au kujiweka pembeni watajirudi na kuonyesha utayari wa kuendeleza mapambano, chama hicho hakitawafungia milango.
“Atakayejirudi na kuonyesha nia ya dhati ya kuendeleza mapambano ya kudai mabadiliko, huyo tutakuwa naye,” amesema.
Kauli ya Mnyika inakuja huku kukiwa na wimbi la waliokuwa wanachama na makada wa Chadema kutangaza kujivua uanachama kwa kile wanachodai ni kuchoka kubaguliwa kutokana na kumuunga mkono mwenyekiti wa zamani, Freeman Mbowe wakati wa mchakato wa uchaguzi wa ndani.
Baadhi wajumbe wa kundi la G55 wakiongozwa na msemaji wao, John Mrema ndio walifungua pazia la kujivua uanachama wakati wa mkutano wao na waandishi wa habari Mei 7, 2025.
Hadi sasa, makada kadhaa wa Chadema wakiwemo viongozi wa zamani na wa sasa katika ngazi ya wilaya, majimbo, mikoa na kanda wametangaza kujivua uanachama.
Kama ilivyokuwa kwa wenzao wa kundi la G55, karibu wote waliojivua uanachama wa Chadema bado hawajaweka wazi vyama vyao vipya watakavyojiunga navyo kwa kile wanachosema bado wanatafakari.
Hali ya umoja haujarejea ndani ya Chadema tangu kumalizika kwa uchaguzi wa ndani ya chama hicho uliofanyika Januari 21, 2025 na kushuhudia Mbowe akiangushwa na Tundu Lissu aliyekuwa makamu wake kabla ya uchaguzi.